BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KURA YA SIRI YANUKIA KUTUMIKA KATIKA KUAMUA MAAMUZI VIKAO VYA BUNGE MAALUM LA KATIBA DODOMA.


Mwenyekiti mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akizungumza na mwandishi wa Mwananchi, Fidelis Butahe nyumbani kwake mjini Dodoma juzi. Na Mpiga Picha Wetu.


DODOMA.
MWENYEKITI Mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano wa kutumia kura ya siri katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya Katiba.

Sitta aliyechaguliwa juzi kushika wadhifa huo, alisema atashirikiana na kamati ya uongozi itakayoundwa ya wenyeviti wa Kamati 15 za Bunge hilo na kamati ya ushauriano kupata jawabu la suala hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani kwake mjini Dodoma juzi, Sitta alisema: “Unajua kuna baadhi ya vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba ni vizuri vipigiwe kura ya wazi na vingine ambavyo ni nyeti zaidi vipigiwe kura ya siri.”
Alisema si vizuri vifungu vyote vipigiwe kura sawa, yaani si lazima zote ziwe za siri au ziwe za wazi.
Alitoa mfano wa ibara inayosema kutakuwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na kusema: “Hatuwezi kushindana katika suala la kuwapo kwa Mahakama na ni wazi kuwa jambo hilo mnaweza kupiga kura ya wazi. Nasema hivyo kwa sababu Katiba yoyote lazima ionyeshe mihimili yote ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.”
Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alishinda kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika juzi kwa kura 487 kati ya 563 (sawa na asilimia 85).
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki ambaye kaulimbiu yake ni ‘kasi na viwango’, alisema vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba vinavyoweka misingi ya Katiba, ni vizuri vikapigiwa kura ya siri.
“Unajua tuna viongozi wa dini na halitakuwa jambo la busara kama tukizijua hisia zao. Kama wewe uko karibu na imamu au askofu halafu anapiga kura ya wazi ya kutaka Serikali tatu wakati wewe muumini unataka Serikali mbili ni wazi kuwa jambo hilo linaweza kuleta hisia tofauti na kuwanyima watu haki na uhuru wa kuamua,” alisema Sitta.
Alitoa mfano wa Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba inayozungumzia Serikali na muundo wa madaraka katika Jamhuri ya Muungano na kufafanua kuwa katika sura hiyo atapendekeza ipigiwe kura ya siri.
Kuhusu suala hilo la muundo wa Serikali alisema: “Kikubwa ni wajumbe kujenga hoja, hatuwezi kwenda na misimamo isiyobadilika kwa sababu tunataka maridhiano. Nitatenda haki na nitatoa muda mrefu zaidi kwa wajumbe kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo zina uzito mkubwa kuliko sura nyingine ambazo ni za maelezo tu. Mfano suala la haki za binadamu ambazo wote tunakubaliana nazo.”
Alisema wakati wa kujadili muundo wa Serikali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifika, ataishauri kamati ya uongozi, kutenga muda wa ziada katika suala hilo na mengine yenye utata.
Mwenyekiti huyo alisema suala la upigaji kura linatakiwa kuamuliwa kwa busara na atatumia hekima zake na za wajumbe wa Bunge hilo, kutatua mgogoro wa kura ya siri au ya wazi. MWANANCHI 
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: