“Hakuna kifungu cha sheria kinachosema Rais anaweza kulivunja Bunge hilo, bali linaweza kuahirishwa. Nami ningeshauri liahirishwe hadi hapo maridhiano yatakapopatikana,”.
Dar/Zanzibar.
Zikiwa zimebaki wiki mbili kuanza vikao vyake, baadhi ya wanasheria wamehoji uhalali wa Bunge hilo kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba bila ya kuwapo kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wamesema msimamo wa Ukawa kukataa kurejea katika vikao vya Bunge hilo na kushikilia msimamo wa kutaka ijadiliwe Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, utafanya akidi ya wajumbe kwa ajili ya kupitisha uamuzi katika Bunge hilo kutotimia.
Wanasheria hao waliohojiwa jana kuhusu msimamo wa Ukawa kususia Bunge na hatima ya Katiba Mpya wamesema hakuna uwezekano wa kisheria kuipitisha wala kufanya mabadiliko ya vifungu ili kupata uhalali wa kufanya hivyo.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Julai 8 mwaka huu, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta alisema iwapo Ukawa watarudi bungeni lakini wakasusa tena kadri mjadala utakavyoendelea, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.
Hata hivyo, wanasheria hao walisema kwamba bila kuwapo maridhiano, Bunge hilo haliwezi kufikia tamati na si rahisi kupata akidi ambayo si tu inatakiwa na Kanuni za Bunge na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bali pia Katiba ya sasa.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Kifungu cha 26(2) kinaeleza: “Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika Bunge Maalumu, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Zanzibar.”
Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jesse James alisema iwapo hakutakuwa na maridhiano hakuna chochote kinachoweza kufanyika au kupitishwa zaidi ya kuahirisha Bunge hilo hadi pale watakapokubaliana.
“Hakuna kifungu cha sheria kinachosema Rais anaweza kulivunja Bunge hilo, bali linaweza kuahirishwa. Nami ningeshauri liahirishwe hadi hapo maridhiano yatakapopatikana,” alisema James.
Kuhusu kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kubadili akidi ya wajumbe wa pande zote mbili, James alisema hilo litasababisha vurugu zaidi.
Alisema hilo linaweza kufanyika kwa kuitishwa kwa Bunge la Muungano, lakini kwa maoni yake itakuwa ni uhuni kwa kuwa haiwezekani kubadilisha kanuni wakati mchezo umeshaanza.
“Wakifanya hivyo itakuwa ni vurugu tupu, watakuwa wanapitisha kwa matakwa yao kitu ambacho kitaleta shida wakati itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya upigaji kura,” alisema James na kuongeza:
“Wakati wa upigaji kura italeta shida kwani hawa ambao hawakubali watapiga kampeni kuwaeleza wananchi wasiikubali kwa kuwa si matakwa yao na hapo itakuwa vurugu zaidi.”
Akizungumzia suala la Sitta kuitisha kikao cha maridhiano James alisema Mwenyekiti huyo wa Bunge la Katiba amefanya hivyo kutokana na mambo kuwa magumu lakini hana mamlaka ya kufanya hivyo kisheria.
Haya hivyo, wakili na kiongozi mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kitendo cha kutaka kubadilisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kitapoteza uhalali wa kisheria wa kuwapo kwa Bunge hilo na ni kinyume na Katiba ya nchi Ibara ya 98 inayoeleza kuwa, ili Bunge liweze kufuta mambo fulani ni lazima likubalike katika pande zote za Muungano (Bara na Zanzibar).
Sungusia alisema ili kubadilishwa kwa sheria hiyo, ni lazima Bunge la Muungano likutane na kuongeza kuwa, kwa muda uliobaki jambo hilo ni gumu, labda kiitishwe kikao cha dharura cha Bunge.
“Haya yote yametokana na Bunge la Jamhuri kuwa sehemu ya Bunge la Katiba. Ilitakiwa mabunge haya yajitegemee na kutoingiliana katika utendaji wake wa kazi. Ndiyo maana wapo wanaolalamikia tafsiri ya Kifungu cha 25 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura alisema: “Endapo Ukawa hawatarudi bungeni hakuna uamuzi utakaopitishwa na hata ikibadilishwa sheria ni wazi kuwa itakuwa kwa manufaa ya watu fulani.”
Alisema Bunge linaweza kubadili sheria lakini ubadilishwaji huo usiwe kwa sababu ya kukwepa upungufu wa akidi na kusisitiza kuwa ni lazima zitafutwe njia za kuwarejesha wajumbe wa Ukawa bungeni na kila upande uwe na utashi.
“Kama kuna sheria ifuatwe na kama kuna tatizo litatuliwe na siyo kubadili sheria husika. Kama yote hayatawezekana ni vyema mchakato ukaanza upya,” alisema.
CCM, Ukawa wazungumza
Mjumbe wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema wapo katika mazungumzo na CCM kutafuta mwafaka.
“Tupo katika mazungumzo ila kwa sasa hatuwezi kusema kama tutashiriki au hatutashiriki vikao vingine. Tukiridhiana kisiasa tunaweza kwenda katika kikao cha Sitta (cha maridhiano),” alisema Mbatia.
Hata hivyo, Mbatia alisema ni vigumu Bunge la Katiba kupitisha jambo lolote bila akidi kutimia na kusisitiza kuwa kama sheria itabadilishwa, ni wazi haitakuwa sheria nzuri.
“Uandikaji wa Katiba ni tendo la maridhiano na siasa inafuata baadaye, ili kubadili sheria ni lazima Bunge la Jamhuri likutane wakati ratiba zinaonyesha kuwa litaketi Novemba,” alisema.
Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisisitiza msimamo wa Ukawa na chama chake kuwa wajumbe wake hawatarejea bungeni iwapo itajadiliwa rasimu nyingine tofauti na ile ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe alitaja mambo mengine ambayo yatawafanya warejee katika Bunge hilo kuwa ni kuendeleza mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete kwa sababu ndiye msimamizi mkuu wa mchakato huo.
Nape alia na Ukawa
Wakati Ukawa wakiwa katika mazungumzo na CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye amewataka Ukawa kurudi bungeni, akisema suala la kuzunguka kwa wananchi ili wasiipigie kura Katiba Mpya ni la mwisho ambalo kila mdau atashirikishwa ili kuipata katiba iliyo bora.
Nape aliyasema hayo akijibu msimamo uliotolewa na Mbowe wa kutorejea bungeni na kwenda kwa wananchi kuwaambia waikatae Katiba itakayopendekezwa.
“Nilisikia alichokisema Mbowe jana (juzi). Sisi (CCM) tunawashauri warudi bungeni ili tuipitishe Katiba na muda utakapofika wananchi waambiwe ukweli. Wao waipinge na sisi tuitetee ili tuone wananchi wataamua nini kwa sababu kwa vyovyote itakavyokuwa, wao ndio wenye uamuzi wa mwisho,” alisema Nnauye.
ZIRPP wamkosoa Sitta
Katibu wa Kamati ya Kuwaunganisha Wazanzibari katika mjadala wa Katiba Mpya (ZIRPP), Muhammed Yussuf Mshamba amesema Sitta alianza kazi yake vibaya kwa kuruhusu kanuni kubadilishwa kabla ya kuanza kutumika kupitisha Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hayo jana wakati wajumbe sita wa kamati hiyo walipokutana na kumteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Kiongozi Zanzibar, Ali Abdallah Suleiman kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo.
Alisema kwa kuwa kanuni zilitungwa na kupitishwa na bunge hilo, haikuwa mwafaka kubadilishwa kabla ya kuanza kutumika katika kupitisha vifungu vya Rasimu.
Imeandikwa na Boniface Meena, Fidelis Butahe, Julius Mathias na Mwinyi Sadallah.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment