BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KIKONGWE ALIVYOUAWAWA KISHA KUCHUNWA NGOZI, ATEKWA USIKU WA MANANE WAKATI AKIENDA KUJISAIDIA HAJA NDOGO KATIKA KITONGOJI CHA GONGO KIJIJI CHA MGATA MOROGORO.

Mzee Steven Francis (50) kulia, mke wake Yustina Kasian (40) aliyembeba mtoto James James Peter na Eliza Steven (19) wakizuru kaburi la marehemu Hellan Petri Mahunzila (75) aliyeuawawa kisha mwili wake kuchunwa ngozi hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Morogoro. PHOTO/MTANDA BLOG.

Diwani wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu kulia akifafanua jambo mbele ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Mgata na kitongji cha Gongo katika eneo la Mondo ambalo ndipo marehemu, Hellan Petri Mahunzila (75) ulitupwa mwili wake baada ya kuuawawa kisha kuchunwa ngozi katika mauaji ya kutatanisha hivi karibuni halmashauri ya wilaya ya Morogoro.
Mzee Steven Francis (50) akiwa na familia yake katika kitongoji cha Gongo kijiji cha Mgata kata ya Bwakilajuu.

Eneo hili ndilo linalodaiwa mwili ulitupwa.

Mtanda Blog.
TUKIO la kifo cha kikongwe, Hellan Petri Mahunzila (75) ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 12 kisha siku ya 13 mwili wake kuonekana kando ya shamba lake huku maiti yake ikiwa imechunwa ngozi mwili mzima, imezua hofu kubwa na kukubikwa na usiri wa mauaji hayo huku wakazi wa kitongoji cha Gongo kijiji cha Mgata kata ya Bwakilajuu mkoani Morogoro wakiishi kama mnyama digidigi ambaye amekuwa akiwindwa na binadamu kwa ajili ya kitoweo.

Wakazi hao wamekubwa na hofu hiyo wakihofia maisha yao na kulazimika haja ndogo na kubwa kujisaidia katika makopo hasa nyakati za usiku ndani ya nyumba zao na asubuhi kumwaga kinyeshi na mkojo na kubadilisha kabisa mfumo wa kutembea, kulala na kulazimu kila kaya kuingia ndani ya nyumba kuanzia majira ya saa 12 hadi saa 12:30 jioni kuepuka mtego wa kutekwa.

Ni majira ya saa 7 usiku, siku ya jumatano kuamkia alhamisi ya oktoba 2 mwaka huu, Eliza Steven (19) anaamka na kumnyonyesha kichanga chake, James Peter (miezi mitatu) baada ya kilio cha kichanga hicho kilichokuwa kinahitaji huduma ya kunyonya kutoka kwa mama yake ndicho chanzo cha kubainika kwa kupotea kwa marehemu Hellan Petri Mahunzila.

Baada ya James kunyonya na kushiba kichanga hicho kilinyamaza kulia na kumpa fursa ya mama yake kutoka ndani ili aende nje kwa ajili ya kujisaidia haja ndogo, anafungua mlango wa chumba chake na kutoka nje kujisaidia huku akipiga jicho na kuangalia mlango wa chumba anacholala bibi yake anaona mlango upo wazi.

Jambo hilo la kukuta mlango wa bibi yake kukuta ukiwa upo wazi hakulitilia mashaka kwani alikuwa na imani angeweza kukutana naye nje ama chooni lakini haikuwa hivyo bali akawa na imani tena pakuwa hakuweza hakuonana naye nje wala chooni aliingia ndani na kwenda moja kwa moja hadi katika chumba anacholala bibi yake na kuingia ndani.

Alipoingia katika chumbani chake aliangalia kitandani ili kuweza kujijibu maswali yake yasiyojaa kichwani likiwemo la kwanini bibi yake ameshindwa kufunga mlango kama alitoka nje ? anaanza kusema alisema Eliza.

Eliza aliendelea kueleza kuwa baada ya kuchunguza katika chumba kile kinachotumiwa na bibi yake, Hellen ambaye alikuwa na kawaida ya kufunga pindi aiingiapo kulala hakumwona na kuchukua jukumu la kumwamsha mama yake mzazi, Yustina Kasian (40) ili aweze kusaidiana naye kumtafuta.

“Niligonga mlango wa chumba alicholala mama na baba na nilimwita mama na alipotoka ukumbini usiku ule nilimweleza kuwa mlango wa chumba cha bibi upo wazi lakini hata na ule mlango mkubwa nao pia nimeukuta umeegeshwa tu na nimeenda chooni pengine yupo kule lakini hayupo”. Alisema Eliza ambaye ni mjuu wa bibi huyo.

Yustina Kasian ambaye ni mtoto wa pili kwa kuzaliwa kwa bibi, Hellen Petri Mahunzila alisema kuwa baada ya kuelezwa maneno yale na mtoto wake, Eliza Steven ambaye ni bibi yake alienda katika kile chumba anacholala mama yake na kuangali huku na huku lakini naye hakuweza kuona dalili ya uwepo wa mtu katika kitanda, uvungu na eneo la chumba kwa ujumla na kwenda moja kwa moja chooni ili akamwangalie huko pengine alikuwa huko.

“Nilienda chooni na kuangalia ndani ya chooni lakini sikumwona na badala yake nilirudi ndani na kumwamsha mume wangu, Steven Francis (50) ili naye aweze kutusaidia kumfuata kwani tayari hofu ilianza kutanda moyoni mwetu na kujiuliza maswali ambayo hatuweza kupata majibu kwa usiku ule”. Alisema Yustina.

Mimi baada ya kuelezwa jambo hilo na mke wangu nilitoka nje na tochi hadi chooni na kumulika ndani na kuzunguka kile choo sikuweza kumwona na kuhamishia kufanya zoezi hilo kwa kuzunguka nyumba, banda la kupikia chakula na eneo zima la migomba lakini mama mkwe wangu hakuweza kuonekana akiwa hai ama amekufa. Alisema Steven Francis ambaye ndiye mwenye kaya hiyo yenye familia ya watu sita.

Francis alisema kuwa zoezi hilo la kumsaka lilifanya kwa umbali wa mita 100 kutoka eneo la nyumba kwa usiku huo huku mvua kubwa ikinyesha na giza nene limetanda akishirikiana na familia yake lakini hakukuwa na mafanikio na kuchukua jukumu la kuomba msaada wa jirani ambapo alienda kwa Selis Silili na Calist Stephano ili wasaidie mchango wa kimawazo na kusamkasa mama mkwe wake.

Jirani zake hao walitoa wazo la kwenda kutoa taarifa la tukio hilo kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Gongo kijiji cha Mgata kata ya Bwakilajuu, Festo Mfaume usiku ule wa majira ya saa 7:45 ambapo mwenyekiti huyo aliwaeleza kuwa kutokana na giza nene na mvua zoezi hilo litafaa kufanywa asubuhi yake siku ya alhamisi. Alisema Francis.

Mwenyekiti huyo wa kitongoji cha Gongo, Festo Mfaume alisema kuwa ilikuwa siku wa jumatano ya oktoba 2 majira ya saa 7:45 kuamkia alhamisi oktoba 3 mwaka huu aliamshwa na Steven Francis, Selis Silili na Calist Stephano na kuelezwa juu ya tukio la kupotea kwa bibi Hellen Petri Mahunzila kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Ni kweli usiku wa oktoba 2 siku ya jumatano kuamkia alhamisi ya oktba 3 majira ya saa 7:45 niligongewa mlango na nilipotoka nje niliwaona mama mkwe wa bibi Hellena (Steven Francis), Selis Silili na Calist Stephano na kunieleza juu ya kupotea kwa bibi Hellen Petri Mahunzila (sasa ni marehemu) nami niliwajibu kuwa pakuwa nanyi mmefanya juhudi za kumtafuta bila mafanikio tuaghalishe zoezi hilo ili asubuhi mapema tuanze kazi ya kuongeza nguvu ya kumsaka”. Alisema Mfaume.

Mfaume alisema kuwa siku hiyo ya alhamisi oktoba 3 majira ya saa 11 alfajiri alienda sehemu maalum ya mlima ambayo hutumika kutoa taarifa kwa kupaza sauti yake na wakazi wa kitongozi hicho cha Gongo walikusanyika kwa haraka katika nyumba ya, Steven Francis na muda mfupi wananchi hao walijigawanya katika makundi na kuanza kazi ya kumsaka huku akifanya jitihada za  kuwajulisha viongozi wa kijiji cha Mgata akiwemo Mwenyekiti na Mtendaji wake ambao nao waliungana na wananchi hao katika zoezi hilo asabuhi ile.

“Kitongoji changu kina zaidi  ya wananchi 325 na tukio hili limekuwa la kwanza kutokea na nilichofanya ni kuwatawanya watu katika makundi kuanza kumtafuta bibi yetu Hellen sehemu za misitu, vichanga, shambani kwake, mapango na kutoa taarifa vitongoji vya jirani ili nao watusaidie kumtafuta, lakini tulifanya kazi hiyo kwa siku sita bila mafanikio na kukata tamaa”. Alisema Mfaume.

Mfaume alisema vitongoji vilivyoshiriki kumtafuta katika maeneo yao ni pamoja na Dinila, Mituna na shuleni vilivyopo ndani ya kijiji cha Mgata, kazi ya kumfuta kuanzia siku ya alhamisi oktoba 3 hadi 8 mwaka na ile usiku ule aliotoweka nyumbani kwake lakini mwenyezi mungu ndiye aliyejua kiume wake amepotelea.

Katika ardhi ya kitongoji hicho hakuna sehemu ambayo wananchi wameshindwa kufika lakini cha ajabu baada ya wao kukata tamaa kwa kumtafuta kwa siku sita, mwili wake ulionwa na mjukuu wake, Eliza Steven siku ya tarehe 15 mwaka huu ikiwa ni siku saba mbele yake siku ya ijumaa saa 7 mchana kando ya shamba lake ukiwa umechunwa ngozi na kutelekezwa baada ya kutupwa na kuvingika umbali wa mita zaidi ya 50 tangu utupwe katika mtelemko wa mlima. Alisema Mwenyekiti huyo wa kitongoji cha Gongo.

Siku ya oktoba 15 majira ya saa 7 mchana mwaka huu, Eliza Steven aliondoka nyumbani na chombo kwenda shambani kuchuma mbaazi kwa ajili ya mboga katika shamba la bibi yake, mita chache kabla ya njia walioizowea kuingilia shambani anaona nyasi zimelala na mburuzo kwa kitu jambo hilo lilimstua kwa eneo hilo lilikuwa na kichanga vyenye mchanganyiko wa miba.

“kabla ya njia ya kuingilia shambani hatua chache tu niliona nyasi zimelala na kama kuna kitu kilikuwa kimeburuzwa, nilistuka kidogo kwa sababu eneo hilo la mburuzo kuna nyasi lakini na mibamiba hivi nami nikaona ngoja nipite katika njia hiyo ya mburuzo huo nione mwisho wake”. Alisema Eliza.

Katika maelezo yake kwa mwandishi katika kitongoji hicho, Eliza alisema kuwa alipita njia hiyo ili kuweza kujua mwisho wa mburuzo huo ambao alitembea zaidi ya umbali wa hatua 18 za miguu akaanza kuona khanga na hatua mbili mbele yake akaona tena kitenge vipo chini na aliponyanyua macho mbele yake aliona mwili wa mtu.

“Nilitambua zile nguo kuwa ni za bibi yangu Hellen aliyepotea siku 13 zilizopita na niliposogelea zaidi ule mwili nilitambua kwa kuona ngua nyingine ambazo alivalishwa likiwemo gauni, bangili, heleni na shanga shingoni lakini mwili wake nilishangaa kuuona umekuwa mweupe hauna ngozi”. Alisema Eliza.

Eliza alisema kuwa baada ya kuona vile alipatapwa na mshtuko mkubwa huku moyo ukimdunda kwa hofu kwa kuona tukio hilo ambalo kwake ni la ajabu na kuamua kurudi kinyumenyume huku akimwita mama yake ambaye naye alienda shambani huko akimpelekea mtoto wake ambaye alikuwa analia ili aweze kumnyonyesha kwani sio mbali na shamba.

“Bibi amekufa, kifo cha kikatili sana, ni tukio la ajabu na kusikitisha sitaweza kusahau katika maisha yangu ya hapa duniani kwani kila aliyeona ile maiti alishikwa na butwaa na kuangua kilio, nimewahi kuona maiti wakati wa kuaga katika misiba ya majirani zetu na nimeona tofauti kubwa, bibi ameuawawa kisha amechunwa ngozi mwili mzima”. Alisema Eliza kwa huzuni.

Alienda kwa mama yake aliyekuwa shambani ameanza kuchuma mbaazi huku akimbembeleza James aliyekuwa analia na kumchukua mtoto wake na kumnyonyesha kisha kumweleza kila kitu alichoona na baadaye mama yake alifuata ule mburuzo hadi kwenye mwili wa marehemu yake naye alipojiridhisha kuwa ndiye aliyekuwa akisakwa kwa udi na mavumba aliangua kilio huku akielekea njiani. Anasema Yustin Casian.

Kilio cha Yustin kilikusanya wakazi wa eneo hilo na kuanza kumiminika umati wa watu kutoka katika kitongoji kile katika eneo la tukio na taarifa kusambaa kila kona ya kijiji huku wengine wakijulishana jambo hilo kwa njia ya simu za viganjani.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Gongo, Festo Mfaume anaeleza kuwa baada ya kuonekana kwa mwili huo alifuatwa nyumbani kwake na kijana aliyefahamika kwa jina la, Anthony Kalist na kumweleza kuwa bibi aliyepotea ameonakana kando ya shamba lake lakini tayari amekufa.

Nilienda eneo la tukio na nilipouna tu ule mwili nilibaini kuwa amechunwa ngozi tena kwa utalaam wa hali ya juu kwani hakuna sehemu ya mwili wake ambayo ngozi ilibakia si katika nywele wala katika vidole vya kucha hakukuwa ngozi iliyobakia katika mwili wake. Alisema Mfaume.

Nilipiga simu huku na kule kujulisha viongozi wenzangu kuanzia ngazi ya kijiji, kata na wengine waliendelea hivyo hivyo lakini baada ya kumpigia Diwani wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu majira ya saa 8 siku ile ya oktoba 15 yeye alinieleza kuwa watu wote wa kitongoji na kijiji cha Mgata wasiondoke eneo la tukio hadi kesho yake ya oktoba 16 mwaka huu.

“Baada ya mimi kujulishwa juu ya tukio lile na kuona mwili namna ulivyochunwa ngozi mwili mzima nilienda ofisi ya Mtendaji na Mwenyekiti wa kijiji cha Mgata kutoa taarifa pia nilimjulisha Diwani kwa njia ya simu naye akatoa agizo la kuulinda mwili ule hadi siku ya pili wakati yeye akifanya utaratibu wa kuwaleta askari polisi na daktari ili wachunguze tukio hilo”. Alisema Mfaume.

Mfaume alisema kuwa tukio hilo limekubikwa na utata mpaka wakati huu kutokana na mazingira yake ya kupotea kisha kifo chake kimekuwa na usiri mkubwa, na hata baada ya mwili wake kuonekana kando ya shamba lake bado kuna jambo limejificha kwa raia wa kawaida inamuumiza kichwa zaidi ya wahusika kufahamu nini wamekifanya na malengo yao.

“Mimi baada ya kumjulisha Kidevu (Diwani kata ya Bwakilajuu) tukio la kuonekana kwa marehemu huku mwili mzima ukiwa umechunwa ngozi yeye alitoa amri kwangu kwa kunitaka nitoe taarifa kwa wakazi wote kuulinda ule mwili kuanzani muda ule wa saa 7 mchana mpaka asubuhi siku ya pili yake”. Alisema Mfaume.

Msafara wa Daktari kituo cha afya Duthumi na askari wa kituo kidogo cha Kisaki-Gomero na Mtendaji wa kata ya Bwakilajuu ukiongozwa na Diwani wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu uliwasiri eneo la tukio majira ya saa 8:30 mchana siku ya jumatano oktoba 16 mwaka huu kwa ajili ya uchunguzi mwili na kuchukua maelezo kwa upande wa familia ya karibu ya marehemu.

Msichana Yusta Ostach (15) mkazi wa kitongoji hicho cha Gongo anasema kuwa yeye tukio hilo wakati linatokea hakuwepo katika kitongoji hicho bali alikuwa safarini na aliporejea siku tangu tukio kutokea alielezwa juu ya tukio hilo likiwemo la watu wa kitongoji hicho kujisaidia haja ndogo na kubwa katika makopo nyakati za usiku na muda wa kuingia ndani ni saa 12 ama 12:30 jioni.

Ostach alisema kuwa hali hiyo imekuwa kero kwake kwa hasa kitendo cha kujisaidia haja kubwa na ndogo katika chombo na suala la kuingia ndani saa 12 au umezidisha kukaa nje basi iwe saa 12:30 jioni kuwa maisha hayo yamekuwa hanaya tofauti na mnyama digidigi ama mtu aliye katika kifunguni japo kunakuwa na tofauti ndogo.

“Nilipoelezwa tukio la bibi Hellen kufariki dunia tena amechunwa ngozi niliingiwa na uoga lakini nilikubaliana na ushauri wa wenzangu wa kutotoka nje nyakati za usiku na kama nitakuwa nimebanwa na haja kubwa ama ndogo basi sina budi kujisaidie katika mkopo na asubuhi nitamwaga sasa hali hiyo kwangu imekuwa kero kwangu kwani sijazoea”. Alisema Yusta huku akiwa ameinamisha kichwa chini.

Aliendelea kusema msichana huyu kuwa licha ya kupewa onyo la kutotoka nje nyakati za usiku, jambo lingine aliloelezwa na ndugu zake ni pamoja na kuzingatia muda wa matembezi ukiwemo wa kurudi nyumbani kuwa ni lazima uwe saa 11:30 ama saa 12:30 jioni awe tayari katika mazingira ya nyumbani kwao.

Marehemu Hellen Petri Mahunzila (75) ameacha watoto watatu wakiwemo wa kiume wawili, Kassim Athmani Lingila (58), Banzi Mazangwa (55) na mwanamke pekee, Yustina Kasian (40) na aliachana na mumwe wake miaka 10 iliyopita huku historia yake ikielezwa kuwa maisha yake yote alijighulisha na suala la kilimo.

Akieleza mkasa uliokumkuta mama yake kupotea hadi kifo chake cha mateso, Banzi Mazangwaalisema kuwa mama yake alikuwa mpole na mkimya huku akieleza kuwa hakuwahi kusikia kama amewahi kugombana na mtu yoyote siku za hivi karibuni na alikuwa anafanya kazi ndogo ndogo za nyumbani kutokana na uzee wake.


Mazangwa anasema kuwa mama yao siku za hivi karibuni nyakati za usiku alikuwa anatoka sana nje kwa ajili ya kusaidia haja ndogo, lakini miaka mitatu nyumba aliwahi kumweleza mama kwa kuwa yeye sasa umri aliokuwa nao ni mkubwa inafaa awe anajisaidia haja ndogo na kubwa katika kopo hasa nyakati za usiku wajuu zake watafanya kazi ya kumwaga asubuhi lakini jambo hilo alikataa.

“Miaka mitatu nyumba niliwahi kumweleza mama awe anajisaidia haja ndogo katika kopo nyakati za usiku lakini alikataa na kunieleza kuwa bado ana nguvu za kutembea mwenyewe hivyo haoni haja ya kufanya hivyo”. Alisema Mazangwa.

Akielezea kwa masikitiko tukio hilo la mauaji ya mama yake, Mazangwa alisema kuwa ameshangwa na mauji hayo pamoja na ukatili uliofanywa huku mwili wake ukiwa umechunwa ngozi na kutupwa shambani kwake baada ya kupotea kwa siku 13 kabla maiti yake kuonekana kandao ya shamba lake.

“Eneo ambalo mwili wake ulitupwa kando ya shamba lake, sisi familia tumefika zaidi mara tatu ama nne na watu wengine walifanya hivyo lakini baadaye wananchi katika zoezi la kumsaka kwa siku nane bila mafanikio, wananchi, ndugu, jamaa na marafiki tumeshangazwa eti eneo hilo hilo ambalo watu wamefika na hawajaona kitu, ndipo mwili wake umeonekana ?”. Alihoji Mazangwa.

Kuna siri kubwa imefichika katika tukio hilo na bila shaka baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mgata watakuwa wanahusika na hawawezi kukwepa kuhusika kwao kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo ya mama yake kwanini tangu amepotea alikuwa wapi katika siku 13 zote ? kabla ya kifo chake kama si kuhifadhiwa ndani ya nyumba za mmoja wa wakazi wa Mgata ?.

Aliendelea kusema kuwa wauaji hao ni watu wanaowafahamu vizuri tu familia yao kwani baada ya yeye kuona mwili wa mama yake ulionyesha kuwa amekufa siku moja ama mbili zilizopita kabla ya kuchunwa ngozi na ilionekana ni watu ambao wametumia utalaam wa hali ya juu kuweza kufanikiwa zoezi hilo kupata ngozi ya mama yao.

Siku ya jumatano oktoba 15 mwaka huu majira ya saa 8 mchana ndiyo mwili ulionekana lakini ndugu, jamaa na wananchi wa kitongoji na kijiji Mgata walilala eneo hilo usiku kucha wakiulinda wakati wakisubiri ujio wa daktari, askari polisi na diwani kwa ajili ya uchunguzi lakini cha kushangaza eneo hilo halikuwa na harufu yoyote kama binadamu aliyekufa siku 13 zilizopita. Alisema Mazangwa.

Mazangwa ametoa wito kwa jeshi la polisi kuchunguza tukio hilo kwa kina kwani ana imani endapo watafanya hivyo watafanikiwa kuwabaini wahalifu ndani ya kijiji hicho na wale ambao wameshirikiana nao katika mauaji hayo ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa mkondo wake kwani wananchi sasa hivi wanaishi kama wanyama wanaowindwa na binadamu kwa ajili ya kitoweo.

Diwani wa kata ya Bwakilajuu, Emili Kidevu anasema kuwa tangu kutokea tukio hilo hakuna uchunguzi wowote umefanyika kutoka ndani ya jeshi la polisi zaidi ya kufika siku ya tukio.

Kidevu alisema kuwa kijiji cha Mgata kimekuwa kikipokea wageni wengi ambao wengi wao ni wafanyabiashara wanaoenda kijijini hapo kwa ajili ya kununua zao la iriki hasa katika kipindi cha kuanzia mwezi tano hadi wa nane na tukio hilo limetoka mwezi wa 10 jambo ambalo kwa upande wake anatilia shaka na kujiuliza maswali yasiyo na majibu.

“Jambo hili linavyoonekana halikufanywa na mtu mmoja na kama jeshi la polisi lingefikilia kuweka mitengo katika barabara ya Dakawa-Bwakilajuu, Mgata-Bwakilajuu kutumia askari wa polisi jamii wa vijiji husika nina imani lazima wangeweza kunasa mfuko ya plastiki ama chombo chochote ambacho wamehifadhi ngozi hiyo na kukamata wahalifu”. Alisema Kidevu.

Kidevu aliendelea kutoa ufafanuzi kuwa mitego kama ingetegwa katika kijiji cha Dakawa, Bwakilajuu na Mgata katika barabara ambazo ndizo zinazotumika kuingia na kutoka baada ya kutokea.

Shaka nyingine inayumkumba diwani huyu na jamii ya kitongoji cha Gongo, kijiji cha Mgata na vijiji jirani ni namna tukio hilo lilivyotekelezwa kiutalaamu bila kukosea, kwanza anaweza kusema kuwa marehemu alitekwa, kisha akahifadhiwa ndani ya nyumba kwa siku 1o kabla ya kifo chake.

“Nina imani kama jeshi la polisi likichunguza mauaji hayo wataweza kuwatia nguvuni wahusika hasa kwa kuanzia katika kile kitongoji cha Gongo na kijiji cha Mgata inanipa imani kabisa kulingana na mtirirko wa tukio lenyewe, kwani haiwezekani apotee kwa siku 11 na siku ya 12 ndio mwili wake uwe umeonekana tena umechunwa ngozi kilataalam ?. alihoji Diwani huyu.

Naye Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile akitolea ufafanuzi na kuthibitisha kutokea kwa tukio la marehemu, Hellen Petro (75) kufariki dunia baada ya kupotea kwa siku 11 kisha mwili wake kukutwa umechunwa ngozi siku ya 12 amelihusisha tukio hilo na masuala ya ushirikina.

Shilogile alisema kuwa jeshi la polisi lipo katika uchunguzi wa kuwabaini wauaji na watakapobainika sheria itafuata mkondo wa sheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.

“Hili tukio jeshi la polisi mpaka sasa bado lipo katika uchunguzi, uchunguzi upo wa aina nyingine hilo siwezi kulibainisha kwani itaharibu mitego yetu ila ninachoweza kusema kuwa tunafanya uchunguzi si lazima pale katika kitingiji aonekane askari la hasha”. Alisema Shilogile.

Akifafanua zaidi juu ya uchunguzi wa tukio hilo Kamanda Shilogile aliongeza kwa kusema mpaka sasa bado wanaendelea kukusanya taarifa mbalimbali na nyingine kuzichuja ili kuweza kuwabaini wauaji na wakati mungine uchunguzi unaweza kuchukua zaidi ya mwezi mmoja kabla ya wahusika kunaswa.

Bado mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba baada ya kutokea tukio aliagiza polisi kuanza kazi ya kuchunguza kwani hatuwezi kukamata wananchi ovyo bila kuwa na vyanzo vya uhakika.

Mwili wa kikongwe Hellan Petri Mahunzila (75) aliyefariki dunia kati ya oktoba 14 na 15 mwaka huu ulizikwa majira ya saa 2 usiku ya eneo la Mondo mita chache kutoka eneo alilotupwa kando ya shamba lake baada ya uchunguzi wa daktari wa kituo cha afya Duthumi chini ya askari polisi wa kituo cha Kisaki-Gomero katika wilaya ya hamashauri ya wilaya ya Morogoro.

Kitongoji cha Gongo kijiji cha Mgata kipo umali wa kilimeta 14 ukitokea Bwakilajuu ili kuweza kufika katika kitongoji hicho itakulazimu kutembelea kwa miguu masaa matano kutokana na kutokuwepo kwa barabara inayokuwezesha kutumia usafiri wa gari ama pikipuki huku kijiji cha Bwakilajuu nacho kikiwa na umbali wa kilometa 16 kutoka kijiji cha Dakawa kilichopo barabara kuu ya Mvuha-Kisaki chenyewe kikipitika kwa nyakati zote za masika na kiangazi kwa usafiri wa gari ama pikipiki.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: