BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS WA MALAWI JOYCE BANDA AANZA TENA KUICHOKONOA TANZANIA, SAFARI HII ADAI AKINA ASHA-ROSE MINGIRO NI WANANCHI WAKE.

RAIS WA MALAWI "JOYCE BANDA" SASA ADAI KUWA MKOA WA RUVUMA NA WANANCHI WAKE WOTE NI MALI YAKE.

Rais Jakaya Kiwete wa Tanzania kushoto na Rais Joyce Banda wa Malawi katika mazungumzo hivi karibuni.


RAIS wa Malawi, Joyce Banda ametajwa kuendeleza chokochoko baina ya nchi yake na Tanzania, huku sasa akidaiwa kutumia redio na runinga za nchini mwake kutangaza kuwa mkoa wa Ruvuma, viongozi na wananchi wa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake.



Aidha, amesitisha safari za meli ya mv Ilala iliyokuwa ikifanya safari kwenye Ziwa Nyasa kusafirisha mazao na wananchi wa ukanda huo upande wa Tanzania.


Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa soka wa Mbambabay juzi, Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba, alisema Rais Banda ambaye aliibua upya mzozo wa mpaka baina ya nchi hizi mbili, kuwa ni mkorofi kutokana na kufanya vitendo vinavyoonesha uhusiano baina ya nchi hizi mbili kuzorota.


Komba alibainisha vitendo hivyo mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akisema imefika mahali Rais Banda anapotosha ukweli kuhusu mpaka kati ya nchi hizo mbili na kudai sehemu ya mwambao wa Ziwa upande wa Tanzania ni yake.


Mbunge huyo alisema jimbo la Mbinga Magharibi ambalo ni Wilaya ya Nyasa, wanasikiliza matangazo ya redio za Malawi, na anazitumia kupotosha umma kuwa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake na wananchi wanaamini hivyo.


Rais Banda anatangaza kupitia vyombo vya habari vya nchi yake ambavyo vinasikika vizuri katika wilaya hiyo kutokana na wilaya ya Nyasa kutopata mawasiliano ya redio na runinga za nchini.


Komba alisema kutokana na wilaya hiyo kukosa mawasiliano ya vyombo vya habari, wananchi wake wanakosa kusikiliza matangazo zikiwamo hotuba za viongozi wa Taifa.


Wananchi wanakosa kusikiliza matangazo zikiwamo hotuba ya Rais Kikwete ya kila mwezi na hotuba za viongozi wengine wa kitaifa wakiwamo Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.


“Kutokana na kukosekana usikivu huo, Rais Banda anatumia nafasi hiyo kutangaza kuwa viongozi wote wa wilaya na mkoa na eneo lote ni mali yake,” alisisitiza Komba.


Aliongeza kwamba watu wote walioko kwenye mkutano huo isipokuwa Katibu Mkuu Kinana, akiwamo Dk Asha-Rose Migiro ambaye alizaliwa Mbambabay wote ni mali ya Rais Banda.


Mbunge huyo alisema wananchi wa eneo hili nao ni Watanzania wanaostahili kusikia na kupata habari za nchi yao, badala ya kusikiliza nyimbo na matangazo ya Malawi ambayo yanakuwa na ajenda zake.


Mbunge Komba alimwomba Katibu Mkuu Kinana kwenda kuhimiza kutekelezwa haraka kwa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ya kuleta meli ili kuwa na usafiri wa uhakika wa mali na wananchi katika eneo hilo.


Kinana alisema ahadi ya meli ya Rais, hiyo ana uhakika itatekelezwa na kufafanua kuwa meli tatu zinatengenezwa Korea Kusini na zitakapokamilika ya Ziwa Nyasa itapelekwa kutoa huduma.


Alisema baada ya Banda kuondoa meli hiyo wananchi wa Mbambabay wanatumia boti dogo kusafirisha abiria na mizigo, hali ambayo inatia shaka.


Kinana alisema amesikia kilio cha Mbunge Komba, kwamba ahadi ya Kikwete itatekelezwa ili kuwapa wananchi usafiri wa meli, ingawa itatumia muda kutokana na kuhitaji muda mwingi kubuni na kutengeneza. CHANZO: HABARI LEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: