RAIS KIKWETE ACHUKIZWA NA VITENDO VYA WALIMU KUWALIMISHA WANAFUNZI MASHAMBANI ILI KUPATA CHAKULA CHA LISHE YA UJI.
Rais Jakaya Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete ametaka kuondolewa kwa mpango wa kuwalimisha wanafunzi ili waweze kupata chakula wakiwa shuleni kwani dhamana ya kumlisha mtoto ni ya mzazi na mtoto hatakiwi kujilisha mwenyewe.
“Dhamana hii lazima wazazi wabebe ili mtoto asilimie uji wake,” alisema Rais Kikwete. Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Kauli ya Rais Kikwete ilikuja baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Ally kusema wanafunzi wa shule za wilaya hiyo wamekuwa wakipata uji na chakula cha mchana shuleni lakini baada ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kujitoa kulisha uji shule zimelazimika kuwa na mashamba yao ili kuwezesha watoto kupata uji wakiwa shuleni.
Rais Kikwete alisema ni vizuri shule zikaanza kidogo kidogo kujitegemea kwa wazazi kuchangia ili watoto waendelee kupata uji shuleni. “Mkianza kusema watoto wajilimie wenyewe itakuwa taabu walimu wataanza kushindana na watoto,” alisema.
Alisema watoto wa shule za msingi ni wadogo hiyo ni dhamana ya wazazi wao lazima watimize wajibu wao. Alisema wakiachwa watoto walimie uji wao itakuwa ni shida kubwa kwa watoto, kwani watakuwa hawasomi ni majembe tu.
Ameitaka halmashauri hiyo kuangalia namna ya kuwapatia uji wanafunzi wakiwa shuleni ikiwa ni pamoja na wazazi kutimiza wajibu wa kuchangia chakula kila baada ya mavuno, ili shule ziendelee kuwa na akiba ya chakula bila kutegemea watoto kulima.
Awali Mkuu wa ofisi ya WFP Mkoa wa Dodoma, Neema Sitta alisema mpango wa kutoa chakula shuleni uko katika wilaya nne za Mkoa wa Dodoma ambapo wanafunzi wa shule za msingi zaidi ya 400 wanafaidika nao.
Alisema, siku za nyuma walikuwa wakitoa uji na chakula cha mchana, lakini baada ya ufadhili kupungua waliamua shule zijitegemee kwa uji, lakini wao wataendelea kutoa chakula cha mchana.
Alipohojiwa na Rais Kikwete mpango wa chakula mashuleni utatolewa na WFP mpaka lini alisema bado hajajua ni lini, lakini WFP imepunguza idadi ya shule ilizokuwa ikizihudumia. Wilaya ya Chamwino ina jumla ya shule za msingi 110.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment