PROFESA LIPUMBA, MBOWE WATAMJIBU RAIS KIKWETE JUU YA HOTUBA YAKE YA UZINDUZI WA BUNGE MAALU LA KATIBA MJINI DODOMA.
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamesema watajibu hotuba ya Rais Kikwete kwenye Bunge Maalum la Katiba na nje ya Bunge kwa kutumia taarifa mbalimbali za tume ya marekebisho ya katiba ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina. Katika mazungumzo yao na waandishi wa habari jana, viongozi wa umoja huo ambao ni kutoka vyama vya upinzani pia walishukuru wabunge wao kwa kutotoka nje ya Bunge wakati Rais Kikwete anahutubia licha ya kuwa hotuba hiyo haikuwafurahisha kabisa.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema watakachojadili bungeni ni rasimu ambayo imetokana na maoni ya wananchi ambayo imewasilishwa bungeni na mwenyekiti wa tume ya marekebisho ya katiba, Jaji Joseph Warioba na ndicho ambacho watakisimamia na sio vinginevyo.
“Hotuba ya Rais sio rasimu iliyoko bungeni, ule ni msimamo wa CCM na unafahamika tangu mwanzo, hivyo kazi ya Bunge hapa ni kujadili rasimu ya wananchi na kuainisha maoni ya tume,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Bunge limepewa kazi ya kujadili rasimu iliyopelekwa bungeni hapo na sio kujadili hotuba ya mwenyekiti wa CCM.
“Wale ambao wanataka kujadili rasimu ya Rais Kikwete ambayo ni rasimu ya CCM waende makao makuu ya chama hicho watajadili lakini bungeni tutajadili rasimu.”
Profesa Lipumba alisema alichofanya Rais Kikwete ni kuwasilisha msimamo wa chama chake ambao alisema unapingana na maoni ya wananchi.
Alisema watatumia bango kitita ambalo lina sababu zote za tume kupendekeza rasimu hiyo.
Alisema bango kitita lina majibu na wale ambao watapinga pendekezo la tume waje na majibu ya kile kilichoainishwa kwenye rasimu na taarifa za tume na sio kutumia hotuba ya Rais ambayo ni maoni ya chama chake.
“Tume ina majibu ya hoja zetu, tutajenga hoja na hatuko tayari kujadili rasimu nyingine zaidi ya hii tuliyoletewa na tume, napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa pamoja na vitisho vilivyotolewa na Rais katika hotuba yake, lakini majibu yapo kwenye taarifa za tume,” alisema Profesa Lipumba.
Tundu Lissu katika mazungumzo yake alisema kuna mjadala mzito ambao unatakiwa kujadiliwa kuhusu muungano iwapo kweli Zanzibar itaruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa, kukopa ni sawa na kuwapa mamlaka kamili kisiwa hicho.
Lissu alisema wana majibu ya kina ya kujibu hotuba ya Rais na akasema kwamba hoja alizozitoa Rais kuhusu muungano na mamlaka waliyoipa Zanzibar yatatoa majibu ya kuwepo kwa serikali tatu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema alisema kitendo cha Rais Kikwete kubeza maoni ya wananchi ni hatua mbaya kwa kuandika katiba ya wananchi na akaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuvuruga uandikaji wa katiba hiyo.
“Hapa Amos Wako (mwanasheria mkuu zamani wa serikali wa Kenya) ametuonya kuwa katiba yao ilikataliwa na wananchi baada ya serikali kuingilia mchakato wenyewe, na hiki ndicho Rais amefanya,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti wa Ukawa, James Mbatia alisema Rais Kikwete amekinzana na hotuba yake aliyoitoa Desemba 30 akiwataka wanasiasa kuweka itikadi za vyama vyao pembeni na kuheshimu maoni ya wananchi, lakini yeye amegeuka na kufanya propaganda ya chama chake.
Alisisitiza kuwa msimamo wake kuhusu Zanzibar kwamba wataruhusiwa kujiunga na taasisi za kimataifa, bado linahitaji mjadala mpana kwenye katiba, kwani ni sawa na kuipa uhuru Zanzibar wakati Tanganyika haina uhuru huo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment