BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIKUTOSWA UKUU WA MKOA ETI KWA SABABU YA KUMSAPOTI SUMAYE KATIKA MBIO ZA URAIS 2010 BADALA YA KIKWETE.

 
Mkuu Mkuu wa Mkoa mstaafu wa Morogoro, Stephen Joshua Mashishanga akizungumza na mwandishi wa Mwananchi, Lilian Lucas kwenye makazi ya mkongwe huyo wa siasa maeneo ya Forest kata ya Boma mjini Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Na Lilian Lucas, Morogoro.
“Mimi sikuachwa na Kikwete (Rais Jakaya Kikwete) kwa sababu hiyo, kwa wakati ule Sumaye (Frederick Sumaye) alikuwa waziri wangu mkuu, hivyo ilikuwa lazima nimuandalie mazingira mazuri, sasa watu ndiyo wakatafsiri vinginevyo, kama ningeonyesha hadharani kumpinga isingeleta picha nzuri.”
Hiyo ni kauli ya Stephen Mashishanga aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa.


Ambapo awamu ya nne hakuwamo katika nafasi yeyote ya uongozi serikalini na kubaki kuwa mstaafu aliyeamua kuweka makazi yake katika kituo chake cha mwisho cha utumishi wa umma mkoani Morogoro.

Mashishanga ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80, wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, wakati huo akiwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, ilidaiwa alikuwa kambi ya Waziri Mkuu Frederick Sumaye, aliyekuwa ndani ya mchakato huo.

Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi, nyumbani kwake maeneo ya Forest katika Kata ya Boma manispaa ya Morogoro, kwa mara ya kwanza Mashishanga anasema; “Si kweli hata kidogo, baada ya Kikwete kushinda urais na kufanya uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, watu wengi walijua nimeachwa kwa sababu hiyo,”anasema.

Mkongwe huyo wa siasa na mkulima mkoani Morogoro, anasema wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM, hakuwa upande wowote wala wa Sumaye. “Mkoani Morogoro wagombea walipita wote na mimi ndiyo nilikuwa mwenyeji wao, kutokana na utaratibu wa CCM ilikuwa ni lazima ampoke kila anayepita,” aliongeza.

Anasema kwa kipindi kile watu walikuwa wakifuatilia kwa umakini, na yeye (Mashishanga) walimuweka kambi mbalimbali za wasaka urais, lakini kiukweli hawakuwa wakifahamu anayemuunga mkono.

“Kauli ya kuwa niliukosa ukuu wa mkoa kwa kuwa nilikuwa kambi ya Sumaye, si kweli na ni upuuzi mtupu.”

Anasema hakuachwa na Kikwete kwa sababu hiyo ya kuwa kambi fulani, watu wamekuwa wakitafuta maneno ya kuzungumza kwa wakati hule, watu waliiona ile baada ya uteuzi wa wakuu wa mikoa. “Wengi walijua ningeteuliwa kutokana na utendaji wangu, lakini umri ulikuwa umewadia wa kupumzika,” anasema na kuongeza;

“Mimi sikuachwa na Kikwete kwa sababu hiyo, kwa wakati ule Sumaye alikuwa waziri wangu mkuu, hivyo ilikuwa lazima nimuandalie mazingira mazuri sasa watu ndiyo wakatafsiri vinginevyo, kama ningeonyesha hadharani kumpinga isingeleta picha nzuri,” alisema.

Anasema uteuzi wa Rais Kikwete ulizingatia umri, ambapo aibainisha kuwa kwa mwaka 2006 alikuwa na umri wa miaka 72, hivyo alishafikisha umri wa kustaafu wa miaka 60 na alipitiliza miaka 12 zaidi, hivyo ilikuwa ni vyema kutoteuliwa.

Mashishanga anasema sifa za kuteuliwa ukuu wa mkoa alikuwa nazo na alipopeleleza aligundua kuwa ni umri ndiyo ulichangia, na kwa wakati ule hakuna mkuu wa mkoa aliyeteuliwa akiwa na umri mkubwa.


Anasema watu wengi walitegemea kuwa yeye angeteuliwa kuwa RC, na hiyo ni kutokana na utendaji wake mzuri katika Serikali aliokuwa ameufanya kwa miaka yote, pia alimshukuru Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa kumteua kuwa mkuu wa mkoa kwa mara ya kwanza, na kwamba hata wakati huo umri ulikuwa umeenda.

Mashishanga anasema katika uchaguzi ujao atamuunga mkono atakayeteuliwa na chama chake, na kwamba kwa sasa hayuko wazi kumuunga mkono yeyote, kwani chama bado hakijateua mgombea pamoja na kuwapo kwa wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.

Kama akiteuliwa kuwa RC
“Siku hizi suala la uwajibikaji limepungua sana, kama nitateuliwa tena kwenye ukuu wa mkoa (ingawa alisema haitaji), ningesimamia suala ya uwajibikaji kutokana na kupungua kwa kasi kubwa, watu na viongozi wengi nchini wamekuwa wavivu, wanakosa maadili katika kazi,” anasema.

Mashishanga alitoa mfano kwamba unakuta diwani, mbunge, mkuu wa wilaya ama mkuu wa mkoa na wakurugenzi, halmashauri ya kata na vijiji wamekuwa si wasimamizi kikamilifu, wamekuwa watu wa kutoa maagizo bila kufuatilia.

Anasema watu wamekuwa na mmomonyoko wa maadili, kikuthiri kwa rushwa na ufisadi, viongozi wamekuwa na maneno mengi bila kuwajibishana.

“Hivi inakuwaje watoto wanakaa chini wakati huu na viongozi wapo, DC (mkuu wa wilaya), RC (mkuu wa mkoa) wanafanya nini, mfano mdogo wakati ule tukiwa viongozi ukienda mahali ukikuta watoto wanakaa chini unakaa hapo mpaka kuhakikisha madawati yanatengenezwa, angalia miti tuliojaaliwa na Mungu ipo, watu wamekuwa wakipiga kelele tu,” anabainisha.

Anasema watu wamekuwa wakipiga kelele na kutosimamia masuala ya maendeleo,halafu kauna ufuatiliaji wa karibu ndio maana kumekuwa na kudororo kwa utendaji kazi mahali pa kazi.

Maisha bora kwa kila Mtanzania imetekelezeka?
Mashishanga anasema kaulimbiu ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ imefanya vizuri, ingawa inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Anasema serikali imejitahidi kutimiza baadhi ya ahadi zake na kwamba inaendelea kufanya hivyo, na alisema changamoto tatu hazijaweza kutekelezeka kikamilifu.

Alitaja changamoto hizo kuwa ni kutotekelezeka kwa bajeti pamoja na kwamba imekuwa ikipitishwa, lakini utekelezaji wake haufanyiki, fedha zinazotengwa zimekuwa hazifiki kwa wakati unaohitajika na kwamba hii inatokana na mawaziri wengi kutofuatilia ipasavyo, na jambo la tatu ni usimamizi mbovu.


Mashishanga anasema Wizara ya Fedha ihakikishe inapeleka fedha zilizopitishwa katika bajeti kwa wakati, ili malengo na usimamizi wa miradi uweze kuwepo.

Mtazamo wake ndani ya CCM
Mkongwe huyo katika siasa alikitaka chama chake kurudia kusoma mwongozo wa mwaka 1980, uliokuwa ukizungumzia nini chama kinatakiwa kufanya pamoja na serikali ifanye nini kwa wananchi kulinganaa na ilani yake, chama lazima kiisimamie serikali.

Anasema kuwa kwa sasa mwongozo huo hautumiki vizuri, na serikali imekuwa ikifanya madudu katika vijiji na tarafa na chama kipo, lakini hakisimamii ipasavyo na hata hakiwawajibishi wanachama wake.

Mashishanga athari za kutoufuata mwongozo ni majengo kujengwa chini ya kiwango na chama hakisemi chochote, wakati kipo kila sehemu na watendaji wanakula rushwa, hivyo kihakikishe kinarudi na kufuata mwongozo.

Alimpongeza Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kwa namna anavyofanya kwa sasa, kwa kuwaumbua mawaziri mizigo ambao hawawajibiki, ambaye ameanza kurudisha mwongozo wa mwaka 1980.

Mashishanga anasema Kinana amekuwa akifokea viongozi ambao hawasimamii ipasavyo sera na ilani ya chama, ambapo amemuomba asikate tamaa na aendelee kupigania, kwani kila alipokwenda amefokea serikali na viongozi wake pale kinapofanya vibaya.

Anasema chama kisiwe na uwoga kwa serikali katika suala la kufanya kazi, chama kikisimama imara uwajibikaji, maadili, nidhamu ya kazi, ubadhilifu na kuondoa umaskini kwa kufanya hivyo heshima ya itarejea.

Mashishanga anatoa mfano wa wakati wa utawala wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, kwamba wakati huo kiongozi alipokuwa akifanya ufisadi na kutowajibika, hatua za haraka zilikuwa zikichukuliwa na wale wakorofi walikuwa wakiondolewa tofauti na sasa.

Anasema anashangazwa na baadhi ya mawaziri wanaoropoka ovyo bila aibu, alitoa mfano wa waziri mmoja (bila kumtaja jina), ambaye alitoa kauli bungeni akisema haogopi kuzomewa kwa madai amezoea.

“Nilishangazwa na waziri mmoja alituhumiwa na kusema siondoki na kujibu ovyo kabisa kuwa amezoea kuzomewa, hivi kama waziri anasimama na kusema amezoea kuzomewa anamwakilishaje rais katika sehemu nyeti kama ile na chama hakijasema lolote kimekuwa kimya,” anahoji kwa masikitiko.

Mashishanga anasema Bunge la sasa halina nidhamu kutokana na baadhi ya mawaziri kuropoka, tena bila kufikiria nyadhifa walizonazo.


Mbio za urais
Anasema kwa mtazamo wake, urais si jambo la kukurupuka inatakiwa kujiandaa na kuona kama unakubalika ndani ya chama chako na wananchi.

Mashishanga anasema kuwa mtu anayefaa kuwa kiongozi wa nchi, lazima awe na alama ya vyema mgongoni mwake asiyekuwa na makovu na awe anafahamu historia ya nchi na vitendo vyake viwe vya kuridhisha.

Umri katika urais
Suala la umri katika urais lisiwe ni kigezo kinachotakia ni kuangalia wasifu wake, awe na sifa zinazokubalika na awe pia mtu anayeweza kuingia sehemu yeyote na kukubalika na makundi yote.

Anasema katika urais ukiruhusu suala la umri utagombanisha makundi yaliyopo, suala la ujana na uzee lisipewe kipaumbele katika kuelekea uchaguzi mkuu.

Mashishanga anasema Chama Cha Mapinduzi (CCM) lazima kitafute mgombea urais ambaye ni chaguo la wengi ambaye ana uzalendo uliotukuka, aliongeza kuwa siku hizi kumekuwa na upendeleo katika chama na kimekuwa hakifanyi utafiti wa nani anafaa kuwa kiongozi wa mahala fulani.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: