BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ASKARI WA USALAMA BARABARA WABEBESHWA LUNDO LA LAWAMA, WATAJWA KUWA CHANZO CHA KUKITHIRI KWA AJALI TANZANIA.


POLISI wa usalama barabarani, wametwishwa zigo la kuwa chanzo kikubwa cha ajali zilizoshamiri nchini, kutokana na vitendo vyao vya kuendekeza rushwa kutoka kwa madereva wa mabasi ya abiria.

Katika mkutano wa wadau wa sekta ya usafirishaji ambao ulikuwa ukizungumzia namna ya kumaliza ajali, trafiki walinyooshewa kidole kuwa wamegeuza tochi na vizuizi, kama miradi na vitega uchumi kwa ajili ya kujipatia mapato yasiyo halali.

Ilielezwa kuwa kutokana na rushwa kuipotosha trafiki, madereva hawaheshimu tena ratiba walizopangiwa na Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kwani kila kwenye vizuizi vya polisi wanaacha fedha na hata ratiba hiyo kutozingatiwa.

“Ratiba inasema kutoka Singida kuja Dodoma ni saa 2, lakini mtu anatumia saa moja na nusu, na hakuna hatua zinazochukuliwa kwa sababu polisi wamegeuza kazi zao kama miradi ya kujitajirisha,” alisema Ally Mkali ambaye ni mmliki wa mabasi ya Mangole.

Sababu nyingine ambayo imejitokeza kwenye mkutano huo kuwa inachangia ajali nyingi ni kutokana na wamiliki wengi wa mabasi na malori kutumia madereva ambao hawana mafunzo mazuri ya udereva.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alisema wamefanya ukaguzi na kubaini kuwa wamiliki wanatumia madereva ambao hawana mikataba yoyote kwa kuogopa kuwalipa madereva wenye ujuzi mishahara mizuri.

Kuanzia sasa Kabaka aliagiza Sumatra ihakikishe madereva wote wanakuwa na mikataba halali na waajiri wao na wafuate taratibu zote za uajiri, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mikakati ya Sumatra
Mtendaji Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alitaja mikakati ya kupunguza ajali kuwa ni kuimarisha kupima ulevi na kampuni ambazo madereva wake watabainika na makosa hayo watatangazwa kupitia vyombo vya habari na kuwachukulia hatua.

Alisema kila dereva atakayekutwa na kosa, watataka kuona mkataba wake wa ajira na kadi yake ya mifuko ya pensheni aliyojiunga nayo ili kuepusha wamiliki kutoajiri madereva wasomi.

Alisema hilo litasaidia kuwa na uhakika na kupunguza ajira bandia. Kuhusu nyaraka zinazoghushiwa, Ngewe alisema wameona inatosha sasa kuendelea na teknolojia hiyo badala yake sasa wanatafuta ufumbuzi kwa kutumia vifaa vya kielektroniki ambavyo havighushiwi.

Pia alisema wataendesha kampeni ya nchi nzima kuelezea madhara ya ulevi wakati wa kuendesha magari, lengo ni kutaka wananchi kuwa na uelewa utakaowazesha wapige simu Sumatra kwa mabasi yote ambayo yataenda mwendo kasi.

Kuhusu safari ndefu kama kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kutakuwa na kituo cha kubadilishana madereva ambacho kitakuwa ni Manyoni.

“Hapa dereva atakayetoka Dar es Salaam hataiona tena Mwanza, atakomea Manyoni kulisubiri basi hilo kesho litakapogeuza.”

Taboa Katibu Mkuu wa Taboa, Ernea Mrutu alitaja sababu za ajali ni mabasi kutojali ratiba, miundombinu mibovu, barabara kuwekwa lami inayoteleza dereva anapokanyaga breki gari halisimami, vipuri feki ni vingi kwenye soko kwa sababu eneo hilo limeachwa tu bila mkaguzi.

Kuhusu ratiba za mabasi, Mrutu alikiri kuwa kuna udhaifu mkubwa wa usimamizi kwa upande wa Polisi ambao wanawaachia madereva kutokana na kuwapa rushwa.

Alitaja hatua walizochukua kama Taboa baada ya kubaini kuwa sekta ya usafirishaji ina matatizo makubwa ni kuwaandikia barua baadhi ya madereva ili wazungumze nao lakini madereva wengi hawakuhudhuria kwa sababu wamiliki wa mabasi yao sio wanachama wa Taboa.

Kamanda Mpinga
Kamanda wa Usalama barabarani Mohammed Mpinga alisema matukio ya ajali yanaweza kudhibitiwa iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kuanzia dereva, mmiliki, wasafiri na waendao kwa miguu na Jeshi la Polisi ambao wana wajibu wa kusimamia sheria.

Mpinga alisema Polisi wameona kuna maeneo yenye matatizo kama leseni na akasema wanalifanyia kazi, ukaguzi wa magari ambako alisema wanaandaa kanuni zinazoelekeza kila gari likaguliwe na pia upande wa madereva wametengeneza kanuni ambazo zitatumika wakati utoaji wa leseni za kisasa.

Mpinga alisema wanatengeneza kanuni ambazo zitawalazimisha madereva kwenda kusoma tena kwani wamebaini kuwa madereva wengi wamesoma kidogo na hawaendi tena vyuoni.

Alisema kuna haja ya madereva hao kwenda shule tena kwa ajili ya kujikumbusha yale ambayo wamesoma miaka ya nyuma.

Kuhusu mwendo kasi pamoja na kutumia speed radar (tochi), Mpinga alisema wana mpango wa kupata tochi za kisasa ambazo zinaona hata namba ya gari na pia wanatafuta vifaa vya kupima mwendo kasi wenyewe bila askari kuwepo barabarani.

Madereva
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Usafirishaji kwa njia ya barabara Tanzania (TARWOTU), Shukuru Mlawa ambaye ni dereva alisema wamiliki wa mabasi watengeneze mazingira mazuri ya dereva kujitambua na sio kuwanyooshea vidole madereva ambao kazi yao ni ngumu.

Alipendekeza mikataba ya madereva iboreshwe vizuri na wizara ya kazi waisimamie. Alisema kwa sasa mikataba ya sasa inasimamiwa na vishoka ambao ndio wanaoenda wizarani na Sumatra kufanya mikataba feki wakati madereva wanaoendesha mabasi wenyewe hawana mikataba yoyote.

Alisema madereva wenyewe wamefanya utafiti na kubaini kuwa kati ya madereva 3,600 ni madereva wa kampuni moja tu ya ABC ndio wana mikataba halali.

“Hawa madereva wengine wako wapi? Alihoji dereva huyo. Mangu faini IGP Ernest Mangu alisema kama madereva na wamiliki faini za barabarani zinawauma waheshimu sheria. “Sisi ni serikali hatuwezi kuwaachia tu mfanye mtakavyo.”

Aliwashauri madereva kutii sheria bila shuruti na akasema faini zote zinazotozwa na polisi ni halali.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: