ITALIA KUANZA UPYA KAZI YA KUSAKA MIILI YA WATU WALIOFARIKI BAHARI YA MEDITERANIA KATIKA KISIWA CHA LAMPEDUSA KUFUATIA MASHUA ILIYOKUWA INAWASAFIRISHA WAHAMIAJI WAAFRIKA KUWAKA MOTO.
Vyombo vya idara ya huduma za dharura ya Italia.
IDARA ya huduma za dharura nchini Italia inatarajia kurejea kusaka miili ya watu waliofariki baharini jana licha ya hali mbaya ya hewa na mawimbi makubwa baada ya boti kuzama katika bahari ya Mediterran
ean.
Katika boti hiyo ambayo ilikuwa na zaidi ya abiria 450, idara ya huduma za dharura imethibitisha kuwa wahamiaji 111 kutoka Afrika wamefariki na kiasi wengine 200 bado hawajulikani waliko.
Wakati utafutaji wa miili nje ya kisiwa cha Lampedusa umesitishwa jana Ijumaa kutokana na hali mbaya ya hewa , kiongozi wa kanisa Katoliki ambaye alizungumza akionesha hisia kali amesema, kuwa "ilikuwa siku ya kububujikwa na machozi" katika "dunia hii ya kikatili" ambayo inawapuuza wakimbizi.
Serikali imeuomba umoja wa Ulaya usaidie kuzuwia uingiaji wa wahamiaji , wakati nchi hiyo inaomboleza vifo hivyo.
Papa Francis wa kanisa Katoliki
Wafanya maombi.
Wakaazi wa kisiwa hicho kidogo cha jamii ya wavuvi wamefanya misa pamoja na maandamano ya kimya kimya ya kuwasha mienge , wakati bendera zikipepea nusu mlingoti nchini Italia jana Ijumaa na shule zilifanya kumbukumbu ya wahanga kwa kukaa kimya kwa dakika moja.
"Hii ni shughuli muhimu kwa wahanga na kwetu sisi", amesema Michele Rossi , mkaazi wa eneo hilo ambaye ni mmiliki wa duka. "Tumezowea kufanya kila tunaloweza kuokoa maisha lakini hatujaona kitu kama hiki."
Idara ya huduma za dharura katika kisiwa hicho , ambacho kiko katika eneo la mbali upande wa kusini kabisa mwa Italia , zimesema kuwa zimetoa kutoka majini miili 111 hadi sasa na wameokoa watu 155 ambao wako hai kutoka katika boti hiyo ambayo inakisiwa kuwa ilikuwa na watu kati ya 450 na 500.
Waokoaji wamesema mawimbi makubwa na upepo katika kisiwa hicho huenda yameisukuma miili mingine mbali zaidi ndani ya bahari lakini hawakuweza tena kuondoka bandarini kwasababu ya upepo mkali pamoja na mawimbi yenye urefu wa mita mbili.
Maiti za wahamiaji waliokufa maji
"Kuna hali ya kuogofya. Maiti kadha , huenda kwa mamia," Rocco Canell, ambaye anaendesha shule katika kisiwa hicho ya udereva na alikwenda katika eneo la bahari kabla ya msako kusitishwa , ameliambia shirika la habari la Italia ANSA.
"Miili imepandana, imelundikwa, mmoja juu ya mwingine. Wale wenye bahati ni wale waliofariki kwanza," amesema baada ya kutoka katika eneo hilo la kutisha lililopinduka boti hiyo, ambapo boti hiyo imezama kabisa katika kina cha karibu mita 40.
Wakiwa na hofu waliruka majini
Wahamiaji , karibu wote wakiwa ni Waeritrea , waliondoka kutoka bandari ya Libya ya misrata na walisimama kuchukua watu zaidi mjini Zuwara, pia nchini Libya.
Wamewaambia waokoaji kuwa walichoma blanketi katika boti hiyo nje kidogo ya Lampedusa kuashiria kwa walinzi wa pwani baada ya boti yao kuanza kuingiza maji.
Moto huo haraka ukasambaa katika boti hiyo yenye urefu wa mita 20, ambayo ilizama majira ya alfajiri siku ya Alhamis(03.10.2013) ikiwa ni mita chache tu kutoka Lampedusa, wakati abiria waliokuwa na hofu kubwa walianza kuruka majini wakiwa wamemwagikiwa na mafuta.
Miili ya wahamiaji katika kisiwa cha Lampedusa
Nahodha wa boti hiyo raia wa Tunisia , ambaye aliwahi kukamatwa na polisi nchini Italia mwezi Aprili kwa kusafirisha watu kinyume na sheria na kurejeshwa nchini mwake Tunisia , anashikiliwa na polisi.
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Angelino Alfano ametoa wito wa kuongezwa msaada wa mataifa ya Ulaya katika kufanya doria katika mipaka ya majini nchini Italia pamoja na hatua zaidi katika nchi barani Afrika kuzuwia wimbi la wakimbizi wanaovuka mipaka na kuingia nchini humo. DW
0 comments:
Post a Comment