CHAMA cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kimesema hakitarudi nyuma katika mpango wa kutoa mafunzo
ya ukakamavu kupitia kikundi chake cha red brigade.
Chama hicho kimesema, tayari
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), vyote vikiwa miongoni
mwa `vyama vikubwa nchini’, vina vikundi vya aina hiyo.
Mkurugenzi wa
Oganizasheni na Mafunzo Chadema, Singo Benson, ametoa msimamo huo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Tamko la Chadema kuanzisha
mafunzo hayo, limeibua taharuki na kusababisha watu kad
haa akiwamo Rais Jakaya
Kikwete, kutaka mpango huo usitishwe.
LENGO LA MAFUNZO.
Benson alisema lengo la
kuimarisha kikundi hicho, ni kujikinga dhidi ya mashambulizi yanayoelekezwa kwa
viongozi, wanachama na wafuasi wake, ambapo CCM ikitajwa kuwa nyuma ya
mashambulizi hayo.
Alisema Chadema,
imekamilisha maandalizi ya mafunzo yatakayowajumuisha zaidi vijana, ili wapate
mbinu za kujikinga na kuwalinda viongozi wao ikiwa ni pamoja na katika mikutano
ya hadhara.
Hata hivyo, alisema mpango
huo hauhusishi mafunzo ya kijeshi, akidai kwamba mafunzo kama hayo yanatolewa
kwa vijana kupitia kambi maalum zinazoratibiwa na CCM.
MAKAMBI YA CCM.
Benson alidai kuwa kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Igunga mkoani Tabora mwishoni mwa 2011, CCM
iliandaa makambi mbalimbali ya kufundisha vijana mbinu za kijeshi.
“Iweje Chadema tuambiwe kuwa
ni haramu kwa mwaka huu, wakati mwaka jana vijana wa CCM walifanya mafunzo na
paredi ya jeshi ambayo ni hatari kwa nchi,” alihoji.
Alidai kuwa moja ya matokeo
ya kambi za vijana wa CCM kule Igunga, ni kupigwa hadi kuuawa kwa Mbwana Masoud
na Msafiri Mbwambo waliotokea Arumeru Mashariki.
Alidai kuwa matukio hayo
yanajulikana hadi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, lakini
hakuna hatua zilizochukuliwa.
AMGEUKIA MWIGULU.
Benson alisema IGP Mwema
anatakiwa kuanza kuwashughulikia Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba,
kwa madai ya kuwa mmoja wa waasisi wa kuwabebesha vijana silaha za kwenda
kushambulia raia wasiokuwa na hatia.
Hata hivyo IGP Mwema
aliliambia gazeti hili jana kwamba atatoa tamko kuhusiana na sakata hilo
Jumatatu ijayo.
“Kikwete (Rais Jakaya
Kikwete) awaeleze hao vijana wa CCM wanafanyaje hayo mafunzo yao, na wamekuwa
wakitumika kuwapiga viongozi wa Chadema mbele ya polisi na hakuna hatua
zinazochukuliwa,” alisema.
Benson alisema kabla ya
polisi kuanza kuwashughulikia Chadema, wanapaswa kuanzia CCM.
“Sasa Rais Kikwete aseme hao
ni wajasiriamali ama wanajeshi, na kama ni wajasiriamali bunduki walizo nazo ni
za nini,” alihoji Benson.
Hata hivyo, alisema kikundi
chao walichokianzisha kipo kwa mujibu wa kikatiba na kwamba watafundishwa
kulinda haki za Watanzania, kuwalinda viongozi na mikutano ya Chadema.
Alisema mafunzo ya
kuimarisha kikundi cha ulinzi cha Chadema yatanza wiki ijayo katika mikoa
mbalimbali.
Pia, Benson alisema leo,
Chadema wanatarajia kuzindua msimamo wa chama kuhusu rasimu ya Katiba Mpya
katika Shule ya Msingi ya Ukombozi iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam.
UVCCM NAO WAIBUKA.
Kwa upande wake, Jumuiya ya
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), imeshutumu hatua ya Chadema
kuanzisha mafunzo kwa kikundi hicho cha ‘Red brigade’.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam jana, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela, alisema kuwa wana
wasiwasi na mafunzo yatakayotolewa na Chadema, yatakuwa na ‘sura ya kigaidi’
kwa vile yatafanyika kwa siri.
“Tunalaani
vikali mafunzo hayo, hayana tija yoyote kwa jamii yeyote,” alisema Shigela.
Kwa mujibu wa Shigela, UVCCM
haifanyi kazi za ulinzi kama `red brigade’ badala yake wanaangalia ni jinsi
gani vijana wanaboreshewa huduma mbalimbali za kijamii kupitia siasa.
WAISEMEA KATIBA MPYA
Shigela aliipongeza rasimu
ya Katiba Mpya kupitia Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, kwa kuwaandaa
wabunge wenye umri mdogo, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Rasimu ya Katiba Mpya
inaainisha kwamba wagombea nafasi za ubunge wanatakiwa kuwa na umri wa miaka 21
hadi 25,ila awe anakidhi kiwango na sifa za ubunge, hili ni jambo jema”,
alisema. NA MPEKUZI
0 comments:
Post a Comment