BAJETI YA MWEKYEMBE YATIKISA BUNGE LICHA YA KUPITA.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15 bungeni Dodoma, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Dodoma.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana usiku alikuwa katika wakati mgumu wakati Bunge lilipoketi kama Kamati ya Matumizi, kiasi cha kutishia bajeti ya wizara yake kukwama.
Hata hivyo, Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15 yalipitishwa.
Wabunge wa vyama vyote walimbana Dk Mwakyembe na kutoa shilingi karibu katika kila kifungu wakihoji mambo mbalimbali hasa juu ya mgogoro wa umiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), uimarishaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), usafiri wa majini hususan usalama wa meli ya Mv Victoria.
Sakata la Uda
Sakata hilo la Uda lilisababisha mvutano baina ya Naibu Spika, Job Ndugai na Dk Mwakyembe ambaye alilalamikia mjadala wa Uda kuruhusiwa katika hotuba ya wizara yake.
Hata hivyo, Ndugai alipangua hoja hiyo akisema mbali na kwamba Uda inagusa wizara nyingi, lakini ni suala linalohusu uchukuzi hivyo ilikuwa sahihi kujadiliwa katika mjadala huo.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla ndiye aliyeibua suala hilo kwa kuhoji sababu ya Serikali kutoa taarifa zinazokanganya kuhusu Uda, hali kamati anayoiongoza ilishakaa na pande zote husika wakiwamo wataalamu na kuwa na hitimisho kwamba Kampuni ya Simon Group Ltd ni waendeshaji halali wa shirika hilo.
Hoja hiyo iliibua mjadala ambao pia ulichangiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba ambaye alisema Simon Group Ltd waliuziwa kihalali hisa za Uda na kwamba wamiliki hao wanazongwa kutokana na kwamba ni ngozi nyeusi (Watanzania).
Kwa upande wake, Waziri Kivuli wa Uchukuzi, Moses Machali alisema maelezo ya Serikali kuhusu umiliki wa Uda yana mkanganyiko, hivyo Simon Group Ltd wanaandamwa bila sababu za msingi.
Kwa upande wake Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Serikali inajiweka uchi, kutokana na majibu yanayokinzana kutoka kwa mawaziri na Kamati za Bunge.
Hoja ya Mbowe ilipingwa na waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), aliyesema Serikali haijajivua nguo na kwamba itachukua hatua za kuliweka sawa kwa kutoa taarifa moja.
Awali, akihitimisha hotuba yake huku akipangua hoja mbalimbali za wabunge, Dk Mwakyembe alisema mwaka 2012/2013 ilikuwa ni kuitoa Sekta ya Uchukuzi kutoka katika chumba cha wagonjwa mahututi.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment