Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya.
LICHA ya kuwa katika kampeni kali na ngumu ya usiku na mchana ya kukabiliana na wahamiaji haramu nchini, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya amekuwa pia akipigania kuwapo kwa mpaka unaoeleweka baina ya Tanzania na nchi jirani ya Burundi.
Kwa sasa, mpaka pekee unaoeleweka baina ya nchi hizi upo Manyovu, katika wilaya mpya ya Buhigwe na kwa upande wa Burundi, ni eneo la Mugina, Mabamba katika Jimbo la Makamba.
Akizungumza hivi karibuni ofisini kwake eneo la Maweni, mjini Kigoma, Luteni Kanali Machibya alisema tangu alipokabidhiwa jukumu la kuuongoza mkoa huo Septemba mwaka 2011, amekuwa na kiu ya kutaka kuona kunakuwa na mipaka ya nchi inayotambulika ili kurahisisha kazi za kiutawala.
Machibya ambaye alihamishiwa Kigoma akitokea Morogoro, alisema anaamini kutokuwepo kwa mipaka ni tatizo na kwamba hata `kufurika’ kwa wahamiaji haramu nchini huenda linachangiwa na hali hiyo.
Aliyataja maeneo yanayohitaji kubainishwa mipaka ya nchi ni kuanzia Kagunga katika wilaya ya Buhigwe na eneo lote linalozunguka Mto Malagarasi ambali alisisitiza ni kubwa. Maeneo mengine ni Kigadye katika wilaya ya Kasulu na pia wilaya za Kibondo na Kakonko.
“Ukiondoa Uvinza na Kigoma Mjini, wilaya nyingine kuna matatizo ya aina hiyo…tunafanya kazi kwa karibu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi chini ya mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka.
“Sisi wa hapa mkoani tunamshukuru amelipokea vizuri jambo hilo na ameshatuma maofisa wake kuja kuangalia hali halisi…nina uhakika tutafikia pazuri na mwisho wa siku tutakuwa tunajua mipaka yetu halisi.
Hatutaki yaje kutokea kama
yale ya Malawi,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa aliyesisitiza anakerwa mno na
wahamiaji haramu aliowataja waziwazi kuwa ni chanzo cha matatizo mengi
yanayotishia amani na usalama wa nchi.
Kauli ya Luteni Kanali mstaafu Machibya imekuja huku Tanzania ikiwa katika mgogoro wa mpaka na Malawi katika eneo la Ziwa Nyasa.
Kauli ya Luteni Kanali mstaafu Machibya imekuja huku Tanzania ikiwa katika mgogoro wa mpaka na Malawi katika eneo la Ziwa Nyasa.
Mgogoro wa kuwania umiliki wa Ziwa Nyasa ambalo Malawi wanaliita Ziwa Malawi, uliibuka upya mwaka jana baada ya Malawi kupeleka kampuni za utafiti wa mafuta na gesi katika ziwa hilo hadi eneo la Tanzania, jambo ambalo liliifanya nchi hiyo kuingilia kati na kutaka shughuli zote zisimame hadi pale ufumbuzi utakapopatikana.
Kwa muda mrefu, tangu enzi za utawala wa Rais wa Kwanza wa Malawi, Hastings Kamuzu Banda, Malawi imekuwa ikidai kuwa ziwa hilo lote ni mali yake wakati Tanzania ikisisitiza kuwa nusu ya Ziwa iko Tanzania.
Na katika kuhakikisha suluhu ya kweli inapatikana, Tanzania imekuwa ikifanya juhudi za kila aina ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo, lakini Malawi haionekani kuridhishwa na njia hiyo ya utatuzi wa mgogoro. Katika kuthibitisha hilo, ilijitoa kwenye mazungumzo ya usuluhishi na kuamua kupeleka mgogoro kwenye Mahakama ya Kimataifa (ICJ).
Rais wa Malawi, Joyce Banda alikaririwa na vyombo vya nchini mwake akisema nchi yake haitopoteza muda na usuluhishi uliokuwa ukifanywa na marais na viongozi wastaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) chini ya Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano.
Chimbuko la mzozo wa mpaka uliopo sasa, baina ya nchi hizi mbili jirani, rafiki na ambazo watu wake ni ndugu, ni makubaliano baina ya Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka yaliyofanywa Julai Mosi, 1890.
Makubaliano hayo yajulikanayo kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland Treaty) yalitiwa saini Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza na Wajerumani. Wakoloni hao walikubaliana kuhusu mipaka baina ya makoloni yao na baina yao na wakoloni wengine waliopakana nao.
Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na Wajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa Tanzania. Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi ya Malawi. Kwa upande wa Mto Songwe mpaka ulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa Tanzania.
Hata hivyo, katika kipengele cha Sita cha Mkataba huo, wakoloni hao walikubaliana kufanya marekebisho ya mpaka mahali po pote kama itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana na mazingira na hali halisi ya mahali hapo. Kwa mujibu wa kutekeleza matakwa ya kipengele hicho mwaka 1898 Tume ya Mipaka iliundwa. Ilianzia kazi katika Mto Songwe kuhakiki mpaka baina ya Tanzania na Malawi.
Tume ilikubaliana kuhamisha mpaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati ya mto. Baada ya uhakiki katika eneo hilo kukamilika, mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo. Tume iliendelea na kazi yake katika Ziwa Tanganyika na kuhamisha mpaka kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkataba mpya kusainiwa mwaka 1910.
Kwa bahati mbaya Tume hiyo haikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokea kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 - 1918. Itakumbukwa kwamba, Waingereza na Wajerumani waligeuka kuwa maadui na kupigana hata hapa nchini.
Baada ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Baraza la Umoja wa Mataifa (The League of Nations) liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika. Hivyo, Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.
Wakati Tume ya Uingereza na Ujerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Ureno iliendelea na kazi. Matokeo yake, mwaka 1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891 ulioweka mpaka wa Ziwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa, yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji, na kuuhamishia katikati ya ziwa, lakini haikufanya hivyo kwa upande wa Tanganyika na Malawi kwa kuwa zilizokuwa chini ya mtawala mmoja, yaani Mwingereza.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment