

Na Lilian Lucas, Morogoro.
Wigo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Nje ya Bunge, umezidi kupanuka baada ya Shura ya Maimamu na Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, kutangaza kujiunga nao, hatua ambayo baadhi ya viongozi wake, wametamba kuwa itasaidia kuiondoa CCM madarakani kwa urahisi katika uchaguzi mkuu ujao.
Kabla ya Shura hiyo kutangaza kujiunga na Ukawa juzi, umoja huo ulikuwa unaundwa na vyama vya upinzani vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo wabunge wake, walitoka nje ya Bunge la Katiba wiki moja kabla ya kusitishwa kwa shughuli zake mwezi uliopita.
Bunge hilo lilisitishwa April 18 mwaka huu ili kutoa nafasi ya wabunge wa Bunge la Muungano kushiriki katika Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
Msimamo wa Shura kutangaza kujiunga na Ukawa, ulitangazwa juzi na Katibu Mkuu wake, Sheikh Rajab Kitimba, alipokuwa akiwahutubia wananchi katika Uwanja wa Kiwanja cha Ndege,mjini Morogoro.
Shekh Kitimba alisema wao kama jumuiya, wameona ni vema kujiunga na Ukawa ili kupigania katiba inayotokana na maoni ya wananchi.
Alisema hatua hiyo imekuja baada ya kuona kuwa malengo ya jumuiya hiyo na ya vyama vinavyounda Ukawa, yanafanana kwa maana ya kuwahudumia wananchi na si kama inavyodhaniwa na baadhi watu.
“Jumuiya ya Kiislamu Tanzania lengo letu ni kuwahudumia wananchi, wanaosema sisi ni wachochezi na wavunjifu wa amani ni waongo,”alisema katibu huyo
Heche amshukia Kinana.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavita), John Heche, alimshukia Katibu wa CCM, Abdulrahaman Kinana kwa kile alichodai kuwa ni kuupotosha umma kuhusu Katiba Mpya.
“Kwa kauli zake, Kinana kama katibu mkuu wa chama kinachotawala, ingekuwa katika nchi nyingine angekuwa amevuliwa ama kufukuzwa nyadhifa zake,”alisema Heche
Alisema CCM inatumia nguvu kubwa na fedha nyingi kubeza maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu Katiba Mpya na kupandikiza maneno ya chuki huku iking’ang’ania muundo wa Serikali mbili unaopingana na rasimu ya katiba iliyoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Pia mwenyekiti huyo wa Bavicha aliwataka wananchi kutazama Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma, ili washuhudie namna wabunge wa upinzani wanavyotetea maslahi ya wananchi.
“Wabunge wetu hatutakuwa nao kwa muda huu labda pale itakapolazimika, kwa sasa wamehamia katika Bunge la Bajeti ili kutetea maslahi yenu na sisi wapiganaji tunaendelea na harakati za kudai Serikali tatu kulingana na maoni ya wananchi,”alisema.

0 comments:
Post a Comment