MATUKIO YA KISIASA.
Moshi ukifuka kutoka kinu cha umeme cha Gaza kilichoshambuliwa na Israel usiku wa kuamkia tarehe 29 Julai 2014.
Israel imeendelea na mashambulizi yake dhidi ya Gaza, sasa ikilenga miundombinu, ambapo hivi leo kinu pekee ya kuzalishia umeme kimeshambuliwa sambamba na nyumba ya kiongozi wa Hamas, Ismael Haniya.
Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Nishati ya Palestina, Fathi al-Sheikh Khalil, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kinu hicho cha umeme kimesita kufanya kazi kutokana na mashambulizi ya Israel usiku wa jana, ambayo yaliliharibu jenereta na matangi ya mafuta ambayo yaliripuka kabisa.
Mwandishi wa AFP ameshuhudia moto mkubwa karibu na kinu hicho asubuhi ya leo, akisema kwamba idara ya zimamoto hadi wakati huo ilikuwa haijaweza kulifikia eneo hilo.
Mashambulizi dhidi ya kinu hicho pekee yanaongezea madhila tu juu ya jaala ya Gaza ambayo kwa siku ya 22 sasa imekuwa ikitwangwa makombora ya Israel mfululizo. Kuharibiwa kwa kinu hicho kunamaanisha pia kwamba huduma ya umeme ambayo tangu hapo ilikuwa si ya uhakika, inazidi kuwa mbaya, kwani Gaza ilikuwa ikitumia kinu hicho pamoja na umeme inaonunua kutoka Israel, ambao nao sasa haupatikani kutokana na njia za umeme kuharibiwa vibaya na mashambulizi ya Israel.
Khalil amesema katika kila njia kumi za umeme ndani ya Ukanda wa Gaza, njia tano zimeharibiwa. Tayari hospitali, ambazo hata nazo hazisalimiki na makombora ya Israel, zimeanza kulalamikia uwezo mdogo wa nishati ya kuhifadhia maiti na kutibia majeruhi.
Nyumba ya Haniyeh yalengwa
Sehemu ya nyumba ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, iliyoshambuliwa na Israel usiku wa kuamkia tarehe 29 Julai 2014.
Usiku wa kuamkia leo pia umeshuhudia mashambulizi mengine dhidi ya makaazi ya raia, ambapo kombora lililorushwa kutoka ndege ya Israel liliangukia nyumba ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, ingawa kiongozi huyo na familia yake walinusurika kuuawa.
"Jana usiku wakati tumelala, milango ya saa saba unusu, maroketi yakaanza kuanguka, yalikuwa mashambulizi matatu tafauti. Tukawachukuwa watoto wetu wakiwa usingizini na kukimbilia upande wa kaskazini, lakini tunamshukuru Mungu hakuna madhara, hakuna majeruhi wala mashahidi, yote kwa rehema za Mungu kuwanusuru wapigania jihadi na Ismail Haniyeh," amesema jirani wa Ismael Haniye, Bi Fatima Abu Riyale.
Hamas pia inasema kuwa kituo chake televisheni na redio, vyote vinavyoitwa Al-Aqsa, pia vilishambuliwa, ingawa televisheni iliendelea na matangazo hata baada ya mashambulizi hao, huku redio ikizimika kabisa. Majengo mengine yaliyoharibiwa kabisa na mashambulizi ya hivi karibu ni kabisa ni Msikiti al-Amin na wizara ya fedha.
Kufikia leo, tayari Wapalestina 1,110 wameshauawa na zaidi ya 6, 500 kujeruhiwa, ambapo Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya asilimia 75 kati yao ni raia. Israel imethibitisha kupoteza wanajeshi wake 53 na raia watatu, ingawa Hamas wanasema idadi ya wanajeshi wa Israel waliouawa ni wengi zaidi. Maelfu ya wakaazi wa Gaza wamegeuzwa kuwa wakimbizi wa ndani, ingawa hawana mahala pa kukimbilia palipo hasa salama.
Shinikizo la kimataifa linaongezeka kwa ajili ya kupatikana usitishwaji mapigano, ingawa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameapa kuendelea na mashambulizi hadi waiangamize kabisa Hamas.DW
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment