Ukumbi wa bunge maalumu la katiba jijini Dodoma.
DODOMA.
TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya Mwalimu Nyerere Idealogy Conservation Society ya jijini Tanga, imefungua Kesi Mahakama Kuu ikitaka kuzuia mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya Mwalimu Nyerere Idealogy Conservation Society ya jijini Tanga, imefungua Kesi Mahakama Kuu ikitaka kuzuia mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Taasisi hiyo inapinga mchakato huo wa Katiba kwa
kile inachodai kuwa ni kasoro zilizojitokeza, ikiwamo wananchi kukosa
uwakilishi uliotokana na ridhaa yao, posho kubwa wanayolipwa wajumbe na
gharama kubwa zilizotumika katika maandalizi ya Bunge hilo.
Kesi hiyo ya madai namba 02/2014, ilifunguliwa
Februari 17, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga na mwenyekiti
wa taasisi hiyo, Dk. Muzzammil Mussa Kalokola.
Washtakiwa katika kesi hiyo iliyofunguliwa kwa
stakabadhi ya malipo ya Serikali namba 49803745, ni Waziri wa Sheria na
Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), (kwa sasa ni Frederick
Werema) na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji
Mstaafu, Joseph Warioba.
Hata hivyo Jaji Werema na Jaji Warioba wamesema hawana taarifa za kesi hiyo.
Dk. Kalokola alisema katika hati yake ya madai kuwa anataka mchakato huo wa Katiba usitishwe kwa kuwa umevunja Katiba iliyopo.
Amesema Katiba ya sasa imekiukwa katika Muundo wa
Bunge la Katiba na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika utekelezaji wa
majukumu na wajibu wake wa kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya
Madadiliko ya Katiba ibara ya 98.
“Vilevile imeshindwa kuzingatia hadidu za rejea
kama zilivyoainishwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83,”
alisema Dk Kalokola.
Dk. Kalokola alifafanua kuwa Katiba ya sasa
imeweka masharti kadhaa, ikiwamo utaratibu wa namna ya kuibadilisha na
sheria nyingine ambazo zimeanishwa katika ibara ya 98 na Sheria ya mwaka
1984 Na.15 ib.14.
“Ibara ya 98 (1) Bunge laweza kutunga sheria kwa
ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii kwa kufuata kanuni
zifuatazo,” alisema huku akiinukuu ibara hiyo na kuendelea:
“Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha
masharti yoyote ya Katiba hii (isipokuwa yale yanayohusika na aya ya (b)
ya ibara hii ndogo) au masharti yoyote ya sheria yoyote iliyotajwa
katika orodha ya Kwanza kwenye Nyongeza ya Pili utaungwa mkono kwa kura
za wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya wabunge wote.
“Muswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha
masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya sheria yoyote
yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya
Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni mwa Katiba hii,
utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za wabunge ambao idadi yao
haipungui theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Bara na
theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment