BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KWANINI PENZI LA KWELI HALICHUJI ?, HIZI NI NJIA ZA KULIFANYA LISIJUCHE SIKU HADI SIKU !!!.


KWANINI penzi kuchuja ?. Ipo hali ya kujisahau baada ya wapenzi kuwa katika uhusiano kwa muda mrefu, haieleweki kama ni tabia ya mtu au ni uhalisia wa mambo kwa sababu ukweli ulio wazi ni kwamba, mwanzo wa uhusiano wengi hujitahidi kufanya mambo mengi ya kuwafurahisha wapenzi wao lakini kadiri siku zinavyosogea, penzi huanza kuchuja.

Kama huamini katika hili, kwa mwanamke, hebu rudisha nyuma kumbukumbu zako kipindi kile ambacho ndiyo jamaa kaamua kukueleza wazi kwamba anakupenda halafu angalia na sasa hivi, utabaini kwamba kuna tofauti kubwa sana.

Huenda mlikuwa na desturi ya kununuliana zawadi kama maua, kadi na chokoleti lakini tabia hiyo huenda ikawa imeyeyuka, hakuna kati yenu atakayekumbuka kitu hicho, ni wachache sana ambao wanakwenda na wakati ndiyo huendelea kuzingatia hayo.


Kuna wale ambao walikuwa na tabia ya kukutana mara kwa mara kimapenzi ambapo kila mmoja alitaka kumuonesha mwenzie jinsi alivyo hodari au fundi wa ‘kuyarudi’ ndani ya uwanja wa mapenzi lakini yale manjonjo huadimika kabisa.


Kawaida yenu ilikuwa kubadilisha hoteli kwa ajili ya chakula cha jioni lakini tabia hiyo hutoweka, labda kila wiki ilikuwa lazima muende ‘out’ mara tatu katika kumbi tofauti za starehe na kufurahia mapenzi yenu, hali hiyo itabaki historia tu.


Hivi hujawahi kusikia mtu anasema: “Enzi zile naanza uhusiano na mpenzi wangu mapenzi yalikuwa motomoto, kila wiki ilikuwa lazima twende beach lakini siku hizi nikigusia tu kwenda huko ni ugomvi.”


Maneno kama haya huwa yananiuma sana hasa ninapogundua kwamba walio wengi wanakuwa na nguvu ya soda pale wanapoingia katika uhusiano lakini baada ya muda mambo hubadilika kabisa.


Sijajua ni kwa sababu gani lakini kwa utafiti mdogo ambao nilioufanya kwa baadhi ya wanaume ni kwamba, wao wanapofanikiwa ‘kuona ndani tu’ hujenga kiburi fulani kwa wasichana wao huku wakiamini kwamba, hata wawe tofauti vipi hawawezi kuachwa!


Labda nijaribu kushauri kitu katika hili kwamba, kama uko kwenye uhusiano wa kimapenzi au uko ndani ya ndoa, unatakiwa kufanya kila linalowezekana kulifanya penzi lenu lisichuje.


Wewe ndiyo unaweza kulifanya likaendelea kuonekana kuwa jipya kila siku au kulifanya likachuja mithili ya nguo inayochuja rangi iliyotumbukiza katika ndoo ya maji ya moto.


Hatukatai kwamba, kuna mabadiliko ya kimaslahi, pengine mtu na mpenzi wake wameketi na kuona wanatumia pesa nyingi viwanja, kwa hiyo wanaamua kupunguza au kuacha ili kujenga maisha bora ya baadaye, si unajua tena mnapokuwa na malengo ya kimaisha zaidi?


Lakini ukweli unabaki palepale kwamba, penzi la dhati haliwezi kuchuja hata siku moja. Tujue wapo ambao wameishi miaka zaidi ya hamsini lakini penzi lao bado ni la moto licha ya kuwepo kwa mabadiliko madogo ambayo hayakwepeki kutokana na umri.


Yapo mabadiliko mengi, lakini zaidi tujirekebishe, tukumbuke kwamba baadhi ya vitu tulivyokuwa navyo huko nyuma ndivyo viliwavutia wepenzi wetu na kukubali kuwa nasi kwa hiyo tukiacha tunakuwa tunawakatili.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: