TANZANIA KUSITISHA WAGONJWA KWENDA NJE YA NCHI KWA AJILI YA HUDUMA YA UPASUAJI WA KICHWA 2015.
PICHA YA MAKTABA.
Wagonjwa wanaohitaji huduma ya upasuaji wa kichwa, uti wa mgongo na nyonga kuanzia mwakani hawatapelekwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya serikali kukamilisha jengo la hospitali ya magonjwa hayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk. Othman Kiloloma, alisema jengo hilo lenye ghorofa saba limegharimu Sh. Bilioni 17.6 hadi kukamilika kwake.
Alisema hospitali hiyo mpya ya MOI, itakuwa na vifaa vya tiba vya kisasa vyenye thamani ya Sh. Bilioni 12 na itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 350 kwa wakati mmoja.
Dk. Kiloloma alikutana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa ajili ya kuitambulisha rasmi hospitali hiyo pamoja na kuelezea mikakati yao ya utoaji wa huduma.
Alisema kwa miaka mingi wamekuwa wakiongeza ufanisi wa utoaji wa tiba kuhakikisha huduma ya upasuaji inakuwa bora.
Alisema kwamba kwa sasa matatizo ya ubongo, mgongo, mifupa ya nyoga yanapatiwa matibabu hapa nchini kwa asilimia 95. “Sisi kama MOI tumejipanga kuhakikisha tunazalisha madaktari wengi wa mifupa na ubongo ili tuweze kukabiliana na wingi wa watu wanaopata ajali,” alisema Dk. Kiloloma.
Hata hivyo alitaja baadhi ya changamoto walizonazo kuwa ni ukosefu wa pesa, ongezeko la ajali za barabarani unaosababishwa na uendeshaji mbaya wa bodaboda.
“Katika kuondoa msongamano tumeamua kuweka nguvu zetu kwa kuanzisha matibabu katika Hospitali za Wilaya na Mikoa, huko tutawatibu wananchi wengi,” aliongeza kusema.
Aidha kwa upande wa serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Tiba asili na mbadala, Paulo Mohame, ambaye alimwakilisha naibu Waziri wa Afya na Istawi wa jamii, Dk. Stephene Kebwe, alisema serikali itaendelea kuisaidia taasisi hiyo kwa kupanua wigo wa utendaji kazi wao.
Alisema mpango walioweka wa kufungua matawi katika Hospitali za Wilaya na Mikoa itasaidia kwa kiwango kikubwa kutoa matibabu kwa gharama nafuu na kwa wakati.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment