BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI ACHIWA KWA DHAMANA NA JAJI WA MAHAKAMA KUU ZANZIBAR.


Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mansour Yusuph Himid akifuatilia hukumu ya ombi la dhamana yake jana. Jaji Abraham Mwampashi alimwachia kwa dhamana dhidi ya kesi inayomkabili ya kupatikana na silaha ya moto na risasi 407.Picha na Mwinyi Sadallah

Zanzibar.
Mahakama Kuu ya Zanzibar imemwachia kwa dhamana waziri wa zamani wa SMZ, Mansour Yusuph Himid ikisema hakuna kosa lisilokuwa na dhamana Zanzibar kwa mujibu wa sheria kwa kuwa si hatari kumiliki silaha, bali matumizi yake ndiyo hatari.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Abraham Mwampashi katika ombi la dhamana lililofunguliwa kwa hati ya dharura, baada ya Mahakama ya Mkoa chini ya Hakimu Khamis Abdallah Shaban kumnyima dhamana ikisema kosa la kumiliki silaha halina dhamana.


Akisoma uamuzi huo kwa zaidi ya saa moja, Jaji Mwampashi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama imeamua kumpatia waziri huyo dhamana kwa vile Kifungu cha 150 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2004 kinaipa uwezo Mahakama hiyo kutoa dhamana kwa makosa ya aina yoyote.


Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, kosa la kupatikana na silaha ya moto halina dhamana katika mahakama za chini, lakini Mahakama Kuu imepewa uwezo wa kutoa dhamana kwa kuzingatia mazingira ya kesi, uadilifu, busara za jaji na rekodi za mshtakiwa kama hajawahi kutenda kosa lolote la jinai au kushindwa kuhudhuria mahakamani.


Jaji Mwampashi alisema hoja za upande wa mashtaka kuwa kuwapo nje kwa mtuhumiwa huyo kunahatarisha usalama wa nchi na jamii kwa jumla haina mashiko yoyote kwa vile hakuna ushahidi wowote uliothibitishwa mbele ya Mahakama namna mshtakiwa atakavyohatarisha amani.


“Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kwa ushahidi namna mtuhumiwa atakavyohatarisha usalama wa nchi, hatukuambiwa kuwa ana tabia ya kutishia watu silaha au ana tabia ya kutembea nayo na kuionyesha mbele ya hadhara.


“Hawakuonyesha kuwa mshtakiwa alikuwa anatishia jirani zake au kuua kunguru nyumbani kwake, lakini hata alipokamatwa, silaha hiyo haikuwa imetundikwa, bali ilipekuliwa na kukutwa imehifadhiwa kwa tahadhari,” alisema Jaji Mwampashi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: