MGOMBEA URASI KUPITIA CCM AENDA VATICAN KUSAKA DUA ZA URAIS.
RAIS JAKAYA KIKWETE WA TANZANIA
NA MWANDISHI WETU
WAKATI joto la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 likiendelea kupanda miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaohusishwa na harakati za kuwania urais, mmoja wa makada hao amekwenda Vatican kwa nia ya kutafuta uungwaji mkono wa Kanisa Katoliki duniani, MTANZANIA Jumapili limedokezwa.
Habari za uhakika kutoka katika chanzo cha karibu na kada huyo ambaye pia ni waziri kwenye moja ya wizara nyeti nchini, kimedai kuwa waziri huyo amezuru jijini Vatican hivi karibuni.
Mtoa habari wetu huyo alilidokeza gazeti hili kuwa licha ya ziara ya waziri huyo jijini Vatican kuonyesha kuwa ni ya kikazi, lakini lengo kuu la kuelekea huko lilikuwa ni kutambulisha dhamira yake ya kuwania urais 2015.
Alisema kuwa waziri huyo, ambaye katika historia ya elimu inaonyesha amepata kusoma shule ya seminari, alipofika mjini Vatican alikutana kwa faragha na maofisa kadhaa wa Kanisa Katoliki duniani, ambapo alitumia nafasi hiyo kupenyeza lengo lake kuhusu dhamira ya kugombea urais mwakani.
“Alikwenda Vatican akiwa na lengo la kutafuta uungwaji mkono wa Kanisa Katoliki na tangu amerudi amekuwa akijinadi kwamba Vatican itamuunga mkono Rais wa Tanzania mwaka 2015,” alisema mtoa habari wetu huyo.
Awali gazeti hili lilidokezwa na chanzo kingine cha habari ambacho kipo naye karibu katika wizara anayoiongoza kuwa waziri huyo alisafiri kwenda Vatican mwishoni mwa Julai na akarejea nchini mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu.
Mbali na ziara ya Vatican, waziri huyo amedaiwa kuwa na mpango wa kukutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki hapa nchini, Kardinali Polycarp Pengo, kwa lengo la kumdokezea juu ya dhamira yake hiyo, hasa baada ya kuwa amerudi kutoka makao makuu ya kanisa hilo.
Katika hatua nyingine, gazeti hili lilimkariri mmoja wa vijana anayeunda kundi linalompigia kampeni waziri huyo akisema: “Tayari tupo vijana ndani ya CCM ambao tumeanza kuzunguka nchi nzima kueneza habari hii ya mavuno kwetu”.
Pia kijana huyo alidokeza kwamba hivi karibuni waziri huyo ameingiza nchini magari 24 aina ya VX Land Cruiser kutoka katika nchi za Falme za Kiarabu kwa ajili ya kuendesha mkakati wa kundi lake wa kuzunguka nchi nzima kutafua ushawishi ndani na nje ya chama.
Kijana huyo alidai kwamba moja ya magari hayo analitumia mmoja wa viongozi wa juu wa CCM ambaye hivi karibuni alikwenda nalo mjini Dodoma kuhudhuria vikao vya Kamati Kuu ya chama (CC).
Waziri huyo anayetajwa katika mikakati ya sasa ni mmoja kati ya makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanatumikia kifungo cha mwaka mmoja cha kutojihusisha na masuala ya siasa kwa kosa la kuanza kampeni za urais mapema kinyume cha kanuni za chama.
Wanaotumikia adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward, Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira.
Wengine ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba pamoja na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment