WAJUMBE WA KAMATI YA BUNGE YA BAJETI KUKWAMISHA BAJETI KUU YA SERIKA YA SH19 TRILIONI.
Kifuko kilichobeba Bajeti ya Serikali.
Dodoma.
Wakati Serikali ikiwa taabani kifedha, wabunge wengi, wakiwamo wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti wanapanga kukwamisha Bajeti Kuu ya Serikali, inayofikia zaidi ya Sh19 trilioni.
Habari kutoka ndani ya vikao vya Kamati ya Bunge ya Bajeti, zinadai kuwa iwapo Serikali haitapunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya pato la taifa (GDP), wabunge hao watakwamisha bajeti hiyo.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alilithibitishia gazeti hili jana kuwa yeye ni miongoni mwa wabunge waliopanga kukwamisha bajeti hiyo na yuko tayari kufukuzwa ubunge kwa hilo.
Lugola alisema kuwa pamoja na kuwepo kanuni inayowakataza wabunge wa CCM kukwamisha bajeti na anayefanya hivyo hufukuzwa, yuko tayari afukuzwe ili ayaponye maisha ya Watanzania milioni 45.
“Kila mwaka tunapiga kelele misamaha ya kodi, wanatumia mwanya huo vibaya na matokeo yake bajeti za Serikali mwaka hadi mwaka hazipati fedha kutoka Hazina,” alisema Lugola na kuongeza:
“Kama hakuna fedha, halafu tunatoa misamaha kiholela, basi ni afadhali bajeti ya mwaka huu tuzibe hiyo mianya, futa kabisa hiyo misamaha isiyo na tija.”
Lugola alisisitiza: “Hatuwezi kuendesha nchi kwa staili hiyo, lazima tufike mahali mambo ya kuwekeana kanuni kuwa tukikwamisha bajeti Bunge litavunjwa, acha livunjwe ili kuliponya taifa.”
Lugola alisema kama Serikali haitakuja na mwarobaini wa misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi, matumizi makubwa ya Serikali na kupambana na ufisadi na wizi, bungeni hapatatosha.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), jana alisema kuwa angetamani kama Bajeti ya Serikali isipite mwaka huu ili wabunge watimize wajibu wao wa kikatiba wa kuisimamia Serikali.
“Nenda kwenye Ripoti za CAG, madudu ni yaleyale mwaka hadi mwaka, misamaha ya kodi ndiyo usiseme, matumizi ya anasa ndiyo balaa. Nchi inakwenda wapi?” alihoji Machali na kuongeza:
“Kama kweli wabunge wanaitakia mema nchi hii, tuungane, kama Serikali haiji na majibu ya madudu yote haya tusipitishe bajeti hii. Tuweke historia ambayo vizazi vijavyo vitatukumbuka.”
Wakati wabunge wengi wakipanga kukwamisha bajeti iwapo misamaha hiyo haitapunguzwa hadi asilimia 1 ya GDP, hadi kufikia Juni 30, 2013 misamaha hiyo ilikuwa Sh1.52 trilioni.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment