BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWENYEKITI WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA AWAPACHIKA JINA LA KUWAKEJELI UKAWA, AELEZA VIONGOZI WAO WANAVIPAJI VYA UIGIZAJI.

 
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.

VITA ya maneno kati ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), imeendelea na safari hii Sitta amewaita viongozi wa kundi hilo kuwa wana vipaji vya uigizaji kwa namna wanavyotoa matamko yao.


Kauli hiyo ya Sitta inatokana na Ukawa kutangaza kuwa wako tayari kumshitaki Mwenyekiti huyo wa Bunge Maalumu kwa madai kwamba kitendo chake cha kugoma kuahirisha Bunge, ni sawa na kuchochea machafuko kwenye nchi na anaweza kushitakiwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita.

Jana Sitta alijibu tuhuma hizo na kusema viongozi wa Ukawa wana kipaji dhahiri cha uigizaji, kutokana na alivyoita vituko vyao wanavyofanya tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba, ambavyo alidai vinadhihirisha kauli yake kuwa ni ya kweli.

Vituko Ukawa
Alitaja baadhi ya vituko vyao, kuwa ni walipokutana mjini hapa kwa siku 18 wakavutana juu ya upigaji wa kura uwe wa siri au wazi, ilipofika siku ya kukubali kanuni hizo, wajumbe wa kundi hilo ambao walipigania kufa kupona kura ziwe za siri, wakaamua kupiga za wazi.

Baada ya kituko hicho, Sitta alisema kilifuata kingine cha kumtumia mwenzao mmoja, kupeleka hoja binafsi kwamba Bunge hilo lisiendelee, hadi hati ya Muungano ipatikane; Serikali ilipopeleka nakala, wakasema inaweza kughushiwa saini ya Mzee Abeid Karume.

“Tarehe 16 Aprili ilipokuja hati halisi ya Muungano wakasusa Bunge na kutoka nje hadi leo, sasa majuzi Rais kama tunavyomfahamu alivyo muungwana, akakutana nao mara mbili kwa saa saba, namshukuru sana Cheyo (John, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia, TCD), amewaumbua kwa ajili ya maafikiano waliyofikia. “Wametoka hapo (katika mkutano na Rais), siku moja tu baadae wamekana yote yaliyotokea hapa Dodoma waliyofanya mbele ya Rais, kwa hiyo wananchi waendelee kuwapima watu hawa, mimi nashindwa kuwaelewa kabisa,” alisema Sitta.

Fani yao

Sitta alisema kule Marekani kulipata kutokea viongozi wacheza sinema kama Ronald Regan, Rais wa 40 wa Marekani na Gavana Arnold Schwarzenegger wa California ambao walifanikiwa kuongoza taifa hilo kwa sababu ni matajiri na wananchi waliwahimili licha ya kufanya mizaha.

“Lakini sisi ni nchi maskini, hatuwezi kuhimili viongozi wa namna hii kabisa, wananchi wajue hilo…Kwa hiyo mimi natoa ushauri tu kwamba mwakani watakaposhindwa vibaya uchaguzi kwa tabia zao hizo hizo, basi warejee katika fani ambayo Mwenyezi Mungu kawajalia, nayo ni uigizaji,” alisema Sitta.

Wakati wa asubuhi, Sitta alitumia muda huo kujibu tuhuma alizoita zimetolewa na msomi mmoja, kuwa kuruhusu wajumbe kupiga kura, ni kuvunja Katiba ya nchi na kuongeza kuwa kinachofanywa na Bunge hilo, ni kupiga kura ya uamuzi kuhusu suala ambalo wajumbe hao wana haki ya kupiga kura na kushiriki kuamua kuhusu Katiba inayopendekezwa.

Alisema ndio maana hata wakati wa kamati, walipigisha kura hata kwa wajumbe ambao walikuwa wamelazwa hospitalini na akasema hilo ni jambo tofauti na kura ya kufanya uchaguzi.

Aliwataka wajumbe hao wasifadhaike kwani watu huko nje wameamua kujisemea lolote.

“Kuna watu wanaojiita wasomi nadhani wanahusiana na hao wanaojiita Ukawa ambao jitihada yao kubwa kwa sasa ni kuzuia kabisa isipatikane katiba…leo nimemsikia mmoja anasema kwamba kupiga kura itakuwa Sitta anavunja katiba ya nchi, huyu mtu kasema kura ya uchaguzi sisi hapa hatupigi kura ya uchaguzi tunapiga kura ya uamuzi,” alisema Sitta.

Dovutwa
Akizungumza jana bungeni hapo, mwakilishi wa vyama visivyo na wabunge, Fahmi Dovutwa ambaye alishiriki kwenye mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na TCD, alisema amepokea simu za vitisho za kudhuru maisha yake kutokana na tuhuma zilizotolewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kumwita kuwa yeye ni kibaraka wa CCM.

Dovutwa alisema analaumiwa zaidi hususani katika hotuba ya Maalim Seif, kwamba ni miongoni mwa vibaraka ambaye ameteuliwa katika kundi la 201 na akasema anashangaa wakati kwenye kundi hilo kuna Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama wengine wa vyama vinavyounda kundi la Ukawa.

“Kutokana na jina langu kuhusishwa na usaliti kuwa mimi ni kibaraka, nimepokea simu tatu za kutishiwa maisha kwamba watanifanyizia,” alisema Dovutwa na akaonesha kushangaa yeye Dovutwa na chama chake iweje wahujumu, CUF, Chadema na vyama vingine.

Alisema kama Ukawa hawakuridhia makubaliano hayo, walikuwa na fursa ya kuomba muda wa kwenda kufanya mashauriano halafu ndipo wajitokeze kusema hayo waliyotangaza hadharani.

Alisema katika kikao cha tarehe 8 mwezi huu, walikubaliana kwamba kufanyike marekebisho machache yanayohusu mambo ya uchaguzi.

Kuhusu Bunge la Katiba, Dovutwa alibainishwa kwamba kwenye kikao cha kwanza ilifika wakati Rais Kikwete alimhoji Tundu Lissu, kwamba iweje amtake Rais avunje Bunge, wakati yeye ndiye aliyesimama kupinga Rais asihusishwe kwenye sheria ya kuanzishwa kwa mchakato huo.

Dovuta aliendelea kutoa siri za kikao hicho kuwa Rais aliwaeleza wajumbe wa TCD kuwa alijua kuwa mjadala huo ungefika sehemu ukwame na alitakiwa awepo mtu wa kuukwamua na akamtaka Lissu amwoneshe sheria atakayotumia, akashindwa na hakukuwa na jibu.

Alisema kuhusu Bunge Maalumu, walikubaliana isihusishwe CCM wala Rais, bali ihusishe TCD ili watoke kwa umoja wao wende kwa wananchi na wawaambie sababu ya kuahirisha Bunge, halafu kwa umoja huo waende bungeni wawaambie wajumbe sababu ya kuahirisha Bunge.

“Lakini viongozi wa Ukawa wanaona kukanyaga mlango wa Bunge ni sawa na kurudia kunyonya, hapo walikuwa ni wakali,” alisema na akahoji “Kama hawako tayari kusimama mbele ya wajumbe wenzao kuwashawishi wavunje Bunge, nani atakuwa tayari kulaumiwa kwa kulivunja Bunge hilo?

Alisema suala pekee ambalo walikubaliana Rais alisimamie ni kuona Bunge linamaliza muda wake Oktoba 4.

Aliongeza kuwa kama Ukawa hawakuwa tayari, wangemwomba Rais akashauriane na vyama vyao halafu wangetoa tamko, kwani kitendo cha kukanusha makubaliano yaliyosomwa kwa waandishi wa habari, ni hatari kwa umoja wa taifa hili.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: