BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JK: RWANDA WANANITUKANA.

JAKAYA KIWETEPAUL KAGAME.

RAIS Jakaya Kikwete ameeleza kushangazwa na kushtushwa na kauli za vitisho na matusi zinazotolewa na viongozi wa Serikali ya Rwanda, tangu alipotoa ushauri wa kuitaka nchi hiyo kukaa meza moja na waasi.

Amesema, pamoja na kwamba viongozi wa Rwanda walimtafasiri vibaya pindi alipot

oa ushauri huo, yeye na Watanzania wataendelea kudumisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili japokuwa Rwanda wanaweza kuwa na lao jambo dhidi yake na Tanzania kwa ujumla.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akilihutubia taifa katika utaratibu wake wa kila mwezi wa kuzungumza na Watanzania.

“Katika kipindi cha miezi miwili sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda unapitia katika wakati mgumu, kwani kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu zetu wa Rwanda, kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania, tunapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote jirani, kwani sisi kama majirani, kila mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.

“Napenda kusisitiza kuwa, mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yoyote jirani au yoyote duniani, kwa sababu hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu.

“Ukweli ni kwamba, wakati wote tumekuwa tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu, kwa kuwa hiyo ni moja ya nguzo kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania na pia huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza.

“Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda, kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu, mambo yapo vile vile kwa kuwa mimi binafsi sijasema lolote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. 


Siyo kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha, sijafanya hivyo kwa sababu sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yoyote na naamini busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo, Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.

“Napenda kurudia kusema, kuwa mimi binafsi na Serikali yetu ya Tanzania, hatuna ugomvi wala nia yoyote mbaya na Rwanda, tunapenda tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda, labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi yetu ambalo sisi hatulijui, maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu, hatupendi kuyaamini moja kwa moja tunayoyasikia, lakini hatuyapuuzi,” alisema Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mtu yeyote anayepewa ushauri, halazimishwi kuukubali bali anaweza kuukataa kama ataona hauna faida kwake.

“Kama mjuavyo, uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi, kwani tumekuwa tukishirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na hata kimataifa.

“Uhusiano wetu unaelekea kupata mtikisiko, baada ya mimi kutoa ushauri kwa Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao na ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo, njia hiyo ni vema itumike na isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo na kwa Serikali ya Uganda.

“Katika mkutano ule, Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga mkono kauli yangu, Rais wa Rwanda hakusema chochote pale mkutanoni, lakini baada ya kurudi nyumbani, ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia,” alisema Rais Kikwete na kuongeza.

“Kwa kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya, kwani havifanani kabisa kwani mimi nilifanya vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu, kwa sababu tumekuwa tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali ambapo tunazungumza na kushauriana kwa uwazi juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea.

“Wakati wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote, hivyo kupeana ushauri ni wajibu wetu wote na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana, huzungumza, sasa iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu na la kufanya mtu kushutumiwa na kutukanwa, siyo sawa hata kidogo.


Ushauri si shuruti, ushauri si amri, una hiyari ya kuukubali au kuukataa, muungwana hujibu, siuafiki ushauri wako na hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo na ya uongo,” alisema Rais Kikwete.

Majambazi na wahamiaji

Kama alivyosema wakati akiwa katika ziara yake wiki iliyopita mkoani Kagera, Rais Kikwete ameendelea kusisitiza kauli yake, kwamba siku 14 alizotoa kwa majambazi kusalimisha silaha ziko pale pale.

Alisema kwamba, wahamiaji haramu nao pia wanatakiwa kufuata taratibu za kuishi nchini, kwani pindi operesheni itakapoanza, hawatakuwa na mahali pa kujificha.

“Nilisema nilipokuwa mkoani Kagera na narudia tena leo, kuwa baada ya siku 14 kupita, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni maalumu ya kushughulikia matatizo hayo. Nilisema kuwa, operesheni hiyo itafanyika katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala kujificha, nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo, waamue kuchukua hatua muafaka sasa na wasisubiri operesheni iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita, safari hii itakuwa endelevu.

“Hatuwezi kukubali hali hii niliyoikuta mkoani Kagera iendelee, kwani tukiiacha italeta madhara kwa siku za usoni, haiwezekani raia katika nchi yake, akose uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka asindikizwe na polisi na baya zaidi hata polisi nao wanashambuliwa na kuuawa, uhalifu huu lazima ukomeshwe, uishe na usijirudie tena,” alisema.

Pamoja na hayo, Rais Kikwete alizungumzia pia mafanikio ya ziara ya viongozi wa mataifa ya nje wakiwamo Rais Barack Obama wa Marekani, Rais mstaafu wa nchi hiyo, George Bush na Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra. MTANZANIA.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: