Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)wakiimarisha ulinzi kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kaloleni wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo uliofanyika jana.Picha na Filbert Rweyemamu.
ARUSHA.
CHADEMA kimethibitisha umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya kutetea kwa kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana.
Katika uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu
na ambao ulichukuliwa kama kipimo cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na
mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza katikia vituo vyote 136 vya kupigia
kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya
Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih
Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles
Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa
Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah
Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047 dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer
wa CCM. Katika Kata hiyo kulik
uwa na wagombea wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima (TLP;1).
uwa na wagombea wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima (TLP;1).
Katika Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema
aliibuka na ushindi baada ya kupata kura kupata kura 674. Msimamizi wa
Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema Kinabo alifuatiwa na Victor
Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF alipata kura 307.
Kata ya Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna
Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 1,470
dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330 na Abbas Mkindi wa
CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia Makini
aliyeambulia kura mbili.
Kata ya Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman
Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa
kura 2,761 na kumshinda Edna Saul wa CCM aliyepata kura 1,163. Kwa
matokeo hayo, Chadema sasa kimefikisha madiwani 12 wakati CCM kimebakiwa
na kumi na moja na TLP kina wawili.
Ushindi huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya
Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwani CCM kina wajumbe 14 tu
kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati Chadema sasa kimefikisha
15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni madiwani.
Aidha, Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti
kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa
kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alimwambia
mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo hivi
karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na Ofisi ya Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya
aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo kujitoa CCM na kujiunga na
Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika wakati mgumu
kukitetea kiti hicho. CHANZO MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment