WAMEKENGEUKA HAO !!!: CHAMA CHAA MADAKTARI TANZANIA CHAICHONGEA SERIKALINI CHUO KIKUU CHA KIMATAIFA CHA TIBA NA TEKNOLOJIA JUU YA KUTUPA OVYO MABAKI YA VIUNGO VYA MAITI YA BINADAMU LALALANI JIJINI DAR ES SALAAM.
Dar es Salaam.
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimezitaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua kali za haraka dhidi ya taasisi na watu waliojihusisha na utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wito wa MAT umetolewa siku moja baada ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), kukiri kuhusika na mabaki hayo ya viungo vya binadamu yaliyotupwa katika utaratibu usio wa kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho, Dk Primus Saidia alisema wahusika wote wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kitendo hicho kimekiuka sheria, taratibu, ubinadamu, maadili ya ufundishaji na taaluma ya udaktari.
“Kama ni taasisi ya utafiti imepoteza sifa ya kufanya utafiti na kama ni ya mafunzo basi imepoteza sifa ya kutoa mafunzo ya tiba. Kama ni hospitali itakuwa imepoteza sifa za kutoa tiba kwa binadamu,” alisema Rais MAT, Dk Saidia.
Dk Saidia alisema ni wazi kwamba kwa kitendo hicho, watu na taasisi iliyohusika wamepoteza sifa za kufanya utafiti au kutoa mafunzo kwa kutumia miili au viungo vya binadamu.
Alisema kitendo hicho kimeifedhehesha tasnia nzima ya tiba kwa kuwa mwenendo mzima wa kutumia viungo hivyo na kuviteketeza hufanywa kuwa siri na kwa hapa nchini wamekuwa wakitumia viungo hivyo kwa utaratibu mzuri uliowekwa kisheria tangu mwaka 1963 kilipoanzishwa Chuo Kikuu cha Muhimbili kikiwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema MAT inatoa wito kwa vyombo husika; Polisi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Baraza la Madaktari Tanzania, Tume ya Usimamizi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuchukua hatua stahiki kwa mtu au taasisi iliyohusika.
Ni utaratibu wa kawaida.
Dk Saidia alisema katika tasnia ya tiba ni utaratibu wa kawaida unaokubalika duniani kote kutumia miili na viungo halisi vya miili ya binadamu (Cadaver) kufundisha na kufanya tafiti mbalimbali za kiafya, lakini huwahusu zaidi wanataaluma.
“Miili na viungo hivi hutumika kwa heshima kubwa kama walimu wa kwanza katika mafunzo na tafiti za tiba ya mwanadamu. Tafiti na mafunzo haya ndiyo nguzo kuu katika kukuza ufahamu wa mwili wa binadamu na hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya,” alisema.
Alisema kwa sasa jambo geni linaloweza kuzungumzwa ni jinsi mabaki ya viungo hivyo yalivyotupwa katika utaratibu unaozua mjadala.
Mtambo wa kuharibu mabaki.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema jana kwamba juhudi za kutengeneza mashine ya kuteketeza taka ikiwamo miili hiyo (Incinerator) ambayo imeharibika kwa miezi sita sasa, zinaendelea lakini hajui ni lini itakuwa tayari.
Gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, lilieleza jana kwamba kwa miezi sita sasa mashine hiyo haijafanyiwa matengenezo.
Pia Aligaesha alisema hawezi kueleza utaratibu wa kuchukua au kurejesha mabaki hayo katika hospitali hiyo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia upatikanaji wake akidai kufanya hivyo kunaweza kuingilia upelelezi wa polisi
Wizara yaeleza kushtushwa.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeeleza kushtushwa na tukio la kutupwa kwa viungo hivyo na kusema inafuatilia kwa karibu upelelezi wa polisi ili kuchukua hatua.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo, Nsachris Mwamaja alisema jana kuwa tukio hilo ni kinyume na kanuni na sheria za kitabibu, kwani hakuna sehemu yoyote inayoruhusu mwili wa binadamu kutupwa kama ilivyotokea.
“Hatuwezi kulizungumzia sana, tunaweza kuharibu upelelezi, hebu tuache tusubiri polisi watatupa majibu gani.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment