BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ZANZIBAR YAPOKEA VIFAA VYA KUCHUNGUZA EBOLA.


WIZARA ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea vifaa mbalimbali vya kuchunguza wagonjwa watakaobainika kuambukizwa na ugonjwa hatari wa ebola huku ikiweka mikakati zaidi kudhibiti bandari bubu zinazotumiwa kuingiza wageni kinyume cha sheria.

Akikabidhi vifaa hivyo katika kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa cha Abeid Amaan Karume, Ofisa wa kitengo cha kupambana na maradhi kutoka Wizara ya Afya, Salma Masauni alisema kifaa hicho kinachojulikana kwa jina la 'Thermos scan' kina uwezo wa kutambua kama mgonjwa ameambukizwa ugonjwa wa homa ya ebola kwa kiasi gani.

Alisema juhudi hizo zimechukuliwa kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo ambapo vitawekwa katika sehemu zote kuu za kupokea wageni ikiwamo Uwanja wa Ndege pamoja na Bandari Kuu.

Alibainisha kuwa kabla ya vifaa hivyo vya kubaini kiasi cha ugonjwa kwa aliyeathirika na ebola ambao ni tishio kwa baadhi ya nchi zikiwamo za Afrika ya Magharibi, Zanzibar ilikuwa haina vifaa vya kupambana na ugonjwa huo.

Aliongeza kuwa vifaa hivyo lengo lake kubwa ni kutambua ugonjwa huo katika hatua zake za mwanzo na vitawekwa katika sehemu zote za kupokea wageni.

Aidha, Masauni aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa msaada wao mkubwa uliofanikisha kupata vifaa hivyo.

Mapema akipokea vifaa hivyo, Daktari Mkuu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume, Juma Mohamed alisema vifaa hivyo ni muhimu kwa ajili ya kutambua dalili za ugonjwa huo kwa wageni wanaowasili nchini.

Alisema vifaa hivyo vinahitajika sana zaidi kwa sababu uwanja wa ndege wa Zanzibar ni wa kimataifa ukiwa unatumiwa na ndege mbalimbali ambazo baadhi ya mashirika yalikuwa yakiulizia kuhusu kuwepo kwa vifaa vya kutambua ugonjwa huo.

“Tulikuwa tunaulizwa na baadhi ya mashirika ya ndege kuhusu mikakati yetu ya kukabiliana na ugonjwa wa ebola katika hatua za mwanzo,” alisema Mohamed.

Kamati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa wa ebola imesema ulinzi zaidi unatazamiwa kuwekwa katika maeneo ya bandari bubu ambazo hutumiwa kuingiza wageni. Ofisa mmoja kutoka katika ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais alisema zipo bandari nyingi ambazo sio rasmi hivi sasa na zimekuwa zikiingiza wageni kinyume cha sheria.

“Tumeanza kuweka mikakati hiyo ya kuzikagua bandari ambazo sio rasmi zinazojishughulisha kuingiza wageni nje ya nchi,” alisema ofisa huyo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: