JAKAYA KIKWETE KUWASULUHISHA RAIS WA SUDAN KUSIN SALVA KIIR NA HASIMU WAKE RIEK MACHAR ARUSHA.
Arusha. Rais Jakaya Kikwete leo ataongoza mazungumzo ya maridhiano baina ya makundi yanayopingana ndani ya chama tawala cha Sudan Peoples Liberation Movement (SPLM) cha Sudan Kusini.
Mazungumzo hayo yatakayofanyika mjini hapa, yatamshirikisha rais wa nchi hiyo, Salva Kiir na hasimu wake, aliyekuwa makamu wa rais, Riek Machar.
Katibu mkuu wa CCM, Abrahaman Kinana alitoa taarifa hiyo alipozungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema makundi hayo yametambua matatizo yaliyotokea ndani ya chama hasa kwa viongozi, hivyo lengo lililopo sasa ni kurejesha amani na umoja miongoni mwa wanachama na wananchi wa Sudan Kusini.
“Mazungumzo na maelewano rasmi yataanza Jumatatu (leo) ili kurejesha mshikamano ndani ya chama hicho,” alisema.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan Julai 2011 na kuwa nchi huru, lakini Desemba mwaka jana vita ya wenyewe kwa wenyewe viliibuka na kusababisha mgawanyiko kwa chama hicho cha SPLM.
Akizungumza hivi karibuni katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 15 ya Mwalimu Julius Nyerere, Rais Kikwete alisema hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa SPLM, hasa mwenyekiti wake, Rais Kiir kuiomba Tanzania kusaidia jitihada za kisiasa za kupatanisha pande ambazo zinavutana na kutofautiana ndani ya SPLM.
Alisema wanaamini kuwa mapatano ndani ya chama yatafanikisha kumaliza mgogoro wa kisiasa katika serikali ya nchi hiyo changa duniani.
Rais Kikwete alisema kuwa usuluhishi huo utafanywa katika misingi ya kichama kwa CCM kuongoza mazungumzo hayo. Alisema lengo la Tanzania kukubali kuwasaidia ndugu zao wa Sudan Kusini ni kutimiza wajibu wake wa kimataifa.
Tanzania ni kati ya mataifa yaliyopeleka majeshi darfur nchini Sudan kulinda amani kutokana na mgogoro wa kisiasa kati ya Serikali na makundi ya waasi.
Majeshi hayo ya kulinda amani yako chini ya Mpango wa Umoja wa Mataifa.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment