WAKAZI WA PUGU KINYELEZI WALA CHAKULA CHA MCHANA HUKU WAKIWA WAMEJIFUNIKA CHANDARUA KUEPUKA INZI JIJINI DAR ES SALAAM
KATIKA harakati za kujikinga na maradhi na usumbufu wanaoupata wa nzi majumbani, wakazi wanaoishi karibu na eneo la Dampo la Pugu Kinyamwezi, Ilala jijini Dar es Salaam wamebuni mbinu mpya za kukabiliana na tatizo hilo na sasa familia zinalazimika kula chakula zikiwa ndani ya vyandarua. Na imefahamika kuwa, ili kutochosha vyandarua vyao, familia nyingi katika eneo hilo zinakuwa na vyandarua vya ziada, vingine vikitumika wakati wa chakula na vingine usiku wakati wa kulala.
Wakati wa chakula, familia hizo hulazimika kufunga chandarua ama sebuleni au barazani na baba, mama, watoto na wanafamilia wengine huingia ndani yake na kuzuia vizuri mianya ya nzi kuingia kwa kuweka mawe ama mbao na kisha hupata ahueni ya kula bila kuandamwa na nzi.
Hata hivyo, pamoja na ubunifu huo uliotoa nafuu kwa kuwapunguzia maradhi, hali za afya kwao bado ziko hatarini kutokana na harufu kali ya kemikali na taka zinazotupwa katika dampo hilo pamoja na hatari ya kupata saratani kutokana na moshi unaofuka mara kwa mara.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki katika makazi yao yaliyopo karibu na dampo umbali wa kutengwa na barabara inayoingiza magari yanayotupa taka eneo hilo, walilalamikia hali hiyo na kueleza kuwa wameamua kubuni mbinu hiyo ili kunusuru afya zao.
Maua Hamisi (22), Mkazi wa Mtaa wa Kichangani Majohe alisema watoto katika familia wamekuwa wakiugua vifua, matumbo ya kuhara, mafua na malaria kila kukicha kutokana na madhara ya dampo hilo na familia takribani zote, sasa wanalazimika kununua vyandarua zaidi ya viwili kwa ajili ya matumizi hayo.
“Hapa kwetu ‘neti’ (vyandarua) hazina kazi ya kuzuia mbu tu usiku au mchana, bali tunazo zaidi ya mbili na familia nyingi tunazitumia kwa chakula pia, tunazifunga kwa kamba ama misumari ukutani sebuleni ama barazani na tunaweka mawe ama vipande vya miti au mbao kwa chini ili nzi wasiingie kisha tunaingia wote haraka haraka na kuanza kula tukiwa ndani ya neti,” alisema Maua.
Alisema mara zote wanapotaka kula iwe chai, mlo wa mchana ama usiku wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa jambo la ajabu ni kwamba nzi hao hawalali hata usiku ni wasumbufu kama wanavyofanya mchana.
Maua alisema mbali na hatua hiyo, lakini pia wamekumbwa na madhara mengi ya kuugua vifua. Gazeti hili likiwa eneo la tukio linalokaliwa na takribani kaya 200, lilishuhudia wingi wa nzi hao katika bustani za mboga katika makazi ya watu, ukutani na walikuwa wakitua na kuruka kwa wingi kwa watu akiwemo mwandishi wa habari hizi. Awali waandishi walipofika eneo hilo na kuvuta hewa, walianza kuumwa matumbo na vichwa.
Watoto walionekana pembezoni mwa dampo wakicheza huku nzi wakiwa midomoni, puani na maeneo mengine ya mwili, maji machafu kutoka katika dampo yakiwa yanapita na kuingia katika makazi yao huku watoto hao wakicheza kwenye maji hayo wakiwa pekupeku.
Baadhi ya watu walionekana katikati ya dampo wakiokota vyuma chakavu, chupa na vifaa taka vingine bila vifaa vya kinga. Mkazi mwingine wa eneo hilo, Sharifa Mohamed (30) anayeishi katika bonde la dampo, alikiri kula akiwa ndani ya chandarua yeye na familia yake na kueleza kuwa moshi huwa unafuka mara kwa mara kutokana na taka kujipekecha hivyo watoto na watu wazima wanaoishi eneo hilo wapo hatarini kuathirika na saratani muda si mrefu.
Aliomba Serikali kuboresha miundombinu ya dampo hilo kwa kuweka kemikali zitakazoua wadudu hatari kama nzi, mende na mbu na kuzuia harufu mbaya na moshi kufika katika makazi yao.
Alisema miezi mitatu iliyopita waliandamana na kufunga barabara ya kuingia dampo, Serikali ikawaahidi itaboresha eneo hilo, lakini hakuna lolote lililofanyika mpaka sasa.
“Uongozi wa Manispaa ulikuja hapa na kuahidi wataboresha miundombinu ya eneo hili, siku hiyo walimwaga dawa na nzi walipungua kabisa hata moshi haukuwepo, baada ya siku chache, walirejea kama walimwagwa vile, hali ikawa mbaya zaidi ya awali,” alieleza Sharifa.
Nao Moses Lucas na Seif Mbelwa, wakazi wa eneo hilo, walidai kwa nyakati tofauti kuwa, hali za afya kwa wakazi wa eneo hilo ni tete na zipo hatarini kutokana na mazingira yaliyopo hasa nyakati hizi za mvua na kuongeza kuwa, japo wanakula kwenye chandarua, lakini watoto wanacheza kwenye maji machafu yenye kila aina ya madhara kutoka katika dampo hilo.
“Ni hatari mwanadamu kuishi na nzi, mdudu aliyeumbiwa kuishi katika uchafu, zaidi ya saa 24, siku saba, majumba 52 na siku zaidi ya 360 tunaishi na hawa viumbe, harufu mbaya, moshi na hali ngumu ya maisha, tunaomba Serikali iboreshe eneo hili maana dampo lilipoletwa hapa, lilikuta baadhi ya watu,” alisema Eliudi Bihurumba.
Baadhi ya watoto waliozungumza na gazeti hili, Rashid Abdallah (12) na Bariki Massawe (11) walisema kwa nyakati tofauti kuwa wanalazimika kufukuza nzi ndani kwa muda wa nusu saa kabla ya kuweka neti na kula chakula na kuongeza kuwa, moshi, harufu na maji machafu yanahatarisha afya zao.
Mwenezi wa Dampo aliyetajwa kwa jina la Projest Mwemezi, awali juzi hakupatikana kuzungumzia changamoto hiyo kwa wakazi hao na hatua za Serikali kuboresha miundombinu hiyo.
Hata hivyo uongozi wa Manispaa ya Ilala ulinukuliwa ukieleza kuhusu eneo hilo kuboreshwa na kwamba asilimia kubwa ya wakazi waliokaribu na dampo, walilikuta dampo hilo tayari.
Lakini baada ya juhudi za gazeti hili, Mwemezi jana alipatikana na kuzungumzia hali hiyo, akisema Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi alifika eneo la tukio mwaka jana na kuunda kamati ya wananchi itakayoshughulikia kwa kushirikiana na Serikali, kero zote, ikiwemo ya nzi, maji machafu na miundombinu mingine.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Juma Hamis hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo lakini mjumbe mmoja wa kamati hiyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema kamati yao kwa kushirikiana na serikali inashughulikia suala hilo ingawa alikiri wazi kuwa, japo dampo lipo eneo hilo tangu mwaka 2007, wananchi wanaendelea kujenga kwa kasi wakiamini Serikali italihamisha.
Wakati dampo hilo linaanzishwa, ilielezwa kuwa litakuwa la kisasa likiwa na miundombinu inayojali ujirani na makazi ya watu na pia kuzuia uwezekano wa magonjwa ya mlipuko.
Dampo hilo kwa sasa miundombinu yake na namna ya utupaji taka ni wa shaka zaidi na huenda ukasababisha tatizo kubwa katika siku za usoni.
Masaburi alipotafutwa kwa njia ya simu kwa zaidi ya siku mbili, hakupatikana kuweza kulizungumzia suala hilo, kama ilivyokuwa kwa maofisa wengine wa Manispaa ya Ilala.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment