BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAMATI YA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA AWAUNDIA ZENGWE LA NGUVU VIONGOZI WA UKAWA.

 
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta akisisitiza jambo jana, baada ya mkutano wa Kamati ya Maridhiano uliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Rafael Rubava.

Dar es Salaam.
 

Kikao cha mashauriano kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kimeamua kuwa Bunge hilo liendelee kama kawaida Agosti 5, mwaka huu licha ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vyake.


Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kwamba mkutano wa Bunge Maalumu utaendelea kama kawaida kwa kuangalia akidi na iwapo haitatimia wakati wa upigaji kura, wananchi waelezwe kwamba Ukawa ndiyo wamekwamisha na hivyo hawana nia na Katiba Mpya.


“Kutokana na hali hiyo tumekubaliana kwamba hiyo Agosti 5, tutaangalia idadi ya wajumbe watakaoripoti bungeni ili kuona kama akidi itatimia kisha utatolewa ufafanuzi.”


Taarifa hizo zilieleza kuwa kama akidi haitatimia moja ya mambo yatakayofanywa ni pamoja na Watanzania kuelezwa jinsi kususa kwa Ukawa kunavyokwamisha mchakato huo.


Sitta aliitisha kikao hicho cha wajumbe 30 wakiwamo viongozi wa Ukawa jana, akisema kilikuwa na lengo la kutathmini mwenendo wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuondokana na mgawanyiko uliopo.

Licha ya mwaliko huo, hakuna mjumbe yeyote wa Ukawa aliyehudhuria, lakini kwa upande wa vyama vya upinzani wajumbe waliohudhuria ni Peter Mziray wa APPT-Maendeleo na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed ambaye alisimamishwa uanachama wa chama hicho.


“Uamuzi wao (Ukawa) unaweza kukwamisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2015. Ila kifupi vikao vitaendelea na lolote linaweza kutokea. Uamuzi utategemea na akidi itakayokuwapo,” kilisema chanzo chetu ndani ya mkutano huo.


Hata hivyo, mjumbe mwingine wa kikao hicho cha jana alisema: “Unajua katika kikao imeonekana wazi kuwa akidi itatimia kwa kuwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar itatimia tu.”


Habari kutoka katika kikao hicho cha siku mbili kilichoanza jana saa nne asubuhi na kumalizika saa 8:14 mchana, zilieleza kuwa mvutano mkali uliibuka kuhusu akidi ya wajumbe kwa ajili ya kupitisha uamuzi katika Bunge hilo.


Kifungu cha 26 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinaeleza: “Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Zanzibar.”


Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Julai 8, mwaka huu, Sitta alisema iwapo Ukawa watarudi bungeni lakini wakasusa tena kadri mjadala utakavyoendelea, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.


Hata hivyo, wazo hilo tayari limepingwa na wanasheria mbalimbali wakisema suala hilo haliwezekani kwa kuwa Bunge la Muungano lenye dhamana ya kutunga sheria halitakuwa na kikao hadi Novemba na kwamba hitaji la mambo ya Muungano kuamuliwa kwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka kila upande si tu la kisheria, bali pia ni la kikatiba.


Vilevile, mwenyekiti huyo alidokeza kuwa mkutano wa jana ungekuwa kipimo cha kuwaonyesha Watanzania iwapo Ukawa wako tayari kwa Katiba Mpya au la.


Taarifa zaidi zilifafanua kuwa hoja ya Ukawa ya kutaka ijadiliwe Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nayo iliibuliwa katika kikao hicho jana, lakini ilipingwa kwa maelezo kuwa Rasimu hiyo inaweza kubadilishwa na si kuboreshwa pekee.


Awali, jana Sitta alisema kuwa atatoa ufafanuzi wa kilichojadiliwa katika kikao hicho saa 10 jioni, lakini baadaye alituma ujumbe kwamba atafanya hivyo leo saa tatu asubuhi na baadaye muda huo ukaongezwa kuwa itakuwa saa tano asubuhi.


Alipoulizwa kama akidi isipotimia nini kitafanyika, Sitta alisita kujibu swali hilo na kueleza kuwa atakapotoa ufafanuzi kwa wanahabari atafafanua jambo hilo.


Kwa nyakati tofauti, Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wamenukuliwa wakisema kuwa iwapo Katiba Mpya haitapatikana itaendelea kutumika ya sasa ingawa italazimika kufanyiwa marekebisho katika maeneo fulani, ambayo hawakuyataja baada ya maridhiano na pande zote.MWANANCHI

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: