BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WADAU WAMPONGEZA KIKWETE KUKUTANA NA VIONGOZI WA UKAWA.


WADAU wamepongeza hatua ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa juu wa vyama vya siasa. Lakini, wameonya wahusika kuacha misimamo ya kivyama na kuhakikisha wanakamilisha vikao vyao kwa kuimarisha umoja wa kitaifa.

Juzi Rais alifanya mkutano na viongozi hao mjini Dodoma, kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Mkutano huo ulikuwa na ajenda mbili; moja ni mchakato unaoendelea wa kutengeneza Katiba mpya na pili Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mkutano mwingine utafanyika Septemba 8 mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu hatua hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika Idara ya Siasa na Utawala, Audax Kweyamba, alisema hatua hiyo ni nzuri, kwani mazungumzo ni hatua ya kwanza katika sehemu yenye mgogoro.

“Ni hatua nzuri kwani panapokuwa na mgogoro hatua ya kwanza ni mazungumzo. Kwa nilivyofuatilia kwenye vyombo vya habari, inaonesha kuna tatizo la kila chama kushikilia msimamo wake.

“ Ili kuwepo na mafanikio katika mazungumzo hayo, ni vyema kila kundi likaondoa misimamo na kuacha kuweka masharti ya kung’ang’ania serikali mbili au tatu, kwani kufanya hivyo, itakuwa ni kupoteza muda. Kila upande ukubali kupoteza kitu kimoja kwa kupata kitu kikubwa zaidi,” alisema.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye pia ni Mhadhiri katika Idara hiyo, Bashiru Ally alisema hatua ya kiongozi wa juu wa nchi, kutoa nafasi ya kuzungumza na viongozi wa siasa ni ya busara.

Alitaka mazungumzo hayo, yatumike kujadili na kumaliza tofauti.

“Ni nafasi nzuri, kwani badala ya wahusika kutumia njia nyingine nje ya siasa kama maandamano, watumie mazungumzo hayo kuzungumza mambo ya maslahi ya kuimarisha na kujenga nchi,” alisema.

Alisema pia mazungumzo yao yalenge kuimarisha Muungano, kwani kinyume chake itakuwa ni kudhoofisha au kuvunja Muungano, jambo ambalo si jema kwa amani ya nchi.

“Wanatakiwa kuja na mapendekezo ya kuimarisha Muungano, kwani uamuzi tofauti utawafanya hata wanasiasa kutokuwa na maana na kubaki kuwa wanasiasa wa makundi na hawa wako wengi wakitaka mfano, waangalie Sudan Kusini, Libya au Syria,” alisema.

Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa UDSM, Dk. Benson Bana, alipongeza hatua ya Rais Kikwete kuwaita na kuwasikiliza viongozi wa vyama vya siasa. Alitaka Ukawa na washirika wake, kutomlazimisha Rais kuvunja sheria.

“Bunge Maalumu la Katiba linaendeshwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kumshinikiza Rais Kikwete kuvunja sheria si jambo jema, ni jambo baya sana kwa nchi. Tumsaidie Rais ili aendelee kufuata misingi ya sheria,” alisema.

Alisema kama Ukawa wana ushahidi kuwa Bunge la Maalumu la Katiba halifuati sheria, walitakiwa kurudi bungeni, kama walivyotakiwa na wadau mbalimbali na kuomba hoja binafsi au kwenda mahakamani, kutafuta tafsiri ya sheria.

“Ukawa kutorudi bungeni wamejinyima fursa ya kutoa maoni yao, kutekeleza ahadi zao kwa wananchi na kwa hili walipaswa kuwaomba msamaha wananchi,” alisema.

Profesa Kitilya Mkumbo alisema hatua ya mazungumzo hayo ni nzuri na kuwa katika mchakato wa Katiba, kunatakiwa kuwepo kwa majadiliano ya mara kwa mara ;na kinyume chake ni vurugu.

Profesa Mkumbo alishauri wigo wa masuala ya kujadili na wajumbe uongezwe, badala ya kung’ang'ania muundo wa Muungano na wanasiasa.

“Tusing’ang’anie muundo wa Muungano ambao umechangia kuvuruga huu mchakato, tunatakiwa kuangalia kwa upana wake na mambo yaliyo nyuma ya pazia, mfano kama Katiba haitapatikana, je, tuendesheje uchaguzi ujao.

“ Pia wigo wa washiriki kwenye mkutano huo unapaswa kuongezwa, kwani mchakato wa Katiba si wa vyama vya siasa pekee, bali kuna wananchi, viongozi wa dini, taasisi zisizo za kiserikali na wadau wengine,” alishauri Profesa Mkumbo.

Tangu Ukawa wasuse bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, wananchi na makundi mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakitaka wajumbe hao waliosusa, warejee bungeni kuungana na wenzao waliobaki, kutengeneza Katiba yenye maridhiano.

Licha ya kuwepo sauti za kusihi kundi hilo, kurejea bungeni, pia wapo ambao wamekuwa wakisisitiza maridhiano kati ya makundi ya Ukawa na Tanzania Kwanza yapatikane, ili kuunda Katiba yenye ushiriki wa makundi yote.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: