Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.PICHA|MAKTABA
Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amesema hawezi kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu baadhi ya wajumbe wa umoja huo hawautaki Muungano na wamejificha nyuma ya pazia la kutaka muundo wa serikali tatu.
Amesema si kila mtu anayetaka serikali tatu anaupenda Muungano na kusisitiza kuwa ni aibu kuwa na marais watatu ndani ya nchi moja.
“Msimamo wangu wa serikali tatu si msimamo wa marais watatu kwa sababu najua msimamo wa marais watatu utavunja nchi. Msimamo wangu ni rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Mkuu wa Serikali Zanzibar na Mkuu wa Serikali Bara,” alisema.
Zitto ambaye alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya Chadema, moja ya vyama vinavyounda Ukawa, alitoa ufafanuzi huo wiki iliyopita katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam.
Pamoja na Chadema, Ukawa inaundwa na vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi pamoja na wajumbe wachache wa Kundi la 201 ambao walisusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba tangu Aprili 16, mwaka huu, wakitaka ijadiliwe Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba yenye kupendekeza muungano wa serikali tatu badala ya mbili zinazopendekezwa na CCM.
Akieleza sababu za kutoungana na Ukawa, Zitto alisema baadhi ya wajumbe wake wanasema njia nyepesi ya kubakia na Zanzibar ni serikali tatu, wengine wanasema njia nyepesi ya kubakia na Tanganyika ni serikali tatu, “Binafsi ni muumini wa Muungano na dola duniani kote hazivunjwi, bali zinaimarishwa.”
Kuhusu muungano anaoupendekeza alisema: “Chama chenye wawakilishi wengi kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar kitatoa Mkuu wa Serikali Zanzibar na chama chenye wabunge wengi Baraza la Wawakilishi Tanganyika kitatoa Mkuu wa Serikali Tanganyika na Bunge liwe moja.”
Alisema anachofikiria ni namna ya kuzifanya nchi za Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya zinakuwa pamoja na Tanzania na si kujadili namna ya kuzitenganisha na Tanzania.
“Tumeona Ethiopia na Eritrea zilivyotengana. Nini kimetokea pale Wasudani walipoamua kujitenga wenyewe kwa wenyewe. Tujifunze kwa mifano hii, hatuwezi kuwa na wakuu wa nchi watatu ndani ya nchi moja, tutachekwa na dunia. “Lakini kwa sababu wenye sauti za kuukataa muungano ni wengi zaidi katika Ukawa lakini hawawezi kujionyesha, mimi siwezi kuwa nao na nipo wazi kabisa.”
Alisema Ukawa walimwalika katika vikao Dodoma wakati Bunge la Katiba linaanza lakini aliwakatalia na kuwaeleza kuwa miongoni mwao wapo wanaotaka muungano uvunjike.
Kuhusu kuingia bungeni alisema: “Siendi katika vikao vya Bunge la Katiba kwa sababu ni kupoteza muda tu. Huwezi kutengeneza Katiba ya nchi bila maridhiano. Lazima mridhiane ndipo mkae mtengeneze. Katiba haina mshindi.”
Alisema kitendo cha baadhi ya wajumbe kususia vikao na wengine kuendelea si jambo la kufurahia kwa kuwa Katiba inaweza kupata uhalali wa kisheria lakini ikakosa uhalali wa kisiasa.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / ZITTO KABWE !!!! SIWEZI KUJIUNGA NA UKAWA KWA SABABU BAADHI YA WAJUMBE HAWAUTAKI MUUNGANO, WANAJIFICHA KATIKA PANZIA LA KUTAKA MUUNDO WA SERIKALI TATU.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment