BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KIKWETE ASIKWEPE, AIOKOE KATIBA MPYA.

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2014/01/Jakaya-Kikwete-na.jpg
RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE.

Wakati hofu kuhusu mwendelezo wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba ikizidi kupanda, watu na asasi za kijamii, wanatoa rai wakitaka kurejea kwa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Ukawa iliyo upande wa ‘walio wachache’ ndani ya Bunge hilo, walisusia kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni ‘uchakachuaji’ wa rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabaliko ya Katiba baada ya kukusanya maoni ya wananchi.

Eneo lililo msingi wa Ukawa kususia Bunge hilo ni sura inayopendekeza kuwapo kwa muundo wa serikali tatu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pendekezo linalopingwa na watawala wakitoa sababu kadha wa kadha, ikiwamo kufa kwa Muungano ulianza Aprili 26, 1964.

Hadi vikao vya Bunge hilo vilipoahirishwa Aprili 25, mwaka huu, sura zilizokuwa zinajadiliwa pasipo kufikiwa muafaka ni ile ya kwanza inayohusu jina, mipaka, alama, lugha na tunu za Taifa.
Pia, sura ya sita, inahusu muundo wa Muungano, vyombo vya utendaji na mamlaka ya serikali, nchi washirika na uhusiano wa nchi washirika.

Wapo wanaoamini kuwa Ukawa wanapaswa kurejea bungeni pasipo sharti lolote na wapo wanaoamini kwamba, rasimu halisi ya Katiba Mpya lazima ijadiliwe pasipo kuongeza matakwa ya watawala, hivyo Ukawa kupata fursa ya kushiriki.

Kwa upande wa mjumbe wa Bunge hilo, Kajubi Mukajanja, anasema mchakato wa Katiba Mpya bado unakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji dhamira na ushiriki wa Rais Jakaya Kikwete, kuchukua hatua.

Mukajanja, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT), anasema tangu alipolihutubia Bunge hilo, Rais Kikwete alitoa kauli ambazo kwa mujibu wa kanuni za uongozi, zilikuwa kama maagizo kwa wajumbe wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Anasema, Rais Kikwete, alipolihutubia Bunge Maalum Katiba, alipaswa kutoegemea upande wowote ili wajumbe wawe huru kuyasoma na kuyajadili maoni ya wananchi, lakini haikuwa hivyo.

“Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama kilichopo madarakani, anapohutubia na kuelezea msimamo wake, kwa maana na tafsiri rahisi ni kama ametoa maagizo na msimamo usiostahili kupingwa na walio chini yake,” anasema.

Ndio maana, Kajubi anasema kwa namna iwayo yote, hakuna mamlaka inayoweza kufanikisha nia njema ya kuuokoa mchakato huo, isipokuwa kupitia kwa Rais Kikwete mwenyewe.

ASILI YA TATIZO
Kajubi, anasema hivi sasa jamii inaweza kujielekeza zaidi katika hoja zinazokinzana kuhusu muundo wa Muungano, lakini bado kuna sura ambazo mjadala wake unaweza kupingwa na wabunge wa Bunge la Muungano.

Kwa mujibu wa Kajubi, hatua hiyo inatokana na mapendekezo yasiyokuwa rafiki kwa wanasiasa, ikiwama kuwapo ukomo wa kuchaguliwa na wabunge kutokuwa mawaziri.

“Sasa hivi tunalumbana kuhusu muundo wa Muungano, lakini huko mbeleni kunaweza kuibuka mkwamo mkubwa ambao wananchi wanaweza kuwaona wapinzani na watawala wanaungana kupinga maoni ya raia,” anasema.

Kajubi, anasema hatai hiyo na ile inayohusu muundo wa Muungano, ‘viliasisiwa’ katika hatua za awali za uteuzi wa wajumbe kwa kuwahusisha wanasiasa.

Kajubi, anasema hata msimamo wa Rais Kikwete na ule uliofuatia kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, kutangaza kuwapo serikali tatu, vimepanua wigo wa mzozo unaohatarisha kupatikana kwa Katiba Mpya.

VIKWAZO VYA WANASIASA

Akasema, wabunge walio wengi hawataunga mkono pendekezo la kuwapo ukomo wa kuchaguliwa kwao, huku walio katika utawala wakipinga wabunge kutokuwa mawaziri.

“Sioni urahisi kwa mbunge kama Ridhiwani Kikwete ambaye ameingia bungeni hivi karibuni, bado ni kijana, kisha akaunga mkono ukomo wa kuchaguliwa, ama mbunge kupitia CCM akataka mawaziri wasitokane na wabunge,” anasema.

MAONI YA TUME YAHESHIMIWE
Kajubi anasema ipo haja kwa kila raia pasipo kujali wadhifa kwa jamii, kuheshimu maoni ya wananchi yaliyowasilishwa kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.


Anasema hata aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Amos Wako, aliwaonya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na Tanzania kwa jumla, kutokuyapuuzia maoni ya wananchi, na badala yake kuongeza vifungu vyenye maslahi kwa wanasiasa hususani watawala.

Kajubi, anasema kwa hali hiyo hakuna sababu kwa viongozi wa vyama vya siasa kuupotosha umma kwa kutangaza misimamo ya vyama vyao, wakati hakuna mwanachama aliyeshirikishwa kupitisha misimamo hiyo.

SI RASIMU YA JAJI WARIOBA
Kajubi anaweka wazi kwamba rasimu inayopaswa kujadiliwa katika Bunge Maalum la Katiba, si ya Jaji Warioba kama inavyoelewekwa kwa wengi, bali ya Rais Kikwete.

Anajenga msingi katika hoja hiyo kuwa, baada ya uteuzi wake, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya kazi na kuripoti kwa Rais Kikwete, hata ilipomkabidhi rasimu husika kwa nyakati mbili tofauti.

“Mwanzo alikabidhiwa rasimu, akaiona inafaa, ikapelekwa kwenye mabaraza, huko ndipo hujuma zilipoanza kufanyika,” anasema.

Pia, Kajubi anasema ni Rais Kikwete, aliyetoa hadidu za rejea kwa tume hiyo, na baadaye kukabidhiwa rasimu ya mwisho aliyoisaini kabla ya kufikishwa bungeni kujadiliwa.

“Sasa leo hii nikimsikia Rais Kikwete anatamka lililo kinyume cha yaliyomo kwenye rasimu aliyotuletea, nitashindwa kumuelewa..kwa maana atakuwa anajikana mwenyewe,” anasema.

Kwa mujibu wa Kajubi, hujuma dhidi ya rasimu hiyo zilihusisha vyama vya siasa ‘kuwapndikiza’ watu waliotumwa kuwasilisha maoni yanayofafa, kiasi cha kuifanya tume ionye mara kadhaa pasipo mafanikio.
Makala haya yameandikwa na Mashaka Mgeta na Richard Makore.CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: