BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JK AFICHUA SIRI YA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI MOROGORO NA DAWA YAKE TAYARI IPO JIKONI.

RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake italipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo sugu la ugomvi kati ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro ambalo kimsingi linasababishwa na wachungaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima.
Aidha, amewataka wachungaji kuacha mara moja tabia yao ya kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima akisisitiza kuwa hicho ndicho chanzo cha ugomvi kati ya makundi hayo mawili.

Rais Kikwete ambaye anafanya ziara ya siku saba katika Mkoa wa Morogoro ametoa ahadi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa ugomvi kati ya makundi hayo baada ya kulalamikiwa kila aliposimama na wananchi kuhusu tabia ya wafugaji kuingiza na kulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima.

Akiwa njiani kutoka Ifakara, Wilaya ya Kilombero kwenda Wilaya ya Morogoro, Rais Kikwete ameshuhudia mwenyewe malalamiko hayo ya wananchi dhidi ya tabia hiyo ya wafugaji ambao wengi wao sio wakazi ama wenyeji wa Mkoa wa Morogoro.

Baada ya kujaribu kuwaeleza wananchi katika maeneo mbali mbali kuhusu chanzo cha ugomvi huo na nini hasa ufumbuzi wa suala hilo, Rais Kikwete amewaambia wananchi katika Kijiji cha Mgalegole-Mngazi, eneo la Duthumu, Tarafa ya Bwakila: “Nakwenda sasa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Ni lazima tukomeshe tatizo hili.”

Alisisitiza: “Kimsingi, huu ni ugomvi usiostahili kwa sababu kila mmoja kati ya makundi haya anamhitaji mwenzake. Wafugaji wanahitaji chakula…ugali na mchele...kutoka kwa wakulima. Nao wakulima wanahitaji kitoweo…nyama kutoka kwa wafugaji. Kubwa hapa ni wafugaji kuacha kulisha ng’ombe kwenye mashamba ya watu wengine.”

“Mnawaachia watoto kuchunga ng’ombe. Wanaingiza mifugo katika mashamba ya watu. Wakiwauliza mnawapiga, mnawajeruhi. Acheni mambo haya.”

Rais Kikwete alianzia ziara yake juzi kwa kuweka jiwe la msingi katika upanuzi wa Kituo cha Afya Kibaoni, mjini Ifakara, ambacho kinapanuliwa kuwa Hospitali ya Wilaya na baadaye akakabidhi madawati 278 kwa shule 17 za msingi za Tarafa za Mang’ula na Kidatu katika Wilaya ya Kilombero. Madawati hayo yametolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi (TANAPA).

Baadaye, Rais Kikwete anayefuatana na mkewe, Mama Salma Kikwete katika ziara hiyo alipanda treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kwenda Kisaki, Wilaya ya Morogoro, ambako amelakiwa na mamia kwa mamia ya wananchi.

Rais Kikwete pia alizindua Mradi wa Maji wa Duthumu uliofadhiliwa na wanachama wa Lions Clubs za Sweden na pia kuzindua vifaa na huduma ya upasuaji katika Kituo cha Afya katika eneo hilo.

Katika mji mdogo wa Mtamba, Rais Kikwete alizindua soko jipya la kisasa na kuzungumza na wananchi ambako aliahidi kuwa Serikali imeanza kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Bingwa-Mvua kwa kiwango cha lami.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: