WAISLAMU nchini wamewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kurudi katika Bunge Maalumu la Katiba.
Mwito huo ulitolewa jana na Alhaji Seleman Lolila, alipokuwa akisoma salamu za Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) katika sherehe za Baraza la Idd el Fitr zilizofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam jana.
Mbali na salamu hizo za Baraza la Idd, mwito huo pia ulitolewa na mashekhe wa mikoa tofauti nchini kuwataka Ukawa kurejea bungeni.
Akisoma salamu za Idd, Alhaji Lolila alisema Bunge Maalumu la Katiba, limepata pigo kwa baadhi ya wajumbe wake, kuamua kususia. “Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) linawasihi wale wote waliotoka nje ya Bunge warejee mara Bunge litakapoanza shughuli zake ili kuwawezesha Watanzania kupata Katiba yao mpya.
“Taifa tayari limetumia gharama nyingi kuanzisha mchakato huu wa Katiba mpya, kama zipo tofauti za mawazo au msimamo, zijadiliwe ndani ya Bunge kwa kutumia rasimu iliyowekwa mbele yao,” alisema.
Akizungumzia mwito huo wa Baraza la Idd, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema lengo la kuanzisha mchakato huo lilikuwa jema.
Alifafanua kuwa baada ya kutafakari Taifa lilipotoka katika miaka hamsini iliyopita, nia ilikuwa kutafuta Katiba mpya itakayopeleka Taifa katika miaka 50 ijayo kwa maendeleo zaidi.
“Katika miaka hamsini iliyopita tulikuwa tukipambana na umasikini, maradhi na ujinga, tukaona tuweke misingi mizuri zaidi ya kupambana na maadui hawa…hili ndio lengo na nia njema tuliyokuwa nayo,” alisema Pinda.
Alisema ni kweli mchakato huo umepitia katika mtikisiko kidogo, lakini rai hiyo ya Bakwata, ndio rai ya karibu kila Mtanzania kwa Ukawa.
Naye Fadhili Abdallah, anaripoti kutoka Kigoma kwamba waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Kigoma, wametaka Ukawa kurudi bungeni kuendelea na mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya.
Kaimu Shekhe wa Mkoa Kigoma, Iddi Hassan Kiburwa alisema kuwa wajumbe wa Ukawa wanapaswa kurudi bungeni na kwenda kupeleka hoja zao badala ya kupigia kelele nje ya Bunge.
"Kwa sasa tunaomba Ukawa warudi bungeni wakapiganie hoja zao huko na wananchi tuko nyuma yao, tunapenda kuona mchakato wa Katiba mpya unaendelea ili tupate Katiba ambayo itasimamia haki na maslahi ya Watanzania," alisema Shekhe Kiburwa.
Alisema kuwa kitakachojadiliwa bungeni siyo mwisho, kwani ipo sehemu ambayo Katiba italetwa kwa wananchi ili ipigiwe kura na hapo kama kuna mambo ambayo hayakwenda sawa, basi nguvu ya wananchi itatumika kuamua juu ya mustakabali wa Katiba hiyo.
Shekhe wa Wilaya ya Kigoma, Twalha Kiburwa alisema viongozi wa dini hawaoni kwa sasa kama kutoka bungeni ndiyo suluhisho la kile kilichotokea na badala yake warudi bungeni wakazungumze kile ambacho wanadhani kilikuwa kero na kuwafanya wakatoke nje ya Bunge.
Kutoka mkoani Morogoro, John Nditi, anaripoti Kaimu Shekhe wa Mkoa wa Morogoro, Ally Omary, jana alitaka Ukawa kurejea bungeni ili kuendelea kujadiliana katika mambo mbalimbali ya msingi yaliyomo kwenye Rasimu ya pili ya Katiba mpya kwa ajili ya manufaa kwa Watanzania wote.
Alisema kuwepo bungeni ndiyo njia pekee ya kufikiwa kwa makubaliano ya pamoja ya mambo mbalimbali yaliyomo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba mpya. Shehe huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Mashehe wa Mkoa huo, alisema kuendelea kususia Bunge na pia kufanya mikutano ya hadhara kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hakutasaidia jambo lolote .
Hata hivyo, alisema kutosaidia lolote huko kunatokana na wanachokiongelea kwa wananchi hakitokani na maamuzi ya wabunge wote wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwemo walioteuliwa na Rais pamoja na wa kuchanguliwa na wananchi.
“Nawaomba Ukawa warejee bungeni na hata wale walioteuliwa na Rais ...majadiliano ya pamoja ndiyo njia pekee itakayowezesha kupatikana Katiba bora itakayokuwa na maslahi ya wananchi.
“Yatakayoamuliwa katika majadiliano na wabunge wote, ndiyo yatakayoletwa kwa wananchi ili waamue na si kundi mmoja la Ukawa kupita kwa wananchi kuelezea mambo ambayo hayajafikiwa katika uamuzi na kabla ya bunge kumaliza muda wake,” aliongeza kusema.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / siasa
/ WAISLAMU WACHUKUA JUKUMU LA KUWABEMBELEZA VIONGOZI WA UKAWA KURUDI KATIKA BUNGE LA KATIBA DODOMA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment