BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAKADA WAOTAJWA KUWANIA URAIS NDANI YA CCM 2015, WAGAWA FEDHA KWA NJIA YA RUSHWA KATIKA MKUTANO WA NEC UKUMBI WA WHITE HOUSE MJINI DODOMA


Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wakiwa katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa White House mjini Dodoma juzi na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Picha na Ikulu.


Dodoma.
Baadhi ya makada wa wa CCM wanaotajwa kuwania urais kupitia chama hicho wanadaiwa kugeuza mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), kuwa sehemu ya kampeni kwa wajumbe wa mkutano huo wakidaiwa kumwaga fedha usiku kucha.


Gazeti hili lilishuhudia kampeni hizo zikifanywa na wapambe wa wagombea hao nje ya Ukumbi wa Nec uliopo nje ya jengo la White House mjini Dodoma na baadhi ya watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo.


Wapambe hao kwa siku mbili za vikao vya Nec vilivyofanyika mjini hapa kuanzia juzi walionekana wakifika mapema, kusalimia, kujitenga katika makundi madogomadogo na wajumbe wa Nec tofauti na vikao vingine vilivyotangulia.


Harakati hizo hazikuishia katika viwanja hivyo, bali hata nje ambapo mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo kutoka Kanda ya Ziwa ameonekana kukutana na makatibu wa CCM katika moja ya hoteli mjini hapa.


“Huyu jamaa amekutana na makatibu wa CCM mara nyingi katika kile kinachoelezwa kuwa ni kusaka wajumbe ili wasijiunge na kambi nyingine,” kilieleza chanzo chetu.


Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema bado hajazipata taarifa hizo na kwamba kama kuna vitendo vya rushwa vinafanyika ni nje ya mazingira hayo.


Alisema katika mazingira kunapofanyika kikao cha Nec, si rahisi kuwapo vitendo hivyo.


“Sasa kama wanapeana barabarani mimi itakuwa ni vigumu sana. Mimi ninashughulikia na mambo ya humu ndani (kikao cha Nec),”alisema na kuongeza:


“Leteni taarifa nilikuta fulani anagawa ama fulani anapokea, haya maneno ya jumla hivi yanaweza kuwa ni mkakati wa kupaka chama matope,” alisema.


Alisema kama inagawiwa usiku wakati yeye akiwa amelala hawezi kufahamu.


Makatibu na wenyeviti wa CCM wa wilaya wanaingia katika Nec kwa mujibu wa vyeo vyao.


Tayari hali hiyo imelalamikiwa na baadhi ya wajumbe wa Nec, wakisema inakitia aibu chama.


Mmoja wa wajumbe wa Nec, Juma Kilimbah, alisema kitendo cha kufanya kampeni ya kutaka kuungwa mkono ni kinyume cha maadili ya chama.


“Mimi sijafuatwa lakini kama kuna watu wanafanya kampeni ya kutaka kuungwa mkono wakati chama hakijatangaza kuanza kwa mchakato ni kinyume cha maadili ya chama,” alisema.


Rushwa hiyo inadaiwa kufanywa na waratibu wa kundi moja linalomuunga mkono mmoja wa vigogo nchini, ambaye anatajwa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.


Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kumekuwa na waratibu kutoka kanda mbalimbali ambao waligawanywa katika makundi manne na walikuwa wakitoa fedha kwa baadhi ya wajumbe wa Nec ili wamuunge mkono ‘mgombea’ huyo.


Rushwa hiyo imekuwa ikitolewa kwa usiri mkubwa na mmoja wa viongozi wa chama hicho ambaye aliwahi kufanya kazi mkoani Dar es Salaam, anaelezwa kuwajibika katika kuwapeleka wajumbe wa Nec ili wakalipwe kwa mmoja wa waratibu wa mpango huo ambaye imedaiwa ni mmoja wa mawaziri.


Kwa mujibu wa chanzo chetu, wajumbe hao walikuwa wakipewa shilingi milioni moja kama ushawishi ili wamuunge mkono ‘mgombea’ huyo.


Hata hivyo, habari za kutolewa kwa rushwa hizo zilivuja mara baada ya mmoja wa waratibu wa mpango huo kutoka kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuwapa wajumbe Sh700,000 badala ya shilingi milioni moja, jambo ambalo liliwachefua wajumbe waliopunjwa mgawo huo.


Wajumbe waliolengwa zaidi ni wale walioonyesha nia ya kuhamia kwenye kundi la mgombea mwingine, anayeonekana kuwa na nguvu zaidi ya wenzake.


Kwa mujibu wa chanzo chetu, kampeni za kutafuta wajumbe wa Nec wanaowaunga mkono, zinalenga katika mmoja wa watu wanaotajwa kuwania urais kuwa na uhakika wa kupata kura zaidi 190 kati ya wajumbe 370 wa Nec.


Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu madai hayo, Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa Mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga, alisema hawajapokea madai yao.


Hata hivyo, aliahidi kufanyia kazi taarifa alizozipata kutoka kwa mwandishi wa habari.


“Hatujapata madai hayo lakini kutokana na swali lako tunalichukulia kama taarifa ya kuanza kufanyia kazi,” alisema.


WanaCCM ambao wamekuwa wakitajwa kuwania urais ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Frederick Sumaye.


Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.


Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta. Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.


Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.


Tayari CCM imeshawafungia kufanya kampeni baadhi ya makada wake walioonekana kuanza kufanya kampeni kabla ya muda.


Waliotangazwa kufungiwa na kuwekwa chini ya uangalizi ni Lowassa, Membe, Makamba, Ngeleja, Wasira na Sumaye.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: