BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ALICHOSEMA GODFREY MGIMWA KATIKA KUSAKA RIDHAA YA WANANCHI KURITHI JIMBO LA KALENGA KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA UBUNGE IRINGA.

 
MGOMBEA ubunge wa uchaguzi mdogo Jimbo la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Mgimwa, amesema hajaingia katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kujitafutia utajiri.
“Wapo baadhi ya wanasiasa wanatafuta nafasi hii kwa lengo la kutafuta fedha na sio kuwatumikia wananchi; naomba mniamini mimi sijaingia kwa lengo hilo,” alisema.

Alisema hayo wakati wa kampeni zake alizofanya kwa nyakati tofauti jana katika vijiji vya Ilalasimba, Magubike, Kidamali na Nzihi vya kata ya Nzihi jimboni humo.

Godfrey alisema ametoka kwenye ajira iliyokuwa ikilimpa vizuri kabla ya kuamua kutimiza ndoto yake ya siku nyingi ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.

“Kabla sijaja kugombea ubunge katika jimbo hili, nilikuwa mtumishi wa Benki ya Stanbic makao makuu, huko nilikuwa nikilipwa vizuri sana, lakini nikasema siwezi kuendelea ili nirudi kwenu kwa lengo la kuwatumikieni,” alisema.

Aliwaomba wananchi wa kata hiyo na jimbo hilo kumuamini huku akisisitiza kwamba yeye ni msomi asiye na majivuno, msikivu na asiyekata tamaa anapotaka jambo fulani lifanikiwe.

Katika mikutano kwenye kata hiyo, Godfrey alisema atabeba na kuzifanyia kazi nyingi ahadi zilizotolewa na marehemu baba yake, Dk William Mgimwa, ili kuwaletea wananchi wa jimbo hilo maendeleo.

“Maendeleo ya jimbo hili yataletwa kwa kutekeleza Ilani ya CCM ya 2010 lakini kuna ahadi zilitolewa na Dk Mgimwa nje ya Ilani hiyo; niaminini nitazifanyia kazi,” alisema.

Akiwa katika kijiji cha Magubike alisema wakati wa uhai wake, Dk Mgimwa aliahidi kutoa mabati 400 kwa ajili ya ujenzi wa shule na zahanati ya kijiji hicho.

“Pamoja na ahadi hiyo aliahidi pia kutoa Sh milioni moja kwa kikundi cha wajasiriamali wanawake, nazichukua ahadi hizo na nitazifanyia kazi,” alisema.

Akimuombea kura kwa wapiga kura wa kata hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema katika uchaguzi huo mdogo vyama vinavyoshiriki havishindanishi sera.

“Serikali ilikwishaundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, kinachofanywa sasa ni kuziba nafasi ya mbunge aliyekuwepo, kwa hiyo ahadi zinazotekelezwa ni zile zile zilizotolewa kupitia Ilani ya CCM na mgombea husika,” alisema.

Alisema hiyo ni sababu tosha kwa wana Kalenga kumpa kura za ushindi mgombea wa CCM kwa kuwa ndiye atakayemalizia utekeleza wa Ilani na ahadi za Dk Mgimwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Nchemba aliwahakikishia wana Kalenga kwamba Godfrey ana kila sababu ya kumalizia kazi iliyoanza kutekelezwa na marehemu baba yake ili atengeneze jina.

“Mnajua Uchaguzi Mkuu utakaoshindanisha sera za vyama mbalimbali utafanyika mwakani; kujiweka katika mazingira mazuri ni lazima Mgimwa atatekeleza ahadi anazowapeni katika uchaguzi huu mdogo,” alisema.

Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Dk Mgimwa kufariki dunia Januari mosi mwaka huu wakati akiendelea na matibabu yake Afrika Kusini.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: