Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,Dk. Edward Hoseah.Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru) mkoani Dodoma, imesema itaanza uchunguzi wa awali kuhusu madai ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwa kuna wabunge wamehongwa Sh. milioni tatu kila mmoja ili wakwamishe bajeti yake.
Akizungumza jana na NIPASHE, Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Eunice, Mmari, alisema wataanza na uchunguzi wa awali kuhusu tuhuma hizo na sababu nyingine zitafuata baadaye.
“Tutafuatilia kwanza taarifa za awali tujue kama tuhuma hizo ni za kweli au la na kama kutakuwa na sababu ya kumuita Profesa Muhongo tutamuita,” alisema Mmari.
Hatua hiyo, imetokana na kuwapo na mvutano kati ya Waziri huyo na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono, ambao unadaiwa kusababishwa na ujumbe wa maandishi wa kutaka kukwamisha bajeti ya wizara hiyo kusambazwa kwa baadhi ya wabunge.
Ujumbe huo mfupi unamtuhumu Mkono kula njama za kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara hiyo kwa kuwapatia baadhi ya wabunge fedha hizo.
Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, alisema kuwa watamhoji Profesa Muhongo na kwamba alishamuagiza Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma kuchukua hatua hiyo kwa kuwa waziri huyo alitoa madai hayo bila kuyafikisha Takukuru. CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment