Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuzindua rasmi chapisho la tatu la taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi pamoja na tovuti katika kupata taarifa za Sensa na Makazi katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, mwakilishi wa UNFPA, Mariam Khan, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum na Kamishna wa Sensa na Makazi, Amina Mrisho. (Picha na Freddy Maro).
MAENDELEO ya Watanzania na kuongezeka kwa ubora wa maisha yao sasa ni dhahiri baada ya chapisho la tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi, linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, kuonesha hatua walizopiga katika maisha yao.
Ubora huo wa maisha ya Watanzania, umedhihirika katika chapisho hilo lililozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete jana Dar es Salaam, baada ya kukamilika uchambuzi wa taarifa zilizokusanywa katika Sensa hiyo.
Takwimu hizo zilizolinganisha hali ya ubora wa maisha ya Mtanzania kutoka katika taarifa za Sensa hiyo na iliyofanyika mwaka 2002 na miaka mingine ya nyuma, imedhihirisha Tanzania ya sasa miaka 53 baada ya Uhuru si ya wakati wa Uhuru.
“Kwa utaratibu huu wa kufanya Sensa kila baada ya miaka 10, ina maana kuwa sensa inayofuata itafanyika mwaka 2022, ikiwa ni miaka michache kabla ya kufikia Dira ya Taifa. “Hivyo, matokeo haya ni msingi wa kupima mwelekeo wetu kiuchumi na kijamii kufikia lengo letu la kuwa uchumi wa kati ifikapo 2020 kwa upande wa Zanzibar na 2025 nchi nzima,” alisema Rais Kikwete.
Umri wa kuishi
Kwa sasa kwa mujibu wa chapisho hilo lililofanyiwa uchambuzi na wataalamu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), umri wa kuishi wa Mtanzania ni miaka 61, ongezeko la miaka 10 kutoka 2002 ambapo umri wa kuishi wa Mtanzania ulikuwa miaka 51.
Wanawake kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndio wanaoongoza kwa kuishi umri mrefu zaidi wa miaka 63, huku wanaume wakiishi miaka 60.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, mwaka 1988 umri wa kuishi wa Mtanzania ulikuwa miaka 50 wakati wakati wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, umri wa kuishi ulikuwa miaka 37.5.
Kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2013 na takwimu NBS, Tanzania sasa ndio taifa ambalo wananchi wake wana uhakika wa kuishi umri mrefu kuliko nchi zingine katika Afrika Mashariki.
Inafuatiwa na Kenya ambayo wananchi wake wana uhakika wa kuishi miaka 57.86 ikifuatiwa na Uganda (52.72), Burundi (52.09) na mwisho Rwanda (50.52).
“Kuongezeka kwa wastani wa miaka ya kuishi, kunaweza kuwa kumechangiwa na kukua kwa uchumi na kupungua kwa umasikini wa kipato,” imeeleza ripoti hiyo.
Akizungumzia hilo, Rais Kikwete alisema takwimu hizo maana yake ni kuwa, huduma za afya zimeimarika, watu sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
“Hata hivyo, bado hatujafikia viwango vya wenzetu wa Asia na Ulaya ambao wastani wao kuishi ni miaka 70 na kuendelea,” alisema Rais Kikwete.
Asia/Ulaya.
Taifa linaloongoza kwa kuwa na watu wanaoishi umri mrefu duniani kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya 2013, ni Monaco, ambayo umri wa kuishi wa wananchi wake ni miaka 87.2.
Kama kawaida wanawake katika nchi hiyo, wanaishi miaka 89 na wanaume umri wao ni miaka 85.3. Mataifa kumi yanayoongoza kwa wananchi wake kuishi umri mrefu duniani unaoneshwa katika mabano ni Monaco (87.2) ambayo ni ya kwanza, ikifuatiwa na Japan (84.6) na Andorra (84.2) ambayo ni moja ya mataifa madogo yaliyopo katika Bara la Ulaya.
Taifa la nne kwa wananchi wake kuishi umri mrefu duniani ni Singapore (84), likifuatiwa na Hong Kong (83.8), San Marino (83.5), ambayo ni visiwa vilivyopo jirani na Italy vikifuatiwa na Ice Land (83.3), Italia (83.1), Sweden (83) na Australia ambayo nayo pia umri wa kuishi ni miaka 83.
Taifa ambalo wananchi wake wanaishi kwa umri mfupi zaidi duniani kwa mujibu wa taarifa hizo za WHO ni Angola, ambayo umri wa kuishi ni miaka 38.
Mataifa mengine yanayofuatia kwa wananchi wake kuishi umri mfupi zaidi duniani ni Zambia (38.63), Lesotho (40.38), Msumbiji (41.18), Sierra Leone (41.24), Liberia (41.84), Djibout (43. 37), Malawi (43.82), Jamhuri ya Afrika ya Kati (44.47) na Zimbabwe (45.77).
Makazi
Mbali na kuongezeka kwa umri wa Watanzania kuishi, makazi wanayoishi sasa yameboreka zaidi kwa maana ya vifaa vilivyotumika kujenga nyumba hizo, ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya NBS, Sensa ya 2012 imebaini kuwa asilimia 62 ya nyumba za Watanzania, zimeezekwa kwa kutumia mabati, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2002, ambapo ni asilimia 46 tu ya nyumba za Watanzania, zilizokuwa zimeezekwa kwa mabati.
Aidha, nyumba ambazo sakafu zake si za udongo, kwa maana ya kuboreshwa kwa saruji, vigae, mbao au tarazo, zimeongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2002, mpaka asilimia 39 mwaka 2012.
“Ongezeko la kaya zilizotumia vifaa imara kujenga nyumba za kuishi, inaonekana kote Tanzania Bara na Zanzibar. Maboresho ya vifaa vinavyotumika kujenga yamechangiwa na ukuaji wa uchumi na kupungua kwa umasikini wa kipato,” imeeleza taarifa hiyo.
Vifo vyapungua
Taarifa hiyo imebainisha kuwa vifo vya watoto wachanga nchini Tanzania, vimepungua kutoka watoto 115 kwa kila watoto hai 1,000 waliozaliwa mwaka 1988, hadi vifo vya watoto 45 kwa kila watoto hai 1,000 waliozaliwa mwaka 2012.
“Kwa mwaka 2013 tumefikia 21. Vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua kutoka 231 mwaka 1988 hadi 68 mwaka 2012 na 2013 tumefikia vifo 54 kwa 1,000,” aliongeza Rais Kikwete.
Alisema hali hiyo imetokana na ongezeko la chanjo za magonjwa yaliyokuwa yakiua watoto wengi.
“Kwa takwimu za mwaka jana vifo sasa ni 21, tumebakiwa na vifo viwili tu ili tufikie Malengo ya Millennia ya vifo 19, naamini ifikapo mwakani tutafikia lengo hilo. Kwenye vifo vya watoto chini ya miaka mitano tumefikia 54 na kufikia lengo la Millennia tangu mwaka jana.”
Pia taarifa hiyo imebainisha kuwa vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi, navyo vimepungua kutoka vifo vya wanawake 432 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai, kutoka vifo vya wanawake 578 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai kwa mwaka 2004.
Rais Kikwete alisema hiyo ni hatua kubwa kuelekea lengo la Milenia ya mwaka 2015, la kupunguza vifo vya wanawake kufikia 193 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa hai.
Rais Kikwete lisema bado mafanikio katika kupunguza vifo vya wajawazito si mazuri kwani hadi kufika mwakani vifo hivyo vilipaswa kupungua hadi kufikia 193.
“ Takwimu hizi zinatuonesha kuwa tunatakiwa kusogeza huduma za afya kwa watu, tuongeze watoa huduma ili asilimia 80 ya akinamama wajifungulie kwenye mikono ya wataalamu wa afya na tofauti na sasa ambapo asilimia 49 ya wajawazito wanajifungua katika mikono ya wakunga wa jadi. Lengo ni kuhakikisha hakuna kifo kinatokea,” alisema.
Umiliki simu
Katika hotuba yake, Rais Kikwete pia alielezea ongezeko la wamiliki wa simu za kiganjani, waliofikia asilimia 64 ya Watanzania mwaka 2012, ikilinganishwa na asilimia 10 mwaka 2005.
“Kuongezeka kwa simu ni kiashiria cha kuongezeka kwa biashara, idadi ya watu wanaotumia huduma za kifedha kwa njia ya simu na urahisi wa mawasiliano ambao unawezesha usambazaji wa taarifa za kijamii na kibiashara katika maeneo mengi hivi sasa.
Pato
Alisema Dira ya Taifa ya 2025 inataka Tanzania kuwa na uchumi wa kati ambapo wananchi wa kawaida, watakuwa na pato la dola za Marekani 3,000 kwa mwaka. Kwa sasa kipato kimepanda kufikia dola 717 kutoka dola 321 mwaka 2002.
Kikwete alisema pamoja na takwimu kuonesha umasikini umepungua hadi kufikia asilimia 28.2, idadi hiyo ni ndogo lakini lengo la Serikali ni kuondoa kabisa hali hiyo.
“Tunataka tufike mahali kusiwe na masikini kabisa, na hili linawezekana kwani umasikini si laana.”
Mwito Kutokana na takwimu hiyo, Rais Kikwete ametaka mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine, kutumia taarifa zilizotolewa na kuacha tabia ya kupotosha taarifa hizo kwa maslahi yao binafsi.
Alisema kukamilika kwa kazi ya ukusanyaji wa takwimu, kunaelekeza wizara, idara, na taasisi zingine za Serikali, Serikali Kuu na Mitaa kuzitumia katika kupanga mikakati ya maendeleo kwa wananchi.
“Natoa mwito kwa wananchi na wadau wa maendeleo hususani asasi za kiraia, kusoma taarifa na kuzitumia vizuri. Kumekuwapo upotoshwaji mkubwa, wapo wenye kubeza mafanikio yaliyopatikana, wengine hata takwimu za watu wanaojua kusoma na kuandika kuongezeka wao inawaudhi, hata habari za kukua kwa pato la Taifa zinawakasirisha, wao wanataka habari mbaya.
“Kuna watu kazi yao ni kupeleka taarifa mbaya tu ili kupata fedha, kutumia misingi hiyo kujipatia fedha za maendeleo si vizuri, sasa taarifa zimetolewa mtu asiende kutunga zake, taarifa hizi zimetokana na watu kuulizwa,” alisema.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment