MGOMBEA ubunge wa Uchaguzi Mdogo Jimbo la Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Mgimwa jana aliiteka kata ya Wasa katika kampeni za kuomba kuwa mwakilishi wa wananchi bungeni kupitia jimbo hilo. Katika kila kijiji alichopita katika kata hiyo, Mgimwa alilazimika kutumia dakika 10 hadi 20 kusalimiana na wapiga kura wake kwa kushikana nao mikono.
Katika mikutano yake tofauti kwenye vijiji vya Usengelendete, Mahanzi, Ihomasa, Ikungwe, Wasa na Ufyambe, hotuba yake ilikuwa ikikatizwa mara kwa mara na makofi ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza.
“Nawapenda kama navyoipenda familia yangu; nawahakikishieni kwa kupitia mbinu mbalimbali za utekelezaji wa Ilani ya CCM nitahakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010 zinatekelezwa,” alisema.
Aliwataka wananchi wa kata hiyo na jimbo hilo kwa ujumla, kumchagua ili atumie maarifa aliyonayo kuwaletea maendeleo.
“Msinipime kwa umbo langu dogo, nipimeni kwa utekelezaji wa ahadi ninazotoa; nawahakikishieni mtoto wa nyoka ni nyoka, ahadi zote zilizotolewa na marehemu baba yangu nitahakikisha zinatekelezwa,” alisema.
Alisema ana elimu nzuri, ambayo hataki kuitumia kwa kazi nyingine yoyote, ila kwa kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo kuharakisha maendeleo.
Alisema anafahamu changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, maji, elimu, afya, barabara na umeme katika jimbo hilo. Aliahidi baada ya kuapishwa atawabana baadhi ya viongozi ili wamsaidie kuzitekeleza.
“Mtu wa kwanza atakuwa Waziri Mkuu akiwa kama msimamizi wa shughuli za serikali bungeni; lakini na mawaziri wa sekta nyingine zinazohitaji ufanisi katika jimbo hili,” alisema.
Mmoja wa wapigadebe wa mgombea huyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe alisema, “huu ni uchaguzi mdogo, sio uchaguzi ambao kila chama kinachoshiriki kinatafuta ridhaa ya wananchi ili kiunde serikali.”
Alisema litakuwa jambo la kushangaza, kama wananchi wa jimbo hilo watampa kura mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili akawa mwakilishi wao. Akitoa mfano, alisema haiwezekani mtu mwenye suruali nyeusi iliyotoboka, akaweka kiraka cha kitambaa chenye rangi nyeupe.
“Aliyekuwa mbunge wa jimbo hili ni mwana CCM, sasa tunawezaje kuziba pengo lake kwa kuweka mbunge kutoka chama kingine,” alisema katika mikutano hiyo.
Alisema Chadema wanajua kwamba katika uchaguzi huo, wameingia wakiwa wanaenda kushindwa na sasa wanazo kazi mbili, wanazoendelea kufanya jimboni humo.
Alitaja kazi hizo kuwa ni pamoja na kutumia wafuasi wao kutoa Arusha na Kilimanjaro, kuwashawishi kwa fedha baadhi ya wana CCM ili wawauzie shahada zao za kupigia kura.
“Lakini pili wanatengeneza mazingira ya fujo ili kuwaogopesha wazee, kinamama, kinababa na vijana ili wasijitokeza kwa wingi kumchagua mgombea wao wanayemtaka,” alisema.
Aliwaomba wananchi kushirikiana na viongozi wa CCM katika maeneo yao kwa kutoa taarifa za watu hao ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / MGOMBE UBUNGE WA CCM UCHAGUZI MDOGO AITEKA KATA YA WASA JIMBO LA KALENGA IRINGA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment