DODOMA.
WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amechaguliwa kwa kishindo kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba, huku akisema kuchaguliwa kwake ni sawa na kumrudisha chura kwenye dimbwi la maji.
Jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata kura 487 na kumbwaga mpinzani wake, Hashimu Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma aliyepata kura 69.
Wajumbe wengine, Dk. Terezya Huvisa pia wa CCM na John Chipaka wa Tadea, walijitoa katika kinyang’anyiro hicho ambacho tangu awali Sitta alionyesha kujiandaa kwa kutengeneza vipeperushi alivyovisambaza kwa wajumbe kama sehemu ya kujinadi.
Akizungumza na wajumbe ambao muda mwingi walikuwa wakimshangilia, Sitta alionekana kujiamini kabla na baada ya uchaguzi. Pia alitumia misemo lugha ya picha ikiwamo ya chura kuishi majini, akimaanisha kuwa wajumbe wamemchagua mtu mwenye uwezo, uzoefu na weledi wa kuongoza shughuli za Bunge.
“Jamani kunichagua mimi ni kama kumrejesha chura kwenye dimbwi la maji alilolizoea. Msiwe na wasiwasi ataogelea tu na ninawaahidi kuwa ikiwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu, mtanichagua nitawatumikia kwa uaminifu, sitakubali upendeleo wa aina yoyote, nitasimamia kanuni tulizozipitisha hapa,” alisema.
Aliongeza kusema: “Nitawaongoza kwa utumishi uliotukuka na uadilifu ili tupate Katiba bora, yenye viwango na kwa wakati. Nina hulka ya kuwapenda wale ninaowaongoza, kwa hiyo nitakuwa mtetezi wa shughuli mbalimbali…Ninawaahidi Watanzania kutenda haki na kuwapatia Katiba yenye viwango na kwa wakati.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Sitta alikuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiongozwa na falsafa yake ya Bunge la kasi na viwango. Pia anatajwa kufanikiwa kuliongoza Bunge hilo kwa weledi wa hali ya juu.
Kwa sababu ya mafanikio hayo, alipokuwa akiomba kura za wajumbe wa Bunge hilo, hakusita kujifananisha na chura kurudi majini.
Aidha, alisisitiza kuwa ataliongoza Bunge kwa kutumia falsafa yake ya kasi na viwango, huku akiahidi kulisimamia Bunge kwa haki na bila upendeleo kwa kundi lolote.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk. Thomas Kashillilah, alisema Sitta alipata kura hizo 487 ambazo ni sawa na asimilia 86.5, kati ya kura 563 zilizopigwa.
Dk Kashillilah alisema kwamba mpinzani wa Sittta, Hashim Rungwe ambaye jana tulimwandika kimakosa kuwa anatoka NCCR- Mageuzi alipata kura 69, sawa na asilimia 12.3 ya kura zote. Alisema kura saba ziliharibika.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment