TAKUKURU YAELEZA KUWA VIJANA NI WAATHIRIKA WAKUBWA WA RUSHWA.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema kuwa vijana ndiyo waathirika wakubwa wa madhara yanayotokana na vitendo vya rushwa, kwa kuwa ni kundi kubwa linalohusika kila sehemu ndani ya jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Stella Mpanju, wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la mapambano dhidi ya rushwa jijini Dar es Salaam.
“Katika nchi yetu vijana ndiyo kundi kubwa linaloathirika kwa rushwa hivyo wanapaswa kutumia fursa hii kwa ajili ya maendeleo ya jamii na si kunyosheana vidole, bali ni wakati wa kutibu vidonda na makovu ya rushwa kwa kuwawajibisha wapokeaji na watoaji na kusimamia misingi na maadili mema,” alisema Mpanju.
Kwa mujibu wa Mpanju, katika kundi hilo wamo wanafunzi, wafanyabiashara wadogo, wajasiriamali, watafuta ajira, wauzaji na wanunuzi.
Alisema Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa asilimia 34.7 ni Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 na 35, asilimia 17.5 ni Watanzania wenye umri kati ya miaka 36 na 64, ikiwa na maana ya kwamba asilimia 52.2 ya Watanzania wako chini ya miaka 65.
Alisema hadi Agosti mwaka huu, wameshafungua klabu 2,517 zenye wanachama 181,062 katika shule za msingi, klabu 4,032 zenye wanachama 272,079 katika shule za sekondari na klabu 85 zenye wanachama 9,643 katika taasisi na vyuo vya elimu ya juu. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment