FIMBO ZA KUCHUNGIA MIFUGO ULANGA, ZAGEUKA KERO KWA WASICHANA, WANAUME HUTUMIA KUMPATA MSICHANA KIURAHISI.
Na Lilian Lucas, Mwananchi.
Ulanga…Uongozi wa serikali katika Tarafa ya Ngahelango wilayani Ulanga, umewapiga marufuku wananchi wake na hasa wafugaji wa jamii ya Kisukuma, kutembea na fimbo mitaani kwa sababu baadhi yao wanazitumia vibaya ikiwa ni pamoja na kuwakimbiza wasichana wanaowataka kimapenzi.
Kupigwa marufuku kwa fimbo hizo ambazo mara nyingi hutumiwa na vijana wa kiume na watu wazima wa jamii ya wafugaji hasa Wasukuma kama ulinzi wao, kunatokana na kuzitumia isivyo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji vya Ngohelanga na Ihowanja, Ofisa Tarafa ya Ngohelanga Conrad Mzwalandili, alisema uamuzi huo umetokana na malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali kuhusu kuathiriwa na matumizi mabaya ya fimbo.
Hata hivyo wafugaji hao walielezwa kutoridhishwa kwao kuhusu kupigwa marufuku kwa fimbo hizo walizosema kuwa ni sehemu ya utamaduni wao.
Mzwalandili alisema kuwa fimbo hizo wakati mwingine zimekuwa zikitumika kuwashambulia watu wasiokuwa na hatia na kusababisha mauaji.
Ofisa tarafa huyo alisema wakati wakiendela kufanya msako wa kukamatwa kwa fimbo hizo pia wamepiga marufuku ngoma ya kienyeji ijulikanayo kama Sagulaga ambayo imekuwa ikiwadhalilisha wasichana hasa wenye umri mdogo.
“Hadi sasa tumefanikiwa kukamata fimbo zaidi ya 100. Lakini pia tumepiga marufuku ngoma aina ya Sagulaga inayowadhalilisha mabinti wakiwemo wanafunzi,”alisema afisa tarafa huyo.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Ihowanja, katika Tarafa ya Ngohelanga,wameilalamikia serikli ya kijiji chao kugawa maeneo kiholela kwa wageni kutoka nje,huku fedha zinazopatikana wakiwa hawajui matumizi yake.
Walisema baadhi ya vijiji jirani vimekuwa vikigawa maeneo ya kijiji chao isivyo halali kwa wafugaji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihowanja,Yonas Ngonyani, alisema wanaolalamikia matumizi mabaya ya fedha za kijiji ni wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa wakiwashawishi wananchi kutoshiriki kazi za kujitolea kwa maendeleo yao.
0 comments:
Post a Comment