BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MZAZI MZUIA MWANAFUNZI WA DARASA LA SABA ASIFANYE MITIHANI YA TAIFA YA DARASA LA SANA, AHOFIA KUFAULU NA KUKWAMA KUMUOZA.

 
Wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam wakishangilia baada ya kumaliza mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi shuleni hapo jana. Wanafunzi wa darasa la saba nchini kote, walimaliza mtihani huo jana, waliofanya kwa siku mbili. (Na Mpigapicha Wetu).

WAKATI wanafunzi wa darasa la saba juzi na jana walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, mzazi mmoja mkazi wa Bukombe, amejikuta akiingia matatani na vyombo vya dola kutokana na kumzuia binti wake asifanye mtihani, kwa kile kinachoelezwa alihofia akifaulu angekwamisha mpango wake wa kutaka kumuozesha.


Mwanafunzi aliyezuiwa (jina tunalo) alikuwa anasoma Shule ya Msingi Ihulike iliyoko Kata ya Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita.

Hayo yalithibitishwa na Ofisa Elimu ya Msingi wilayani Bukombe, Shadrack Kabanga akisema walipokea taarifa ya ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa wasamaria, ukisema mzazi mmoja amemzuia bintiwe (anamtaja jina) asifanye mtihani kwa hofu ya binti huyo kufaulu na kupata fursa ya kuendelea na masomo, jambo ambalo mzazi hakulipenda, kwani dhamira yake ni kumuozesha.

Anasema taarifa hiyo ilipokelewa Septemba 10, siku ya kwanza ya mtihani huo wa siku mbili na kwamba walipokwenda katika shule anayosoma binti huyo, walithibitishiwa kutokuwepo kwa mwanafunzi aliyetajwa.

“Majira ya saa kumi za jioni nilikwenda shuleni Ihulike kujiridhisha na kukuta kweli mwanafunzi huyo hakuwepo shuleni kushiriki na wenzake kufanya mtihani ingawa alikuwa amejiandaa na hata dawati la kufanyia mtihani alishapewa,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, alilazimika kwenda Polisi alikopewa askari waliokwenda hadi nyumbani kwa mzazi na kumtia mbaroni, anasubiri kusomewa mashitaka wakati wowote kuanzia leo.

Aidha, Kabanga alisema mwanafunzi huyo jana alitarajiwa kufanya mtihani uliosalia kwa kuwa bado ameonesha nia ya kutaka kufanya hivyo.

Ofisa Elimu huyo ametoa wito kwa wazazi wote wenye tabia kama hiyo waache mara moja kuzuia fursa za kusoma za watoto wao, kwani Serikali imejipanga kukabiliana na wazazi wanaokwamisha elimu kwa watoto wa kike.

“Huyu atachukuliwa hatua ili awe mfano kwa wengine wenye tabia ya kutaka kusaka utajiri wa haraka kwa kuozesha mabinti zao wanaostahili kuwapo shuleni,” alisema Kabanga.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha amelaani vikali kitendo hicho, akisema: “Sisi kama Serikali ya Wilaya na Serikali Kuu kwa ujumla wake tunakemea vitendo vya wazazi kama hawa wanaozuia jitihada za Serikali kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu.”

Aliongeza kuwa, Serikali haitavumilia vitendo kama hivi hasa katika maeneo ya wafugaji, wachimbaji wa madini, watu wanaohamahama ovyo ili kuharibu utaratibu wa elimu.

Aidha, Mwenegoha alisema kwa kuwa mtoto huyo ameshindwa kufanya mtihani wa awali, Serikali itahakikisha anafanya mtihani wake wote baada ya kutengewa siku yake ya kufanya hivyo, huku mzazi wake akisubiri kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kumzuia mwanafunzi kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu ya msingi.

Jumla ya wanafunzi 3,731 wilayani Bukombe walitarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi uliofanyika kote nchini kwa siku mbili kuanzia Jumatano ya Septemba 10, mwaka huu.

Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo hakupatikana kuzungumzia suala hilo ingawa baadhi ya wasaidizi wake, walikiri kuwapo kwa tukio hilo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: