HII NDIYO MBINU MBADALA YA NAMNA YA KUJENGA NDOA YENYE FURAHA NA MAFANIKIO.
MARA zote vijana na wale wote wanaoowa ama kuolewa huwa na shauku kuu ya kutaraji na kuwa na matumaini kuwa ndoa yao itawaletea maisha yenye furaha.
Miezi mitatu mpaka sita baadae wanandoa hawa hubaini kuwa ndoa si jambo jepesi,kumbe ndoa ni jambo linalohitaji subira ya hali ya juu.Vifuatavyo ni vidokezo muhimu vitakavyosaidia mume na mke kujenga mahusiano mazuri na yenye furaha.
INGIA KATIKA MAHUSIANO YA NDOA UKIWA NA NIA THABITI,NA KILA MARA IFANYE MPYA NIA YAKO;
Mnapaswa kuyaingia maisha ya ndoa mkiwa na nia safi ya kutafuta radhi za Allah (SW) pamoja na rehma na baraka zake kwa kukusudia kwamba ndoa ni kitu cha kudumu,kufanya hivyo ndoa yenu hugeuka kuwa ibada kitu ambacho kitakuwa kikiwapatia thawabu,nia thabiti ni jambo la msingi litakalowahakikishia amani,umadhubuti wa penzi pamoja na furaha katika muda wote wa maisha yenu ya ndoa.Na kwakuwa tendo hili ni ibada kila mara ifanyeni mpya nia yenu ili kuhakikisha ya kuwa hamtoki nje ya mstari na kukosa faida zitokanazo na uhusiano aupendao Allah (SW)
KUMBUKA PIA MKE WAKO NI NDUGUYO KATIKA UISLAMU:
Mara nyingi waislamu wamekuwa wakiwajali zaidi watu wa nje ya familia yao, kwa wema na uaminifu lakini huwa na tabia tofauti kabisa anapokuwa na mwenzi wake hili si jambo zuri kwani hupelekea kuchokana haraka,Waislamu wanapaswa kuelewa kuwa mpenzi wako katika uislamu ni nduguyo,unapaswa kumtimizia kwa kukamiliha wajibu wako.Jitahidi kuzielewa ipasavyo haki za udugu wa kiislamu na kuzifata kimatendo.
HIMIZA YALIO BORA KWA MPENZI WAKO:
Kwa kuwa hakuna mwanadamu aliyetunukiwa kila aina ya ubora autakao,basi hamasa iwekwe kwa ule ubora alio nao Asali wako wa moyo,Jitahidi kumtia moyo,kumsifia na kuonesha kuridhishwa na ubora alio nao kila mara,kufanya hivi kutaimarisha ubora wake na kumpa fursa ya kuendeleza vipaji vyengine vya ubora alio nao.Jitahidi kutoyatilia maanani mapungufu madogo madogo aliyo nayo mpenzi wako,yasije kumnyima furaha.''KAMA ALIVYOSEMA MTUME (SAW) KUWA:''MWANAMME MWENYE KUAMINI ASIMDHURU MWANAMKE MWENYE KUAMINI,KWANI ANAWEZA KUCHUKIZWA NA TABIA MOJA LAKINI AKAMPENDA NA KUMRIDHIA KWA TABIA NYENGINE.''(Muslim)
KUWA RAFIKI WA KARIBU WA MPENZI WAKO:
Tafakari vipi rafiki wa karibu anapaswa kuwa(best friend) kisha uwe hivyo kwa mwenzi wako,hii inajumuisha kushirikiana katika anavyovipenda,kuujua uzoefu wake,ndoto zake za kimaisha,matatizo yake na hata kukata tamaa kwake.Na hili linawezekana tu pale unapojua mahitaji ya mpenzi wako (anapenda nini hapendi nini) kisha umsaidie kadiri itakavyowezekana.kwani rafiki wa karibu ni mtu unaepaswa kumtunzia siri,kumwamini,kumtegemea katika maisha,hivi ndivyo mpenzi wako anavyohitaji katika maisha yenu ya kila siku.
USIWEKE MATARAJIO YASIO WEZEKANA KWA MWANDANI WAKO:
Mara nyingi kabla ya ndoa watu wengi huwa na mawazo ya kinjozi,kuhusu mke au mume mtarajiwa wengi hutegemea kumwona awe amekamilika kila nyanja,katika uhalisia ni vigumu kumpata mtu aliye kamilika kwa kila jambo.Vinginevyo mawazo hayo husababisha kero na matatizo yasio na muhimu katika ndoa yako.Yafaa tuzingatie Allah( sw) amemjaalia mwanadamu kuwa ni mwenye mapungufu mengi hivyo tutegemee kasoro nyingi,kwa kuzingatia hili la mapungufu ya kibinadamu na kujitahidi kwako kurekebisha mapungufu hayo ya mwenzio,basi uatashangazwa na kuona ndoa yenu itakavyokuwa na maridhiano.
TUMIENI MUDA WA THAMANI PAMOJA:
Mnapaswa kutafuta muda wa ziada katika ratiba zenu ngumu za kimaisha ,kuimarisha penzi lenu kwa kuwa pamoja,na muda wa thamani unaokusudiwa hapa ni kama vile kufanya safari fupifupi pamoja ,au hata kufanya shughuli itakayoruhusu uwili wenu nje ya maisha ya nyumba yenu na mengine mengi mfano wa hayo.
ONESHA HISIA ZAKO MARA ZOTE:
Njia ya mawasiliano yenu yapaswa kuwa wazi na tayari kupokea hisia za mwenzi wako kila zinapoibuka,hii nitiba mujarab ya nafsi,Lakini kuna hatari kubwa kunyamazia hisia za mwenzi wako hasa za kimapenzi.Jitahidini kukidhiana haja.
KIRI MAKOSA NA JENGA TABIA YA KUOMBA MSAMAHA:
Kama tufanyavyo katika kumuomba Allah (sw) msamaha kila mara tukoseapo,hivyo ndivyo tunapaswa kufanya kwa wapenzi wetu,kwani mtu mara na mwenye nguvu ni yule ambae yuko tayari kukiri pale anapokosea,na kisha kuomba msamaha.Baada ya hapo ongeza juhudi kuboresha yale yote yanayoongeza mapenzi,mwanandoa asiye tayari kufanya hivi ategemee maendeleo duni yakimahaba katika ndoa yao.
USIPENDE KUIBUA MAKOSA YA WAKATI ULIO PITA:
Uislamu unakataza mtu kujikita na kusimamia mambo yalio kwisha pita.Mtu anapaswa ayakumbuke makosa yaliyopita ili yasije yakarejewa tena,lakini hili lisiwe linafanywa kupita kiasi,bila shaka sisi kama binadamu hatuna haki yakuwahukumu bianadamu wenzetu.twaweza kuwashauri tu tena kwa kuzingatia maadili.
BAADHI YA WAKATI MSTAAJABISHE MKE WAKO:
Kuna namna nyingi za kumstaajabisha mpenzi wako,kama kumlete zawadi ndogondogo au hata katika muda ambao hakuutegemea,au kumuandalia mlo maalum au kumvalia mavazi ya kupendeza au kujipendezesha,kwa naman nyengine yoyote aipendayo mahabubu wako,hii ni ka wanawake na wanaume. Lengo kuu ni kuyatia ladha mapenzi na uhusiano wenu wa kindoa kwa kuepusha kwa kupesha ratiba zenye kuchosha.
KUWA NI MWENYE MZAHA NA UTANI BAADHI YA NYAKATI:
Uchangamfu,ucheshi,na utani usiopindukia mipaka ya uislamu kwani ni miongoni mwa mambo yanayoongeza ladha ya mapenzi katika ndoa,utani huzuia mabishano na hufungua nuru ya mapenzi katika familia,Kwa kuwa maisha ni mkondo wenye changamoto nyingi na mitihani,kuyaendea vyema maisha hayo humuia rahisi yule mwenye moyo mkunjufu na uliojaa maskhara ya kimapenzi.Hata kama upatikanaji riziki yenu ni mdogo basi utamuona mwandani wako hachoki kuwa nawe popote utapokwenda
0 comments:
Post a Comment