BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIBWEKA VYA WAZIRI WA RAIS JAKAYA KIKWETE !!! AWATIMU WALIMU WA SEKONDARI WALIOTAKA KUPIGA NAYE PICHA YA PAMOJA MOROGORO.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, amewawekea ngumu walimu wa Shule ya Sekondari Mafiga ya Manispaa ya Morogoro kupiga nao picha ya ukumbusho.

Amechukua uamuzi huo baada ya kubaini pamoja na uwingi wao uliofikia walimu 68, wameshindwa kufaulisha wanafunzi wengi na kuifanya shule kuambulia daraja `sifuri’ kwa namna ya kutisha.

Katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana kati ya wanafunzi 226 waliopata daraja sifuri ni 179.

Waziri Ghasia alikuwa katika ziara ya siku moja juzi katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro iliyomfikisha hospitali ya wilaya inayojengwa eneo la Mkundi, Stendi ya Mabasi Msamvu, Ushirika wa Wazalishaji wa Maziwa Bigwa, Shule ya Sekondari Mji Mpya na Mafiga.

Akiwa shuleni Mafiga, baada ya kujionea shughuli mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya maabara, kabla ya kuondoka shuleni hapo aliombwa na uongozi wa shule ili kupinga picha ya pamoja walimu wa shule hiyo, lakini kabla ya kulikubali ombi hilo alitaka kwanza wamfahamishe maendeleo ya taaluma na ufaulu wa wanafunzi wa sekondari hiyo.

Katika taarifa ya matokeo ya ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne kwa mwaka wa masomo uliopita, ilionesha kuwa wanafunzi 179 walipata daraja sifuri, Daraja la tatu walikuwa ni wanafunzi watatu , daraja la pili alikuwa ni mwanafunzi mmoja na hakukuwa na aliyepata daraja la kwanza kati ya watahiniwa 226.

Kwa mujibu wa uongozi wa shule mbele ya Waziri Ghasia, shule hiyo kwa sasa ina jumla ya walimu 68, na vyumba 28 vya madarasa , ambapo inahitaji walimu wanne kwa ajili ya masomo ya sayansi.

Kufuatia taarifa hiyo ya uongozi wa shule hiyo Waziri Ghasia alitakaa ombi la kupiga nao picha na kusema; “ Sipigi picha na nyie hadi mrekebishe kiwango cha ufaulu... shule yenye walimu 68 haijafaulisha vya kutosha...mimi nilitegemea kwa uwingi wenu huu shule hii ingeongoza kwa kufaulisha wanafunzi wengi,” alisema Ghasia huku akiondoka na kuelekea kwenye gari lake.

Kwa mujibu wa Waziri huyo kuwa, shule hiyo yenye vyumba vya madarasa 28 na walimu 68, inaonesha walimu 40 wanakuwa nje ‘ofisi ya walimu’ wakisubiri wenzao wamalize vipindi na wao wapate fursa ya kutumia vyumba hivyo ili kufundisha masomo yao na kuwafanya muda mwingi wakibaki wamekaa bure ‘ kupiga soga’ bila kuwa na vipindi darasani.

“Kwa idadi ya walimu 68, Shule hii walimu hawaingii darasani anakaa muda wa saa sita hana kipindi , jambo hili haliwezi kukubalika, lazima lirekebishwe haraka”, alisema Waziri Ghasia.

Hata hivyo alisema, kutokana na shule hiyo kuwa na jumla ya vyumba vya madarasa 28 na mgawanyo wa walimu ulipaswa kuwa ni 38 , lakini imekuwa na idadi kubwa ya kupindukia.

“Kama shule hii ipo katikati ya mjini na ina walimu wengi na imeshindwa kufaulisha, nina imani hata nyingine zipo kwenye hali hii hapa hakuna ufuatiliaji wa Ofisa Elimu kujua kinachoendelea katika shule za sekondari,” alisema waziri huyo.

Hivyo, akiwa katika majumuisho ya ziara yake hiyo, Ghasia aliuagiza uongozi wa Manispaa kupitia na kufuatilia ufundishaji wa walimu shuleni na pia kuweka mgawanyo wa walimu kulingana na mahitaji ya kila shule.

“Hatusimamii shule ...shule hii ya Mafiga haipo maili 100, ipo karibu, lakini Ofisa Elimu haendi kufuatilia kinachoendelea shuleni, “alisema.

Mbali na hayo pia ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kusimamia vyema ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara kwa kufuata ramani zinazotolewa na pia kuzingatia viwango vyenye ubora unaokidhi thamani ya fedha zinazotolewa baada ya kubaini mapugufu kadhaa kwenye ujenzi wa maabara ya Shule ya Sekondari Mji Mpya.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo, alikiri kuwepo kwa mapungufu katika usimamizi hasa kwa ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule hiyo na kiwango kisichoridhisha cha ufaulu kwa baadhi ya shule za sekondari ikiwemo ya Mafiga.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: