.
NI DHAHIRI
kwamba Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), sasa ni
kitovu cha kusafirisha dawa za kulevya nje ya nchi.
Katika kipindi cha takribani wiki mbili tu, Watanzania wanne
wamekamatwa ughaibuni wakiwa na shehena ya dawa hizo ambazo
walisafirisha kutoa Tanzania kwenda nje kupitia uwanja huo bila ya
kukamatwa.
Mara ya kwanza walikuwa ni wasichana wawili, Agnes Jerald (25) na
Melisa Edward (24), ambao walikamatwa Afrika Kusini na kushtakiwa nchini
humo.
Walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wakiwa na
shehena ya kilo 150 ya dawa aina ya Crystal Methamphetamine zenye
thamani ya zaidi ya Sh.
bilioni 6.8.
Wasichana hao walikamatwa Julai 5,
mwaka huu baada ya kuwasili Johannesburg wakitokea Tanzania wakisafiri
kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na walikamatwa na
Maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.
Ijumaa wiki hii, Watanzania wengine wawili, walikamatwa Hong Kong
wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya
bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia
Dubai hadi Honh Kong.
Matukio haya yote yanatokea wakati wakuu wa Uwanja wa ndege wa Julius
Nyerere zinakopitishwa wakiwa hawana cha kusema juu ya uharamia huo
unaotokea kwenye kitovu cha mawasiliano cha nchi.
Jana, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Nchini,
Deusdedit Kato, alisema jalada la upelelezi kuhusu tukio la kukamatwa
kwa wasichana Afrika Kusini litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
leo ingawa hakuwa tayari kutaja watuhumiwa ni nani hasa wanaoshirikiana
na wafanyabiashara ya dawa hizo.
Kato alisema hawezi kutaja majina ya watu waliobainika kwa sababu
kilichofanyika ni uchunguzi tu na kwamba DDP ndiye mwenye mamlaka ya
kuamua juu ya uchunguzi huo.
“Siwezi kukuambia ni nini kimepatikana katika uchunguzi wala kutaja
majina ya watu, kwa kuwa mimi ninapeleka nilichokichunguza kwa sababu
naweza kukuambia lakini ikawa sio hivyo kwani huu ni uchunguzi tu,”
alisema.
Aliongeza: “Naweza kupeleka jalada langu la uchunguzi kwa DDP lakini
kutokana na utalaam wake akagundua kuna mapungufu, hapo tayari nitakuwa
nimepotosha umma.
Lakini pia akiona upelelezi unajitosheleza yeye ndiye
anaweza kuamua kupeleka Mahakamani.”
Kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Watanzania wengine na dawa za kulevya
Julai 26, mwaka huu huko huko mjini Hong Kong, Kato alisema bado
wanafanya jitahada za kupata kwa undani taarifa hizo.
“Na mimi nimesikia, lakini hatujapata taarifa zaidi ili kujua majina
yao na kama kweli ni Watanzania. Inakuwa ngumu kupata taarifa kwa sababu
aina ya mawasiliano wanayotumia hawa Polisi wa Kimataifa (Interpol )
ni tofauti na ya kwetu kwa hiyo tunategemea wao ndiyo watupe taarifa,”
alisema Kato.
Naye Waziri wa Uchunguzi, Dk. Harrison Mwanyembe, ambaye amejipatia
sifa za utendaji katika siku za hivi karibuni, kwa kuendesha timua timua
katika taasisi zinazosimamiwa na wizara yake kwa tuhuma za uzembe,
amekuwa kimya na pengine kukwepa kabisa kutia mguu katika sakata la dawa
za kulevya JNIA.
Wiki iliyopita NIPASHE lilimtafuta Dk. Mwakyembe mwenye dhamana ya
Viwanja vya Ndege nchini kujua ni hatua gani amechukua, lakini alijibu
kwamba hana taarifa za kina kuhusu sakata hilo.
Uharamia huo wa dawa za kulevya umempa pia kigugumizi Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, ambaye
amekwepa kuzungumzia sakata hilo na kusema liko kwa Kamanda wa Polisi,
Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey Nzowa.
Kamanda Nzowa alipoulizwa alisema upelelezi bado unaendaelea kubaini mambo mbalimbali yaliyoko nyuma ya tukio hilo.
Alipoulizwa ikiwa Polisi wamebaini mmiliki pamoja na maofisa
walioruhusu kupitishwa kwa dawa, Nzowa alisema uchunguzi unaangalia
mambo mengi na ndiyo huo utakuja na taarifa kamili.
Taarifa kutoka Hong Kong za Ijumaa wiki iliyopita zinaeleza kwamba,
maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA), walimkamata
kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 akitokea Tanzania na alikuwa na
dawa za kulevya aina ya heroin kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bilioni
1.5, kwenye mzigo wake wa mkononi.
Taarifa zilieleza kwamba baadaye jioni siku hiyo hiyo, maofisa hao
walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 ambaye alipelekwa
hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.
Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania
wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya
nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa
10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na uharamia huo.
Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za
Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, na kuharibu taswira ya nchi na
kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu
wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment