DKT Jakaya Mrisho Kikwete na Mama Salma Kikwete na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi Mhe James na daktari wa zamu wakimwangalia Mjumbe wa Tume
ya Katiba Dkt Sengondo Mvungi aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kitengo cha Mifupa (MOI) leo Oktoba 3, 2013 kufuatia
kujeruhiwa kwake na watu wanaosadikiwa ni majambazi usiku wa Jumamos
Oktoba 2, 2013.PICHA NA IKULU.
DAR ES SALAAM.
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Dk Sengondo Mvungi amejeruhiwa usiku wa kuamkia jana, baada ya kukatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake Mpiji-Magohe, jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba,
Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi aliwahishwa kwenye Taasisi ya
Mifupa Hospitali ya Muhimbili (MOI), ambako amelazwa katika wodi
maalumu huku hali yake ikiwa mbaya.
Taarifa kutoka kwa ndugu na watu waliomtembelea
hospitalini hapo wanasema kwamba hali ya Dk Mvungi ni mbaya kwani
alikuwa hawezi hata kuzungumza.
Akisimulia tukio hilo, dereva wa Dk Mvungi
anayeitwa Emmanuel Ntaro, alisema akiwa nyumbani kwake majira ya saa
6:30 usiku, alisikia mlipuko mkubwa kisha zikasikika kelele zikitokea
nyumbani kwa bosi wake.
“Nilifika na kukuta hajitambui, tukampeleka
Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani alikopatiwa huduma ya kwanza
kabla ya kumpeleka MOI ambako anaendelea kuchunguzwa na kupatiwa
matibabu,” alieleza Ntaro.
Alisema kuwa watu wapatao sita, walivamia nyumbani
kwa Dk Mvungi ambako baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani,
walimjeruhi kwa kutumia mapanga huku wakidai wapatiwe fedha. Watu hao
walimsababishia majeraha usoni, kichwani na sehemu nyingine za mwili.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mbali na kupata matibabu MOI, pia
walilazimika kumpeleka Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya vipimo zaidi
katika mashine ya CT Scan kama walivyoshauriwa na madaktari wa zamu.
Mbatia alisema kuwa baada ya Dk Mvungi kufanyiwa
kipimo hicho alirudishwa tena MOI kwa matibabu na uangalizi maalumu.
“Hali yake inaanza kuimarika tofauti na nilivyomuona saa nne asubuhi, “
alisema Mbatia muda wa saa 12 jioni jana alipozungumza na gazeti hili.
Alisema kwamba pia watu waliohusika na tukio hilo waliiba kompyuta mpakato (laptop) pamoja na bastola ya Dk Mvungi.
Kamanda wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Cammilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kweli hilo ni tukio la kihalifu na sisi
tunaendelea kulifanyia kazi. Tunawahakikishia Watanzania kuwa watu hao
watapatikana na kufikishwa kwenye mkono wa kisheria,” alisema. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment