Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema
anasikitishwa na matukio ya hujuma yaliyojitokeza Zanzibar, ikiwemo watu
kumwagiwa tindikali, na kutaka uchungunzi wa kina ufanywe kuwabaini
wahusika, na baadaye ripoti ya uchunguzi huo iwekwe wazi kwa wananchi.
Amesema hatua ya kuwekwa bayana ripoti za uchunguzi wa matukio hayo
ya hujuma, ni jambo muafaka katika kufuta dhana zinazojengeka miongoni
mwa wananchi na jamii ya kimataifa kuhusiana na watu wanaohusika kufanya
hujuma hizo.
Maalim Seif ameyasema hayo katika mahojiano maalum juu ya maadhimisho
ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.
Amesema ili amani na mshikamano wa wazanzibari udumu, matukio kama
hayo ya hujuma ambayo yamekuwa yakiwalenga zaidi baadhi ya viongozi wa
dini na hata wageni, hayanabudi kuangaliwa kwa upana wake, na kuwataka
wananchi wajiepushe na kufikia maamuzi ya haraka kuwahusisha wengine
bila ya uchunguzi wa kina kufanywa.
Alisema wananchi walipata matumaini ya kukomeshwa kwa vitendo hivyo
mara baada ya hujuma zilizofanywa dhidi ya viongozi wa dini pamoja na
mripuko uliotokea katika kanisa la Arusha ambapo walihidiwa uchunguzi wa
kina utafanyika na kuhusisha wapelelezi wa kimataifa, lakini hadi sasa
hakuna ripoti yoyote iliyowekwa bayana.
Maalim Seif ameeleza kwamba badala yake matukio ya hujuma yameendelea
na wananchi kuendelea kujenga dhana ya kuwahusisha watu au makundi
maalum bila ya kuwa na uthibisho, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na
utulivu wan chi.
“Ingekuwa wakati ule tungesema ni siasa, lakini sasa tuna serikali ya
pamoja Zanzibar, kwa nini mambo haya yanatokea sasa, huu ni mtihani
mkubwa kwetu”, alisema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF,
amesema pia amekuwa mgumu kuamini kuwa dini inahusika katika matukio ya
hujuma yaliyotokea Zanzibar.
Amesema Zanzibar ina historia ya kipekee ya uvumilivu wa kidini
duniani, kutokana na wananchi wa visiwa hivi kuishi pamoja kwa miaka
mingi bila ya kubaguana kwa misingi ya dini zao.
“Sisi Zanzibar kiwango chetu cha uvumilivu ni kikubwa na nambari moja
duniani, hata ukiangalia Ukristo Afrika Mashariki mlango wake ni
Zanzibar”, alifafanua Maalim Seif.
Akitoa mfano wa uvumilivu huo, Maalim Seif amesema hata unafika mwezi
wa Ramadhan huwezi kumuona mtu wa imani yoyote akila hadharani wakati
wa mchana, na kwamba wananchi wote wanashirikiana katika shughuli za
kijamii bila ya kujali imani zao.
Ameeleza kuwa baada ya matukio ya kujeruhiwa Padri Ambrose Mkenda,
kuuawa kwa Padri Evarist Mushina mripuko wa bomu katika kanisa mjini
Arusha, Serikali iliahidi kuleta makachero wa F.B.I, na hata baada ya
wasichana wa Kiingereza kumwagiwa tindikali inaelezwa wachunguzi kutoka
Scktland Yard wapo, lakini hakuna taarifa hadi sasa iliyotolewa
kuhusiana na uchunguzi huo.
“Tusiajiegemeze kwenye dhana, uchunguzi ndio kitu muhimu. Hawa
wanaoathirika na hujuma mbali ya kuwa viongozi wa dini nao ni binadamu,
tujiulize jee hawakujenga uhasama au kutokufahamiana na wengine huko
katika jamii”, alihoji Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa ni makosa kuendesha mambo kwa dhana, kwa vile
matokeo yake ni kuwaadhibu watu kwa kuwaweka ndani bila ya kuwa na
hatia.
Amewataka wananchi kuwa makini na waendelee kuwa wamoja, ili amani,
mashirikiano na umoja uliodumu uendelee wakati huu ambapo Zanzibar
inaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.
Wakati huo huo Maalim Seif amekutana
na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen QiMan na kuelezea
umakini na uadilifu wa makampuni ya Kichina katika kutekeleza majukumu
yao.
Amesema mara nyingi kazi za kiufundi wanazopewa wataalamu wa Kichina
zimekuwa zikitekelezwa kwa umakini na kwa wakati uliopangwa, hali
inayotoa matumaini ya kuendelea kutoa tenda kwa makampuni hayo.
Aidha amesifu ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na
Zanzibar ambao umekua ukichangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa
jamii.
Amemtaka balozi huyo kuwa kiungo katika kuwashajiisha watalii na
wawekezaji wa China kuja Zanzibar, ili kuendelea kuunga mkono juhudi za
serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema China ni mshirika wa kweli wa maendeleo ambayo imekuwa
ikishirikiana na Zanzibar katika kutatua kero zinazoikabili ikiwa ni
pamoja na kusaidia wataalamu hasa katika sekta ya afya.
Naye balozi QiMan amesema katika kipindi chake cha utumishi hapa
nchini, ameshuhudia mafanikio makubwa yakipatikana yakiwemo kuimarika
kwa majengo, huduma za elimu pamoja na miundombinu ya mawasiliano.
Ameahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Zanzibar na kutoa
michango zaidi katika kusaidia uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.
Balozi Chen QiMan amemaliza muda wa utumishi hapa nchini, baada ya
kuitumikia nafasi hiyo ya ubalozi mdogo kwa kipindi cha miaka miwili na
nusu.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment