VYOMBO vya habari nchini vimeandika
historia ya aina yake ya kupitisha azimio la kuwafungia kwa muda usiojulikana,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamad
uni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni takriban
wiki mbili tangu viongozi hao kutumia mamlaka wanayopewa na sheria ya magazeti
ya mwaka 1976, kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kutochapishwa kwa
madai ya kuchapisha habari za uchochezi.
Wakati gazeti la Mwananchi
likifungiwa kwa siku 14, Mtanzania limefungiwa kwa siku 90.
Vilevile hatua hiyo imekuja zaidi ya
mwaka mmoja tangu viongozi hao walifungie gazeti la wiki la MwanaHalisi pia kwa
madai ya kuchapisha habari za uchochezi.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la
Wahariri (TEF) jana, ilisema kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa pamoja na Jukwaa
hilo, Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT) na Taasisi ya
Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA Tan).
Wamo pia Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Dar City Press
Club (DCPC) na Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC).
Hatua hiyo inamaanisha kuwa kuanzia
jana, habari zozote zitakazotolewa au kuwahusisha Waziri Mukangara na
Mkurugenzi wa Maelezo, Mwambene, hazitaandikwa ama kutangazwa na chombo
chochote cha habari kwa muda usiojulikana.
Hatua ya kuwafungia viongozi hao
inafuatia kikao cha pamoja cha wadau hao kilichofanyika jana jijini Dar es
Salaam kutokana na hatua ya serikali kuyafungia magazeti hayo.
Mukangara na Mwambene wamefungiwa
kwa tuhuma ya kudharau na kufanya uamuzi wa kuyafungia magazeti hayo bila
kusikiliza hoja za upande wa pili.
Wanadaiwa pia kutoa maneno
yaliyolenga kupotosha umma kwa makusudi juu ya hatua ya kuyafungia magazeti
hayo.
Wadau hao walieleza kusikitishwa na
hatua ya serikali ya kupuuza kilio chao cha kuomba kusitishwa kwa sheria
kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976.
Vilevile wanalalamikia kudhoofishwa
kwa mchakato wa kuibadilisha sheria hiyo iliyotajwa na Tume ya Jaji Francis
Nyalali mwaka 1992, kuwa ipo kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
“Hivyo tunasitisha kuandika,
kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na
Waziri Mukangara na Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo.
“Wadau wa habari tutaendelea kupinga
sheria ya magazeti ya mwaka 1976 kwa kupigia kelele kufutwa kwa sheria hiyo na
kuongeza nguvu ya kisheria mahakamani kwenye kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya
Hali Halisi Publishers Ltd, mwaka 2009 inayopinga sheria hiyo,” ilisema taarifa
ya TEF.
0 comments:
Post a Comment