HAKIMU ATAKA WAFUNGWA KUPEWA DHAMANA, KISA GEREZA LIMEJAA WAFUNGWA.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, Jovith Katto amelazimika kuwaomba ndugu wa wafungwa wa Gereza la Biharamulo wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitatu kuwadhamini ndugu zao ili watoke kwa madai kuwa gereza hilo limejaa wafungwa.
"Nitumie fursa hii kuwaomba muende mkawadhamini jamaa zenu walio na kifungo kisichozidi miaka mitatu ili warejee kutumikia adhabu zao huku uraiani kwa kuwa gereza la Biharamulo limejaa," alisema hakimu huyo.
Alitoa kauli hiyo kwenye mafunzo ya wasaidizi wa kisheria yaliyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa haki za binadamu la Community Partcipation Development Association (Copadea) kwa ufadhili wa Sekretariet ya Msaada wa Kisheria Tanzania (LAS).
Kadhalika alilitaka Shirika la Copadea kushirikiana na idara ya maendeleo ya jamii ya wilaya ya Chato ili kuhakikisha wanawasaidia wananchi wenye kuhitaji kuwadhamini ndugu zao waliopo kwenye gereza hilo ambalo linahudumia pia wafungwa kutoka wilaya hiyo ili kuepusha msongamano na malalamiko mengi kwa mahakama yake.
Katto aliwataka wajumbe waliohudhuria mafunzo hayo yatakayofanyika kwa siku 20 kuhakikisha wanakwenda kuielimisha jamii ili kuepukana na kutenda makosa ambayo yamekuwa yakiwasababisha kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa vifungo kwenda gerezani.
Alisema Wilaya ya Chato ni miongoni mwa wilaya za mkoa wa Geita zenye mauaji ya watu kujichukulia sheria mkononi kutokana na kuamini imani za kishirikina ambapo baadhi ya wazee wamekuwa wakiuawa bila kuwa na hatia.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la Copadea, Protas Malijani, alisema asasi hiyo imekuwa ikijishughulisha na utetezi wa haki za binadamu ili kuisaidia jamii kuishi kwa amani na upendo badala ya kuvunja sheria kwa makusudi na kuifanya jamii kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo.
Malijani alisema mafunzo hayo yanatokana na hitaji kubwa la msaada wa kisheria kwa watoto, wanawake na makundi maalumu, ambapo watoto wamekuwa wakiachishwa masomo ili kufanya shughuli za kiuchumi, mimba za umri mdogo na wengine kutelekezwa mitaani.
Aidha, mafunzo hayo yanapaswa kuisaidia jamii kutambua kulinda na kuthamini haki za binadamu ili kuwa na taifa lenye amani, upendo na utulivu.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment