WARIOBA:‘TUMEMALIZA KAZI YETU’ ALICHOZUNGUMZA RAIS KIKWETE NI MAONIN YAKE.
DODOMA.
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua Bunge na kuponda ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema jukumu walilopewa kwa mujibu wa sheria wamelikamilisha na wanawaachia wananchi waamue.
Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi, Jaji Warioba alisema alichokizungumza Rais Kikwete ni maoni yake na kwamba hawezi kuyajadili.
“Rais Kikwete alichozungumza ni maoni yake, kwa sasa sipendi kuyazungumzia hayo, ” Jaji Warioba alieleza.
Alisema wamemaliza jukumu walilopewa na kwamba sasa jukumu lote lipo mikononi mwa Bunge.
Jaji Warioba alisema Tume yake ilikusanya maoni kutoka kwa wananchi, mabaraza ya wilaya ya Katiba na Taasisi mbalimbali, wakatengeneza rasimu ambayo sasa wameikabidhi kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Jaji Warioba pia alikataa kuzungumzia zogo lililoibuka bungeni na kusababisha rasimu kuwasilishwa Jumatano, baada ya kikao cha Jumanne kuvunjika.
Hali hiyo ilitokana na UKAWA kudai muda wa saa 1:30 uliokuwa umepangwa Jaji Warioba ahutubie bungeni uongezwe na kanuni inayoelekeza Rais Jakaya Kikwete ahutubie kabla Jaji Warioba hajawasilisha rasimu izingatiwe, baada ya kutangazwa kuwa Rais angehutubia baada ya rasimu kuwasilishwa.
Profesa Baregu
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu alisema alitarajia Rais Kikwete angezindua Bunge Maalumu na siyo kutoa maagizo na vitisho kwa wajumbe.
Alisema hajui lengo la Rais kufanya alichofanya lakini ana hakika kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotokana na maoni ya wananchi ndani ya rasimu, ameingilia kazi za Tume na hivyo amevunja Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83 toleo la mwaka 2012), inayosema:
“21.-(b) atakayejifanya kuwa mjumbe wa Tume au Sekretarieti; au (c) atakayeendesha programu ya elimu juu ya mabadiliko ya katiba kinyume na masharti ya sheria hii, atakuwa ametenda kosa.
(3) atakayetiwa hatiani kwa kutenda kosa kinyume na Sheria hii, atawajibika kulipa faini isiyopungua Sh2,000,000 (milioni mbili) na isiyozidi Sh5,000,000 (milioni tano) au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na usiozidi miaka mitatu au adhabu zote mbili.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment